Header Ads

ZOMBE ASHITUSHA

*Alia na DPP kumchezea mchezo mchafu
*Aeleza simu zilivyotumika kummaliza gerezani
* Kundi la wanafunzi laibuka mahakamani kumfariji

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe (55), ameibua mapya kwa kudai kuwa barua za washtakiwa wanne katika kesi hiyo walizomwandikia aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, Geofrey Shaidi ni mchezo mchafu uliokuwa ukifanywa na DPP.

Zombe, alieleza hayo jana alipokuwa akihojiwa na mawakili wa serikali na mawakili wa utetezi na kudai aliambiwa na raia wema kwamba barua hizo ndizo zilikuwa chanzo kikuu cha yeye kukamatwa na kuwekwa gerezani.
Alidai washtakiwa waliomwandikia kwa siri DPP barua ambazo pia hazikupitia kwa Mkuu wa Gereza la Ukonga ni mshtakiwa 3, 4, 7, 9 na 10.
Alidai barua hizo ni haramu kwa sababu washtakiwa walioandika barua hizo kwa DPP walikuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Magereza, hivyo zilipaswa zipitie kwa Mkuu wa Gereza, kisha ziende kwa DPP.
“Mtukufu jaji, DPP hana mamlaka ya kuwasiliana na mtuhumiwa aliyepo gerezani bila kupata kibali cha Mkuu wa Gereza, hivyo barua zote hizo za washtakiwa kwenda kwa DPP ni haramu. Barua hizi zilitolewa kwenye nguo za mshtakiwa mmoja Juni 3 mwaka 2006 na Juni 5 mwaka huo zikapelekwa kwa DPP na Juni 9 mwaka huo nikakamatwa.
“Hivyo DPP ambaye sasa ni Jaji Shaidi kwa makusudi alikiuka taratibu za gereza na kama hatadhibitiwa, ipo siku anaweza kutorosha watuhumiwa waliopo magerezani…sijui huyu jaji anatenda haki gani,” alidai Zombe.
Zombe alidai kuonyesha ni jinsi gani kesi hiyo imepangwa na kikundi cha watu fulani, mwaka juzi zilikamatwa simu tano gerezani zilizokuwa zikitumiwa na baadhi ya washtakiwa wenzake kuwasiliana na baadhi ya watu waliokuwa nje kumkandamiza yeye.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili wa Serikali, Alexander Msikila na Zombe.
Wakili: Una elimu gani?
Zombe: Diploma ya Uhasibu na Uongozi.
Wakili: Lini ulijiunga na Jeshi la Polisi?
Zombe: Mwaka 1977.
Wakili: Una muda mrefu kazini?
Zombe: Sana.
Wakili: Ulishawahi kufanya kazi ya uhasibu jeshini?
Zombe: Sijawahi kufanyakazi nyingine yoyote katika Jeshi la Polisi zaidi ya kazi ya kachero.
Wakili: Nitakuwa sijakosea nikisema wewe ni kachero mzoefu?
Zombe: Sana. Mimi ni kachero niliyebobea.
Wakili: Tazama hii barua ya DPP kwenda kwa DCI Adadi Rajabu wakati huo (anamuonyesha). Unaifahamu?
Zombe: Subiri nimwambie wakili wangu anipatie barua ya Juni 6 mwaka 2006, iliyoandikwa na DPP kwenda kwa DCI ambayo nilikabidhiwa na IGP ndiyo nitakupa jibu. Haya nimeishaiangalia, ni hivi hizi barua hazifanani, kwani barua unayonionyesha ina ukurasa mmoja na barua kama hiyo iliyopo kwenye kumbukumbu zangu ina kurasa mbili, hivyo unayonionyesha si yenyewe.
Wakili: Katika barua hiyo kuna sehemu inaonyesha nakala upewe wewe au imetumwa katika anwani yako?
Zombe: Hakuna sehemu inayoonyesha vitu vyote viwili ulivyovitaja.
Wakili: Na hizi barua za washtakiwa wenzako wanne walizomwandikia DPP wamezi address kwako?
Zombe: Hapana, hizi barua ni mchezo mchafu uliofanywa na aliyekuwa DPP Geofrey Shaidi na barua hizo nililetewa na raia wema ambao walioniambia hizo barua ndiyo chanzo kikuu cha mimi kuwekwa rumande.
Wakili: Wewe ulikuwa mjumbe wa Tume ya Mgawe?
Zombe: Hapana. Sikushiriki kupeleleza chochote.
Wakili: Utakubaliana na mimi sasa barua ya DPP kwenda kwa DCI na barua za washtakiwa wenzako walizomwandikia DPP ulizipata kwa njia isiyohalali?
