JAMES KATEKA
Mtanzania wa kwanza kuiongoza ITLOS
Na Happiness Katabazi
MAPEMA mwezi huu, Tanzania iliendelea kung’ara kwenye sura ya dunia baada ya Jaji wa Mahakama Kimataifa ya Sheria ya Bahari (ITLOS), James Kateka, ambaye ni Mtanzania pekee katika mahakama hiyo, kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Taasisi ya Wanasheria wa Kimataifa.
Kutokana na hali hiyo, Tanzania Daima Jumapili ilifanya mahojiano na Kateka kwa njia ya mtandao kutoka nchini Ujerumani ili kujua siri ya mafanikio yake.
Swali: Umeupokeaje ushindi huo?
Jibu: Nimepokea uteuzi huu kwa furaha sana. Hii ni heshima kubwa kutambuliwa na wataalamu wa sheria kimataifa.
Kuchaguliwa kwangu kwa kura nyingi kuliko waliochaguliwa wote (11 kati ya wagombea 28) inaonyesha imani kubwa ya wajumbe wa taasisi hii kwangu.
Pia kuchaguliwa kwangu kushika wadhifa huo kunanifanya niwe mjumbe wa kwanza kutoka Nchi za Afrika Mashariki kujiunga na Taasisi ya Wanasheria wa Kimataifa iliyoanzishwa mwaka 1873 na yenye makazi yake nchini Ubelgiji.
Swali: Tukikuacha wewe, kuna watu wengine waliochaguliwa kuwa wajumbe wa taasisi hiyo?
Jibu: Wajumbe wengine waliochaguliwa ni pamoja na majaji wa mahakama za kimataifa, maprofesa wa vyuo maarufu duniani na wakuu wa vyombo vya utafiti wa sheria za kimataifa.
Na kwa upande wa Waafrika wengine waliochaguliwa kuwa wajumbe ni pamoja na Jaji Abdul Koroma wa Mahakama ya Dunia kutoka Sierra Leone, Jaji Thomas Mensah kutoka Ghana ambaye alikuwa Rais wa kwanza wa ITLOS, Jaji Abdi Yusuf wa Mahakama ya Dunia kutoka Somalia na Profesa John Dugard kutoka Afrika. Kusini.
Binafsi nilichaguliwa katika raundi ya kwanza na nikapata kura nyingi kuliko wajumbe wote waliochaguliwa, katika kikao kilichofanyika Naples, Italia. Walikuwepo wagombea 28 na waliochaguliwa ni 11. Baadhi ya walioshindwa katika uchaguzi huu ni pamoja na Jaji wa Mahakama ya Dunia.
Na wajumbe wengine waliochaguliwa katika taasisi hiyo ni pamoja na majaji wa mahakama za kimataifa, maprofesa wa vyuo maarufu duniani na wakuu wa vyombo vya utafiti wa sheria za kimataifa.
Swali: Unafikiri Tanzania itafaidika vipi na ushindi huo?
Jibu: Kwa vile mimi ndiye Mtanzania wa kwanza kuchaguliwa kwenye taasisi hii, heshima inakwenda kwa taifa lililonilea kwa kunipa nafasi ya kulitumikia katika nyadhifa mbalimbali kwa miaka 35 kabla ya kustaafu.
Pia kuna misimamo inayowekwa na taasisi hii kuhusu maswala mbalimbali ambayo ina faida kwa taifa letu. Kwa mfano katika kikao kilichofanyika Naples, Italia mwezi huu, taasisi hiyo ilipitisha azimio kuhusu vitendo vya uharamia baharini.
Kama mjuavyo, uharamia baharini umekithiri kwenye mwambao wa Somalia. Azimio hili litasaidia katika kufafanua sheria ya bahari na kusaidia kutatua tatizo la maharamia baharini.
Swali: Je utashika nafasi hiyo kwa muda gani?
Jibu: Huu ni uteuzi wa maisha. Ila mtu akibahatika kutimiza miaka 80 anakuwa hana haki ya kupiga kura. Wajumbe walio chini ya miaka 80 hawapaswi kuzidi 132.
Swali: Kitu gani kilikusukuma kusoma sheria?
Jibu: Wakati nilipokuwa nasoma shule ya sekondari Tabora, miaka ya 1960 , baba yangu alikuwa ni mtumishi wa umma... alikuwa ananitumia magazeti yaliyokuwa na picha za majaji wakikagua gwaride kabla ya kuanza mwaka mpya wa mahakama. Kutokana na busara hii ya mzazi wangu, nilianza kuvutiwa kusoma sheria.
Swali: Ni changamoto gani unakabiliana nazo katika mahakama ya kimataifa?
Jibu: Inabidi nisome sana kwani sheria yangu ya kimataifa ilipata kutu wakati nikiwa mwana diplomasia. Bahati nzuri nilisaidiwa na kuwa mjumbe wa Tume ya Sheria ya Umoja wa Mataifa (UN International Law Commission) kwa miaka 10. Pia kwa vile sikuwahi kuwa mwanasheria wa serikali au hakimu au wakili, ilibidi nijifunze upya kuhusu mwenendo wa mahakama na utoaji wa ushahidi. Nilisaidiwa baada ya kuteuliwa kuwa Jaji Maalum wa Mahakama ya Dunia kwenye kesi iliyohusu nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Swali: Unawashauri nini wanasheria wa Tanzania katika kazi zao?
