Header Ads

SHAHIDI:BODI BOT HAIKUWAHI KUMLALAMIKIA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

MENEJA wa Masuala ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Justo Tongola (45), ambaye ni shahidi wa pili katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa BoT, Amatus Liyumba, ameieleza mahakama kuwa hajawahi kuona wala kusikia bodi hiyo ikilalamikia utendaji kazi wa Liyumba.

Akitoa ushahidi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, pia alidai hajawahi kushuhudia bodi hiyo ikikataa kuidhinisha maombi ya menejimeti ya benki hiyo wala aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Balali, akilalamikia mradi wa ujenzi wa minara pacha.

Shahidi huyo alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa maswali na mawakili wa utetezi Majura Magafu, Hudson Ndusyepo, Jaji Mstaafu Hillary Mkate, na Onesmo Kyauke mbele ya Jopo la Mahakimu Wakazi linaloongozwa na Edson Mkasimongwa anayesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa.

Ifuatayo ni mahojiano kati ya mawakili wa utetezi na shahidi huyo:
Wakili:Nani alitoa kibali cha Kurugenzi ya Utumishi na Utawala iliyokuwa ikiongozwa na Liyumba, iratibu mradi huo?
Shahidi:Sina hakika sana ila miradi yote inayoangukia kwenye eneo la Capital Expenditure zote zina ratibiwa na ofisi hiyo.
Wakili:Umesema ofisi iliyokuwa ikiongozwa na mshitakiwa ilikuwa ikiratibu mradi huo ,ilikuwa ikifanyakazi hiyo ya uratibu kwa niaba ya Benki Kuu?
Shahidi:Ndiyo.
Wakili:Taarifa za uaandaaji wa taarifa ya mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi zilikuwa zinaratibiwa na ofisi ya mshitakiwa na nani?
Shahidi:Ofisi ya Liyumba na Meneja Mradi Deogratius Kweka ambaye aliajiriwa na Benki Kuu kwa mkataba.
Wakili:Ninani mweingine alihusika katika uaandaji wa hiyo taarifa ya mabadiliko ya ujenzi,ukiacha Kweka?
Shahidi:Hilo sina taarifa.
Wakili:Taarifa ikishaandaliwa zinapelekwa kwenye bodi?
Shahidi:Ndiyo.
Wakili:Ulisema mradi ulikuwa kwenye Capital Expenditure katika kipindi chochote bodi ilikuwa hailidhiki na mabadiliko?
Shahidi:Kuna kipindi bodi baada ya kupokea maombi kadhaa ilikuwa hairidhiki na ilikuwa inarudisha baadhi ya maombi kwa Menejimenti ili zifanyiwe marekibisho kisha zinarejeshwa tena kwenye bodi na bodi inatoa idhini.
Wakili:Kuna kipindi chochote wewe ulivyokuwa kwenye vikao vya bodi kama bodi iliwahi kumlalamikia Liyumba kama Liyumba?
Shahidi:Hilo sijawahi kusikia wala kuliona kwenye vikao ila kuna wakati Menejiment ilikuwa inaondolewa kwenye vikao.
Wakili:Ina maana Gavana na Naibu Gavana waliondolewa kwenye vikao vya Menejimenti?
Shahidi:Hapana, kwani hao ni kwa vyeo vyao ni sehemu ya bodi ila baadhi ya wafanyakazi waliondolewa
Wakili:Kuna sehemu uliona gavana aliwahi kulalamika kuhusu mradi huo?
Shahidi:Mibinafsi sijawahi kuona hilo.
Wakili:Ni kweli kwamba hakuna hata siku moja kikao cha Menejimenti hakijawahi kujadili mradi huo hata mara moja?
Shahidi:Kumbukumbu zangu vikao vya bodi na menejimenti vilivyouzulia mwaka 2000-2007,kwakweli sikumbuki kama menejimenti iliwahi kuzungumzia mradi huo.
Wakili:Ina wezekana kurugenzi ya utawala ipewe jukumu la kuratibu mradi halafu isiujadili?
Shahidi:Menejimenti ipo katika sehemu mbili.Mosi, Gavana ndiye mwenye mamlaka ya kusimamia menejimenti na gavana halazimiki kupeleka kila jambo kwenye menejimenti.
Wakili:Nitakiwa sijakosoe, mambo yanayofayofanywa na utawala lazima gavana awe na taarifa?
Shahidi:I presume so.
Wakili:Na lazima gavana hayabariki?
Shahidi:Ndiyo.
Wakili:Utakubaliana na mimi jukumu la bodi ni kulinda maslahi ya BoT na serikali kwa ujumla yasihujumiwe?
Shahidi:Ni kweli na hilo ni jukumu la kisheria.
