Header Ads

MAHAKAMA YADANGANYWA

*Wadhamini wawasilisha hati bandia
*Walitaka kuwadhamini vigogo BoT
*Washtukiwa na kusekwa mahabusu

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, jana iliamuru wadhamini watatu waliojitokeza kumdhamini mshtakiwa wa nne katika kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 104 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ally Bakari wakamatwe baada ya kupatikana kwa taarifa kuwa hati walizotumia kumdhamini mshtakiwa ni za kughushi.


Amri hiyo ilitolewa jana mchana na Msajili namba mbili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha, baada ya kukubaliana na maombi ya Wakili wa Serikali, Ephery Fredrick na Proper Mwangamila, waliotoa taarifa za kutolewa kwa hati hizo bandia na wadhamini.

Mawakili hao katika madai yao, waliitaka mahakama isikubali taarifa hizo za udhamini na zisitumike kumdhamini mshitakiwa huyo.

Wadhamini walioamuriwa kukamatwa ambao waliwasilisha hati hizo za dhamana, ni David Majedele, Felix Musa Nyuki na Hamad Juma. Hata hivyo mdhamini wa tatu alitoweka katika mazingira ya kutatanisha hivyo kufanya walioshikiliwa na polisi kubaki wawili.

Hakimu Mlacha alisema, anakubaliana na ombi hilo kwa sababu hati hiyo ya udhamini inaonyesha ilipitia kwa Mthamini Mkuu wa Serikali, kitu kilichodaiwa na mawakili wa upande wa mashitaka kuwa si kweli.

Walieleza kuwa, wanazo taarifa kuwa Mthamini Mkuu wa Serikali hajawahi kutoa hati hizo jambo linaloonyesha kuwa zimeghushiwa.

Tukio hilo lilitokea wakati kesi hiyo ilipokuwa mahakamani jana kwa ajili ya kutimiza masharti ya dhamana.

Majedele aliwasilisha hati na mali namba 105046 kitalu 247 block E Mbezi na taarifa ya uthamini ilikuwa inaonyesha kuwa ina thamani ya sh 369,679,950 wakati upande wa mashitaka ulibaini hati hiyo ilishawahi kupotea na kuripotiwa polisi ambapo ilitangazwa katika gazeti la Daily News la Oktoba 30 na ikatangazwa pia katika gazeti la serikali la Oktoba 24 mwaka jana.

Baada ya kupotea, Majedele alidaiwa kuomba hati mpya ambayo ilionyesha kutolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani, Desemba 10, mwaka jana.
Ilidaiwa mahakamani hapo, hati aliyowasilisha haitambuliwi na serikali na badala yake inayotambuliwa ni hati mpya aliyoomba.

Kwa upande wa Nyuki, aliwasilisha hati ya mali namba 76918 kitalu 74 Gerezani ikionyesha kuwa na thamani ya sh 587,820,000.

Mdhamini wa tatu (Juma) yeye aliwasilisha hati namba 107622 kitalu 40 eneo la Gerezani na jengo lenye thamani ya sh 549,600,000.

Hati zote ziliambatanishwa na taarifa ya Mthamini Mkuu wa Serikali.Lakini baada ya upande wa mashitaka kwenda kuzihakiki katika ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali ilibainika kuwa hazijawahi kutolewa na serikali.

Vyanzo vya kuaminika kutoka serikalini vilidai kuwa, wadhamini hao wanatarajiwa kufikishwa kizimbani leo kwa makosa ya kughushi.

Mbali na Mkonga katika kesi hiyo inayowakabili vigogo hao wa BoT, washitakiwa wengine ni Simon Jengo na Naibu Mkurugenzi Fedha za Nje, Kisima Mkango, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Bosco Kimela pamoja na Mkurugenzi wa masuala ya kibenki, Ally Bakari.

Katika kesi hiyo, washitakiwa wanadaiwa kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2004 na 2007, kuisababishia serikali hasara hiyo kwa kudanganya miongozo kwa kuongeza gharama za uchapishaji wa fedha za noti ikilinganishwa na gharama halisi.
Kesi hiyo ya msingi inasikilizwa katika mahakama ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Oktoba 21, 2009

No comments:

Powered by Blogger.