Header Ads

JAJI RAMADHANI:BUNGE LISIFANYE KAZI ZA MAHAKAMA

*Atolea mfano wa kesi ya Malima, Mengi
*Rais Kikwete aahidi kuwaongezea bajeti

Na Happiness Katabazi

JAJI MKUU, Agustino Ramadhani, amesema dhana ya mgawanyo wa mahakama lazima izingatiwe, kwani kuna wakati Bunge liliwahi kutaka liwe na madaraka ya kimahakama.

Jaji Ramadhani alitoa kauli hiyo katika sherehe ya Siku ya Sheria Tanzania iliyofanyika jana na kuadhimishwa katika viwanja vya Mahakama Kuu, Dar es Salaam, kuashiria mwanzo rasmi wa kazi za mahakama kwa mwaka huu.

Akitolea mfano wa kesi ya mfanyabiasara maarufu Tanzania, Reginald Mengi na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, Jaji Ramadhani alisema Bunge lilichukua kazi ya mahakama na kusikiliza tatizo kati ya wawili hao wakati mmoja hakuwa mbunge.

“Kwa upande mwingine, Bunge liliwahi kutaka liwe na madaraka ya kimahakama dhidi ya watu wanaozozana na waheshimiwa wabunge. Kwa bahati nzuri wazo hilo halikufanikiwa, lakini bado Bunge lilichukua kazi ya mahakama na kusikiliza tatizo hilo kati ya Malima na Mengi ambaye si mbunge,” alisema.

Alisema mahakama imekuwa na matatizo na ngazi nyingine za serikali, kwani baadhi ya hukumu zimedharauliwa na kutotekelezwa na kutolea mfano katika kesi ya Devram P. Valambhia vs Transport Equipment.

Alisema uamuzi wa kesi hiyo ulitolewa muda mrefu lakini kwa miaka mingi utekelezwaji wake ukawa unazungushwa hadi aliyeshinda kesi alipofariki dunia.

Jaji huyo alisema hivi sasa limezuka tishio jingine dhidi ya uhuru wa mahakama kutoka mhimili wa nne wa dola kama vyombo vya habari vinavyojiita.

Alisema baadhi ya vyombo hivyo huandika maoni kana kwamba ndiyo ukweli wenyewe na kwa hali hiyo hupotosha wananchi na athari iletwayo haitibiki hata kwa shubiri.

“Adui mwingine wa uhuru wa mahakama ni kutokuwa huru kifedha, lakini baadhi yetu majaji, mahakimu na viongozi wengine wa serikali tumetafsiri uhuru wa mahakama kuwa ni utengano wa watendaji wa mahakama na viongozi wa serikali.

“Nakubali baadhi yetu mahakamani ni wakorofi na wengine tunanata, lakini ni ukweli pia kuwa tunabaguliwa na hiyo huchukuliwa kuwa ni sehemu ya uhuru wa mahakama,” alisema Jaji Mkuu aliyekuwa akishangiliwa muda wote alipokuwa akisoma hotuba yake.

Katika hatua nyingine, Jaji Ramadhani alisema kuwa mahakama kamwe haiwezi kumtia mtu hatiani kwa shinikizo.

Jaji Ramadhani alisema ibara ya 107A katika katiba ya nchi inatamka wazi kuwa mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano ni mahakama na ibara ya 107B inasema mahakama zote zitakuwa huru katika utendaji wake na kuongeza kuwa ibara hiyo ndiyo chimbuko la uhuru wa mahakama nchini.

Kwa sababu hiyo, mahakama inatakiwa iwe huru na wale wenye kesi mbele yake au kila mwenye kesi asimjulie hali hakimu au jaji anayesikiliza shauri lake.

Mahakama isishinikizwe kumtia hatiani mtu asiye na hatia. Uhuru ni muhimu sana katika nyakati kama hizi za tuhuma zilizokithiri za ufisadi. Baadhi ya wananchi wamekwishawatia hatiani baadhi ya watuhumiwa hata kabla ya kufikishwa mahakamani,” alisema Jaji Ramadhani na kusababisha viongozi na wananchi mbalimbali kucheko.

Kwa mujibu wa Jaji Ramadhani, bado mahakama nchini inakabiliwa na tatizo la udogo wa bajeti. Mwaka wa fedha wa 2007/8 walipewa sh bilioni 25.06; mwaka 2008/9 walipewa sh bilioni 21.08 na mwaka 2009/10 walipewa bilioni 20.03 alichosema kinazidi kupungua wakati gharama zinapanda.

Kwa kiwango hicho cha mwaka 2009/10 Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu zitaweza kila moja kuwa na vikao vinane tu vya kusikiliza mashauri kwa mwaka huo wa fedha na kuongeza kuwa endapo kiwango hicho hakitaongezwa, juhudi zote wanazofanya za kuharakisha usikilizaji wa kesi zitavia.

“Mheshimiwa Rais Kikwete wewe ndiyo tegemeo letu mahakamani. Spika naye ana matatizo yake lakini hali yake si mbaya kama yetu. Mawaziri wote ni wabunge. Hivyo, maslahi ya wabunge yakiwa bora basi maslahi ya mawaziri yanakuwa bora pia. Lakini mahakama tuko kama watoto yatima, hatuna ubia wa maslahi na mhimili wowote,” alisema kwa masikitiko.

Kwa upande wake, Rais Kikwete ambaye kwa mujibu taratibu hakupaswa kuzungumza katika sherehe hiyo, alilazimika kuomba azungumzie baadhi ya mambo yaliyosemwa na Jaji Mkuu.
Rais Kikwete alikiri adharani kwamba hotuba ya Jaji Ramadhani imemgusa na kuahidi kuongeza bajeti ya Idara ya Mahakama katika mwaka ujao wa fedha.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, kaulimbiu ilikuwa: ‘Nafasi ya mahakama katika kutekeleza shughuli za mamlaka ya nchi kulingana na dhana ya mgawanyo wa madaraka’.

Sherehe hiyo iliudhuriwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, mabalozi, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Davis Mwamunyange, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, Mkurugenzi wa Mashitaka, Eliezer Feleshi, Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki, makamanda wa vyombo vya ulinzi na usalama, majaji wastaafu, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu wa kada mbalimbali.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Februari 7 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.