Header Ads

ZOMBE AANGUA KILIO KORTINI

*Ni wakati akitoa utetezi wake
* Atumia saa nne kujieleza
*Aomba korti itende haki

Na Happiness Katabazi

KATIKA hali isiyotarajiwa aliyekuwa Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe (55), jana aliangua kilio mara kadhaa kizimbani wakati akijitetea dhidi ya kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.

Licha ya Zombe kumwaga chozi kwa mara nne akiwa kizimbani, pia alikuwa akitoa utetezi wake akionyesha kujiamini na kunukuu baadhi ya vifungu vya Sheria ya Jeshi la Polisi(PGO), Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 1985 na Sheria ya Ushahidi.

Akitoa utetezi wake kwa zaidi ya saa nne (saa 4:28 hadi saa 8:06 mchana), Zombe alidai kushangazwa na shahidi wa 36, SACP Sidney Mkumbi kuidanganya mahakama kuwa alikataa kuhojiwa.

Alidai Mei 29 mwaka 2006, aliitwa ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkumbi na kuelezwa aandike maelezo na kudai alihoji ni kwa nini aandike maelezo mara ya pili. Alidai alijibiwa kuwa maelezo ya awali hayakuwapo kwenye jalada.

“Napingana na Mkumbi kuniambia nilikataa kuchukuliwa maelezo, kwani mara ya kwanza ilikuwa ni Machi 3 mwaka 2006, niliandika maelezo yangu kwenda kwa IGP kuhusu tukio hilo la mauaji,” alidai Zombe na kuwasilisha nyaraka hizo mbili za maelezo yake, ili zitumike mahakamani kama kielezo.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili Jerome Msemwa na Zombe.

Wakili:
Shahidi unatambua unakabiliwa na kosa gani?
Shahidi: Natambua, ninakabiliwa na kesi ya mauaji ya watu wanne, ila marehemu siwafahamu kabla, wakati na baada ya vifo vyao.
Wakili: Hebu tuambie ilikuwaje?
Shahidi: Juni 6 mwaka 2006 nikiwa ofisini Makao Makuu ya Polisi niliitwa kwa IGP Said Mwema ambaye alikuwa na makamishna wawili, Kamishana wa Mafunzo,Paul Chagonja na Tweve.
Wakili: Baada ya hapo ilifuata nini?
Shahidi: IGP Mwema aliniambia siku hiyo ningeunganishwa kwenye kesi ya mauaji ya watu wanne. Na wakati akinieleza hayo aliniambia DPP amemwandikia barua kwamba mimi natakiwa kushitakiwa.

Mwema alinipa hiyo barua ya DDP ilikuwa ni barua ya Juni 6 mwaka 2006 ikiwa na kumbukumbu namba DAC/C180/3/DAR/1565/11/2006 ambayo iliandikwa kwa DCI na kwamba DDP alifikia uamuzi huo kwa sababu ushahidi uliopo kwenye jalada unanigusa moja kwa moja mimi.

Wakili: Unakubaliana na yaliyoandikwa kwenye barua hiyo?
Shahidi: Sikubaliani nayo, kwani yamepangwa kwani huyu DPP aliandika barua kwa mshitakiwa wa 3, 4, 7, 9 na 10 tuliokuwa nao gereza la Ukonga na hawa ndiyo walimuandikia barua DPP.