Jibu: Kwa vile nimekuwa nje ya nchi kwa muda mrefu na sijafanya kazi za sheria hapo nyumbani, itakuwa sio busara kwangu kudiriki kutoa ushauri kwa wanasheria wa Tanzania. Pia viongozi na majaji wa mahakama, hasa Mahakama ya Rufani nilisoma nao. Hivyo watajisikia vibaya kuona ‘bush lawyer’ wa kesi za ‘Nyarubanja’ akitoa ushauri kwao. Ila naweza kusema kwa ujumla tu kwamba sote katika kazi zetu tutawaliwe na maadili ya taaluma zetu.
Swali: Tueleze historia ya maisha yako?
Jibu: Nilizaliwa katika Kijiji cha Nyakahanga, Wilaya ya Karagwe April 29 mwaka 1945. Nilisoma darasa la kwanza hadi la nne kwenye Shule ya Msingi ya Nyakahanga kuanzia 1952-1955. Nilifuzu na kwenda kusoma Mugeza Middle School, Bukoba darasa la tano hadi la nane kati ya mwaka 1956 na 1959.
Nilichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Tabora ambayo ilikuwa shule yenye hadhi kubwa na ambayo imetoa viongozi wengi. Nilisoma Tabora kidato cha kwanza hadi cha sita toka mwaka 1960 hadi 1965. Nikahitimu na kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwezi Julai 1966.
Oktoba 1966, tulifukuzwa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, kwa kufanya maandamano ya kupinga masharti tuliyowekewa kuhusu kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa. Hivyo nilipoteza mwaka mmoja. Nikahitimu na shahada na LLB (Hons) Machi 1970. Darasa letu ndilo lilifunga Chuo Kikuu cha Afrika ya Mashariki. Nilisoma na baadhi ya viongozi wa sasa kwenye nchi za Afrika ya Mashariki.
Mwaka huo wa 1970 nilijiunga na Wizara ya Mambo ya Nje mshauri wa masuala ya kisheria kwenye Idara ya Itifaki na Mikataba na wakati huo idara hiyo ilikuwa ikiongozwa na Balozi Daniel Mfinanga ambaye sasa ni marehemu.
Katibu Mkuu wa Wizara alikuwa Balozi Obed Mbogo Katikaza ambaye naye pia ni marehemu. Balozi Katikaza alikuwa ni mchapakazi hodari na aliheshimiwa sana na wafanyakazi. Mwaka 1971, ilianzishwa Idara ya Sheria kwenye Wizara na Mkurugenzi wake wa kwanza alikuwa ni Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye nilifanya kazi naye hadi alipochaguliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pia nilikuwa naye wakati akiongoza ujumbe wa Tanzania katika vikao vya Mkutano wa Sheria ya Bahari kutoka mwaka 1971 hadi mwaka 1982.
Kati ya mwaka 1973 na 1974 nilikwenda kusomea shahada ya pili (LLM) katika sheria ya kimataifa huko King’s College, Chuo Kikuu cha London. Kati ya mwaka 1976 na 1980 nilifanya kazi kwenye ofisi yetu ya kudumu ya Umoja wa Mataifa. Balozi wangu alikuwa ni Dk. Salim Ahmed Salim ambaye nilifanya kazi naye wakati Tanzania ikiwa mjumbe wa Baraza la Usalama (Security Council) mwaka 1975 hadi 1976. Pia alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1979.
Niliporudi nyumbani, nilikuwa mkuu wa sehemu ya mikataba, kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Sheria kwa miaka sita toka mwaka 1983 hadi 1989.
Mwaka 1989 hadi 1994 niliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Ujerumani. Pia niliiwakilisha Tanzania huko Austria, Uswiss Romania, Vatican na Poland. Mwaka 1994 nilihamishiwa Moscow, Urusi nilikokaa hadi 1998 nilipohamishiwa Stockholm, Sweden. Huko niliiwakilisha nchini yangu katika nchi za Denmark, Norway, Finland, Iceland na Baltic Republics (Estonia, Latvia na Lithuania). Nilikaa kwenye nchi za Nordic kwa miaka saba hadi nilipostaafu mwaka 2005.
Kwa bahati nzuri, mwaka huo wa 2005 nilichaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Sheria ya Bahari (iliyoko Ujerumani), wadhifa nilioushikiria hadi sasa.
Nimeoa. Mke wangu Adolphina Gabone ambaye ni mchumi.Tuna mtoto mmoja aitwaye Kahabuka. Yeye ni Mwanasheria.
Swali: Je unaonaje hali ya siasa hapa nyumbani?
Jibu: Kwa vile maadili ya kazi hayaniruhusu kujiingiza kwenye siasa, siwezi kusema mengi. Ila ninafuatilia kwa karibu na kwa undani mambo ya siasa kutoka kwenye mitandao mbalimbali. Kuna mambo mengi yanayoendelea. Ninaona kwamba Watanzania wamekomaa katika mambo ya kisiasa. Hii inatokana na msingi mzuri uliowekwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyetufundisha kuwa jeuri na kutokubali kunyanyaswa na mtu yeyote. Pia wigo wa uhuru wa mawazo umeogezeka chini ya uongozi wa serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Vyombo vya habari na wananchi wanao uhuru wa kutoa maoni kuhusu masuala muhimu ya kisiasa na kijamii bila woga. Kwenye Bunge kumekuwepo mijadala motomoto kuhusu ufisadi. Haya yote ni maendeleo katika kukomaa kwa demokrasia. Ni matumaini yangu kwamba jitihada zitafanywa kuzidi kukuza demokrasia na utawala wa sheria.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Septemba 20, 2009
No comments:
Post a Comment