Wakili:Kuna kipindi chochote kuna maombi yalipelekwa na Menejimenti kwenye Bodi na bodi ikakataa kuidhinisha?
Shahidi:Sikuwai kushuhudia hiyo la bodi kukataa kuidhinisha.
Awali kabla ya mahojiano hayo Wakili wa serikali Juma Mzarau, Ben Lincoln.Thadeo Mwenepazi na Prospa Mwangamila walimuongoza shahidi huyo kutoa ushahidi wake.Ifuatayo ni mahojiano kati ya wakili Mzarau na shahidi:
Wakili:Kazi zako kubwa pale BoT ninini?
Shahidi:Tangu 1994 nilianza kujishughulikia maswala ya bodi kwa kumsaidia Katibu wa Benki.
Wakili:Katibu wa benki anaitwaje kwenye Bodi?
Shahidi:Katibu wa Bodi.
Wakili:Majukumu yake ninini?
Shahidi:Kuratibu maandalizi ya mikutano ya bodi na menejimenti na kuakikisha wajumbe wanapata madokezi yote na maadhimio yote yanawekwe kwenye maandishi.
Wakili:Unapoingalia Menejimenti ya BoT inasura ngapi?
Shahidi:Kisheria Menejimenti ipo chini ya Gavana kwa hiyo Menejimenti inapotoa maamuzi inamaanisha gavana katoa maamuzi.Menejimenti nyingine ipo chini ya gavana na Naibu Gavana na Wakurugenzi wa Benki hiyo.
Wakili:Je Gavana anapotoa maelekezo uwa anayatoa kwa njia hipi?
Shahidi:Kwa njia ya dokezo.
Wakili:Umekuwa msaidizi wa Katibu wa Bodi wa vikao vyote hivyo,ieleze mahakama approval structure ya bodi iko je?
Shahidi:Bodi ndiyo yenye mamlaka ya kuunda sera na kuzitekeleza na kusheria imepewa jukumu la kupitisha bajeti inapotokea kazi za Benki za kila siku gavana ndiyo mwenye mamlaka ya mwisho ya kutoa maamuzi mbalimbali.
Wakili:Katika BoT kuna matumizi ya fedha ya aina ngapi?
Shahidi:Aina mbili.Aina ya kwanza ni Capital Expenditure(matumizi ya mradi unaotekelezwa na pili ni Current Expenditure) yaani yale ya matumizi ya kawaida kimsingi yanahusu mambo mbalimbali yanayotokea kila siku yanahusu Benki hiyo.
Wakili:Tukianzia matumizi ya Capital Expenditure,sura yake ikoje?
Shahidi:Ni sera iliyopitishwa na bodi na Capital Expenditure inatakiwa ipate kibali cha bodi.
Wakili: Current Expenditure ikoje?
Shahidi:Inapitishwa na bodi na baada ya hapo matumizi yanapitishwa na menejimenti na kuna mengine yanaitaji kibali cha gavana.Kwa hiyo b inapokuja Capital Expenditure gavana hana mamlaka hadi bodi.
Wakili:Jukumu la Menejimenti ni nini?
Shahidi:Kisera ambayo inapitishwa na bodi ,Menejimenti inapaswa kuwasilisha maombi kwenye bodi na baada kupata kibari ndipo inaweza kwenda kuendelea na matumizi.
Wakili:Katika kipindi cha 2000-2008 ulikuwa unaudhiria vikao vya bodi?
Shahidi:Nilikuwa naingia ila kuna baadhi nilikuwa siingii.
Wakili:Kuna vikao vingapi vya bodi?
Shahidi:Vipo vikao vya aina mbili.Kuna kikao cha kinachofanyika kila baada ya miezi miwili na kingine kinafanyika kwa dharula.Vikao vya dharula uitishwa pale tu kuna jambo la dharula linatokea ili bodi ije iidhinishe.
Wakili:Uliwahi kuufahamu mradi mradi wa ujenzi wa minara pacha?
Shahidi:Niliufahamu kwa kuona ukiendelea pia kupitia vikao mbalimbali vilikuwa vikiujadili.
Wakili:Mradi huo ulikuwa ukijadiliwa kwenye vikao vya bodi?
Shahidi:Ndiyo ulijadiliwa.
Wakili:Nini kilichojadiliwa kwenye bodi kuhusu mradi huo?
Shahidi:Menejimenti ilkikuwa inawasilisha taarifa za utekelezaji wa mradi huo na taarifa za mabadiliko ya upanuzi na kuomba bodi itoe idhini.
Wakili:Kibali cha bodi kiliombwa wakati gani?
Shahidi:Wakati mabadiliko ya mradi na matumuzi yalikuwa yameishatekelezwa kwa maana hiyo kibari kilikuwa kinaombwa kwenye bodi ili kubaliki mabadiliko hayo.

Kiongozi wa jopo Edson Mkasimogwa aliarisha kesi hiyo Oktoba 28 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa ambapo siku hiyo watapanga tarehe ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 24, 2009

No comments:

Powered by Blogger.