Wakili: Una ushahidi wa hizo barua za washtakiwa walizomwandikia DPP?
Shahidi:Ndiyo, hizi hapa (anaonyesha). Ziliandikwa Juni 3 mwaka 2006, ikiwa ni miezi sita tangu washtakiwa hao wakamatwe na kuweka rumande.
Wakili: Hizo barua za watuhumiwa wenzako kabla ya kwenda kwa DPP zilipitia kwa Mkuu wa Gereza?
Shahidi: Zilipitia kwa mlango wa panya, yaani hazikupitia kwa Mkuu wa Gereza.
Wakili: Kwa ufahamu wako barua za mahabusu zinapaswa zipitie wapi?
Shahidi: Kwa Mkuu wa Gereza.
Wakili: Connection ya barua za DPP na washtakiwa wenzako katika kesi hii ikoje?
Shahidi: Wakati nikiwa RCO nilifungua kesi za madai ya kashfa dhidi ya magazeti sita mahakamani na hadi sasa hazijaanza kusikilizwa.
Wakili: Unazikumbuka kesi hizo na namba zake na magazeti uliyoyafungulia?
Shahidi: Ndiyo, nilifungua kesi dhidi ya gazeti la Alasiri, Tanzania Daima, Halihalisi sasa Mwanahalisi, Mwananchi, Mzalendo na Dar Leo. Nadai jumla ya sh bilioni moja kwa kila gazeti.
Wakili: Ulisema hao marehemu walifariki lini?
Shahidi: Januari 16 mwaka 2006, saa 12 jioni.
Wakili: Wakati huo ukiwa na wadhifa gani?
Shahidi: Kaimu RPC na RCO, ila nilikuwa na wasaidizi sita katika nyadhifa hizo.
Wakili:Kwa upande wa cheo chako cha RCO ulikuwa ukisaidiwa na maofisa gani?
Shahidi:Kwa sasa amepanda cheo ni ACP Charles Mkumbo ambaye alikuwa ni Kiongozi wa Kudhibiti Ujambazi jijini, SSP Nyanda, SP Lulu, ASP Kisai hawa wote walikuwa wakinisaidia.
Wakili: Ulikuwa na kazi maalum wakati unakaimu cheo cha RPC?
Shahidi: Kwa kipindi hicho, nilikuwa nikiongoza msafara wa Rais Jakaya Kikwete katika Pairot Car ambapo rais alipoingia madarakani alikuwa na ziara ya kutembelea wizara zote. Nilikuwa nikiongoza msafara kuanzia Januari mosi hadi 30 mwaka 2006 nilipomkabidhi ofisi Kamanda Alfred Tibaigana na kwenda Rukwa kwenye ofisi yangu mpya.
Wakili: Majukumu ya kila siku alikuwa anatekeleza nani wakati upo kwenye ziara ya Rais Kikwete?
Shahidi: Upande wa ofisi ya RPC ni SSP Mafie na wenzake watano ambao nimewataja na kama jambo limetokea walikuwa wakikabiliana nalo.
Wakili: Kwenye ofisi ya RCO nani anakusaidia wakati aupo?
Shahidi: SSP Mkumbo.
Wakili: Katika wadhifa huo ulikuwa unapata taarifa za uhalifu kutoka kwa wasaidizi wako?
Shahidi: Walikuwa wananipa taarifa ingawa si zote, kwani nyingine walikuwa wakinijulisha.
Wakili: Kipolisi Mkoa wa Dar es Salaam una wilaya ngapi?
Shahidi: Wilaya tano za kipolisi.
Wakili: Wilaya ya Kinondoni ilikuwa inaongozwa na nani?
Shahidi: Edward Maro.
Wakili: Hao viongozi wa wilaya kipolisi wanawajibika kwa nani?
Shahidi: Kwangu.
Wakili: Kuna sheria yoyote inamzuia RPC kwenda vituo vya polisi?
Shahidi: Hakuna, kwani vituo hivyo ni nyumba za serikali.
Wakili: Turudi kwenye tukio lililopo mahakamani, kuna shahidi ulitolewa kwamba siku hiyo ulikwenda kituo cha Urafiki, ulikwenda kufanya nini?
Shahidi: Siku hiyo mke wangu ambaye yupo hapa mahakamani alikuwa anaumwa tumbo na alikwenda hospitali ya TMJ kwa kutumia teksi kutoka Mtoni Kijichi hadi hospitalini na alipofika alinipigia simu nikamchukue. Ilipofika saa 1:30 jioni nilikwenda hospitalini hapo na dereva wangu Station Sajenti Alifa ambaye alibaki ndani ya gari na simu ya upepo (Radio Call).

Ghafla dereva alinifuata na kuniambia OCD wa Magomeni, Mentare ananiita kwenye Radio call. Nilipozungumza naye alinitaka niende Kituo cha Polisi Urafiki, ili nikamsaidie kutatua tatizo. Nilipofika Urafiki nilimkuta Mkumbo, Bageni, Ndani na Ahmed Makele.
Wakili: Walikuambia nini?
Shahidi: Mantare aliniambia Bageni na Makele walikuwa wametoka kwenye tukio la wizi la BIDCO ambapo zimepora sh 5,750,000 na walikuwa na sh milioni tano, hivyo kama milioni moja haipo. Akaniambia kuwa kuwa ni maofisa wakubwa, nimsaidie jinsi ya kupata fedha zilizosalia.
Hata hivyo, nilimweleza nina mgonjwa na nilishangaa kuniambia nimsaidie wakati wamesema wameishapata fedha na inakuwaje viongozi wa polisi waibe vielelezo. Ndipo Mtukufu Jaji, nilipokasirika.
Wakili: Eeh nini kilifuata?
Shahidi: Nikamweleza OCD Mantare kama ameshindwa kutatua hilo tatizo, basi ameshindwa kazi na nikamwambia mpaka kufika asubuhi fedha hizo zikiwa hazijapatikana watawajibishwa. Kesho yake Bageni alikuwa na fedha ambazo jana yake walisema hazionekani na walieleza zilikuwa ndani ya gari.
Wakili: Uliviita vyombo vya habari kuvieleza hilo?
Shahidi: Niliviita na wakaja na miongoni mwao ni mwandishi wa Tanzania Daima,Happiness Katabazi na Faustine Kapama wa Daily News, na nikawaeleza kazi nzuri iliyofanywa na polisi ya kukamata majambazi ya BIDCO.
Wakili: Taarifa za mapambano ya askari wako na majambazi ulizipata wapi?
Shahidi: Ni OCD ndiye aliyeniambia majambazi hao wameuwawa, kwani walipambana na polisi na miili ilikuwa imepekekwa Muhimbili.
Na baada ya kelele nyingi kupigwa na wananchi IGP aliunda Tume iliyoongozwa na Mgawe.
Wakili: Lini tume hiyo ilienda eneo la tukio?
Shahidi: Januari 19 mwaka 2006. Mimi na tume hiyo tulikwenda Sinza kukagua. Katika ripoti yake, Mgawe alisema haijakamilika, lakini nimetumia ukachero wangu nimeipata ripoti ya tume hiyo mwisho imeandikwa ‘Hitimisho’. Naomba maneno yaliyopo kwenye ripoti hiyo yatafsiriwe kama yalivyo.

Wakili: Kwenye tume ya Mgawe uliambiwa ufanye nini baada ya ripoti?
Shahidi: Haikuniambia nifanye nini. (Zombe alianza kububujikwa na machozi). Tume haikunigusa, mimi nimeguswa na Tume ya Mkumbi. Na ninashangazwa Rais Kikwete kuingizwa katika kesi hii, kwani alisema ni askari 15 ndiyo wachukuliwe hatua na katika hao jina langu halikuwepo.
Wakili: Mama Mkumbi alisema wewe ulikataa kutoa maelezo ni kweli?
Shahidi: Si kweli, ila ilikuwa ni njia ya kutapatapa kwani nilikuwa nimewashika pabaya.
Wakili: Ni hatua zipi zinachukuliwa kwa mtu ambaye hataki kuchukuliwa maelezo yake na polisi?
Shahidi: Mtuhumiwa anayekataa kutoa maelezo mbele ya askari Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinamruhusu askari kuandika jina la mtuhumiwa na anwani yake, kisha naandika Question Statement, halafu naandika tarehe na saini yangu na ya mtuhumiwa.
Wakili: Yote hayo Mkumbi aliyafanya kwako?
Shahidi: Alipoulizwa na wakili wangu Moses Maira mahakamani hapa alisema mimi nimekataa na alipoulizwa alifuata taratibu alisema hakuzifuata. Mimi ni mpelelezi mkubwa nimesomea ukachero zaidi ya nchi tatu pia sheria naifahamu, DPP akiona kuna dosari katika ushahidi aliopelekewa anarudisha faili polisi lifanyiwe marekebisho. DPP hakufanya hivyo, alifungua kesi kwa kutumia statement za polisi kwamba mimi nina kesi ya kujibu.
Hii inaonyesha ni Polisi na DPP walivyokiuka taratibu dhidi yangu.

Wakili: Kuna ushahidi umesema wewe ulionekana Muhimbili ulienda kufanya nini?
Shahidi: Nilienda huko kwani mke wangu alifanyiwa upasuaji.
Wakili: Uliwahi kukutana na baadhi ya mashahidi watatu ambao walikutaja kwamba ulivaa ninja na mwingine alisema alikukuta ofisi, mwingine alisema ulivaa sare za kazi?
Shahidi: Hivi inawezekana vipi mtu mmoja akavaa nguo mbili tofauti kwa wakati mmoja. Sio kweli mashahidi hao wameidanganya mahakama.
Wakili: Katika maelezo ya mshitakiwa wa 11(Rashid Lema) alisema wewe ndiyo ulitoa amri watu hao wanne wachinjwe. Unasemaje?
Shahidi: Hakuna kitu chochote kinachonigusa mimi. Machi 6 mwaka 2006, Lema alitoa maelezo kwa Mlinzi wa Amani na akadai alimsikia Bageni akisema mimi nimesema watu hao wakachinjwe.

Wakili: Unaweza kusema Lema alikuwa ana nia gani?
Shahidi: Huyu Lema alipangwa animalize, kwani mtu mmoja anaandike statement mbili zenye maelezo tofauti.(Zombe akatoa machozi tena).
Wakili:Katika maelezo ya mshitakiwa wa 12, Bakari alikuwa akimsikia Bageni akisema ‘ndiyo afande,ndiyo afande’ kwasababu walikuwa wote kwenye gari aina ya Pajero ,huyo ndiyo afande ni nani?.
Shahidi: Alinitaja mimi.
Wakili: Kwanini Lema alikutaja wewe?
Shahidi: Sijui, lakini chanzo cha mimi kuunganishwa kwenye kesi hii nasema wazi ni magazeti yalipoanza kuandikwa ‘Zombe kakamatwa. Huu ni mtandao tu. Haiingii akilini mshitakiwa mmoja Lema anitaje kati ya washtakiwa 15. Kuna kitu hapa (Zombe alimwaga machozi).

Wakili: Baada ya tukio lile la mauaji kuna taarifa kwamba ulifanya sherehe na kusema utawapandisha vyeo askari. Ni kweli?
Shahidi: Jamani si kweli. Ukisoma PGO kifungu cha 37 utaona jinsi gani vyeo vinavyopandishwa. Kuna sifa na zawadi katika PGO. Mimi nikiwa Kaimu RPC sijawahi na siwezi kutoa vyeo, anayepaswa kutoa vyeo ni IGP peke yake tena kwa utaratibu maalum. Sina mamlaka ya kupandisha askari vyeo hayo ni majungu.
Wakili: Uliwahi kuulizwa na mpelelezi yoyote kuhusu matumizi yako ya simu ya mkononi?
Shahidi: Sijawahi.
Wakili:Ungependa kuiomba nini mahakama ikufanyie?
Shahidi: Naomba mahakama hii tukufu itoe haki kwa mujibu wa sheria na iangalie ushahidi ulitolewa. Kama nimetenda kosa nihukumiwe kwa kosa nililofanya.

Zombe alimaliza kutoa utetezi wake saa 8: 06 na wakili wake kuomba kesi iahirishwe hadi leo kutokana na hewa nzito iliyokuwapo mahakamani hapo, hoja ambayo iliungwa mkono na mawakili wote.

Leo Zombe ataanza kuhojiwa na mawakili wengine na baadaye wakili wa serikali.

Hata hivyo Zombe wakati anapanda gari kurudi gerezani hakufanya vituko kama ilivyo kawaida yake, bali alipunga mkono na kutabasamu.

Hata hivyo, umati wa watu waliofurika mahakamani hapo kusikiliza ulilalamikia hewa nzito iliyokuwapo mahakamani hapo na kuutupia lawama uongozi wa mahakama kwa kushindwa kudhibiti idadi ya watu na kuonya endapo hali hiyo isipodhibitiwa itaweza kuleta maafa

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Februali 11 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.