Zombe: Hizo barua zilihusu masilahi yangu. Kwa kifupi nilizipata kihalali. DPP anatakiwa afanye kazi kwa masilahi ya taifa na si kuumiza wananchi na ndiyo maana (jana) juzi nililia sana hapa mahakamani. Na kwa taarifa yako moja kati ya barua hizo unazosema nilipewa na IGP, Said Mwema.
Wakili: Soma hizi barua za washtakiwa wenzako zimeandikiwa tarehe ngapi?
Zombe: Baadhi zina tarehe, nyingine hazina.
Wakili: Soma hizi barua orginal za washtakiwa ambazo wewe una photocopy. Zimegongwa muhuri wa nani?
Zombe: Zimegongwa muhuri wa DPP na zinaonyesha zimepokelewa Juni 12 na 13 mwaka 2006. Hata zigongwe muhuri wa DPP, uharamu wa barua hizi upo pale pale, kwani hazikupitia kwa Mkuu wa Gereza, kwani ndiye mwenye himaya ya Gereza la Ukonga.
Wakili: Wewe photocopy za barua za washtakiwa ulizonazo zinaonyesha zilipokelewa kwa DPP Juni 5, lakini orginal ambazo sisi tunazo zinaonyesha zilipokelewa kati ya Juni 12 na 15 mwaka 2006, unaizungumziaje hali hiyo?
Zombe: Si kweli. Na DPP amekiuka taratibu za magereza na ipo siku huyu DPP anaweza kutorosha watuhumiwa gerezani.
Wakili: Sasa nakwambia hizo barua wewe uliiba na ukazighushi, unasemaje?
Zombe: Sijaiba na wala sijaghushi na kwa taarifa yako ninaweza kuleta mahabusu waje mbele ya mahakama hii tukufu kuthibitisha, kwani Juni 3 mwaka huo, waliwaona washtakiwa hao wakiandika barua hizo na zikatoka gerezani kupitia kwenye moja ya nguo za mshtakiwa.
Wakili: Katika ushahidi wako ulioutoa jana (juzi) ulisema hizi barua za washtakiwa ni haramu?
Zombe: Kitu haramu ni kitu haramu huwezi kukifanya kisiwe haramu. Barua hizo ziliandikwa Juni 3 na zikaenda kwa DPP Juni 5 na Juni 9 mwaka huo, nikiwa ofisini pale Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, nilikamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Wakili: Zaidi ya hayo maneno unayoyazungumza kuhusu tarehe hizo, una ushahidi gani mwingine?
Zombe: Sahihi kabisa mtukufu jaji, ushahidi ninao, kwani barua hizo zina maneno yanayofanana na kufundishwa na DPP ambaye sasa ni jaji wa Mahakama Kuu na sijui jaji huyu kama anatenda haki.
Wakili: Una ushahidi na hayo uliyoyasema?
Zombe: Ndiyo, kwani Juni 15 mwaka huo, tukiwa gerezani Ukonga zilikamatwa simu tano zilizokuwa zikitumiwa na baadhi ya washtakiwa. Washtakiwa ambao hawakuandika barua kwa DPP waliniambia kuwa hiyo ilikuwa ni njama na askari magereza ikabidi washtakiwa wote tupekuliwe.
Na siku niliyokamatwa na kupelekwa gerezani baadhi ya washtakiwa tulioshitakiwa nao walishangilia.
Wakili: Katika ushahidi wako tukio la BIDCO ulilijua baada ya kufika Kituo cha Urafiki au kwa PC John wa 999?
Zombe: Mtambo wa mawasiliano upo na Ikulu na maofisa wa polisi kama mimi (kamanda) tunasikia kupitia redio call, kwahiyo nilisikia tukio hilo kupitia 999.
Wakili: Baada ya John kutangaza taarifa za BIDCO, uliwahi kupata taarifa kwamba askari walipambana na majambazi Januari 16 mwaka huo?
Zombe: Ndiyo nilizipata kwa OCD Maro wa Oysterbay na Mantage wa Magomeni.
Wakili: Soma statement yako?
Zombe: Nikiwa ofisini kwangu nilisikia mshitakiwa wa tatu, Ahmed Makele akisema askari walipambana na majambazi na sh milioni tano zilipatikana.
Wakili: Sasa tukueleweje mara ya kwanza ulisema ulipata taarifa kwa OCD Maro au kwenye redio call?
Zombe: Shahidi wa 13, PC John alikuja kwenda mahakama hii tukufu na kuieleza kwamba siku hiyo alikuwa kwenye chumba cha mawasiliano na hakusikia kabisa kwamba mimi nilitoa amri.
Wakili: Sisi serikali tuna ushahidi kuwa wewe ulimwambia Makele, kwamba marehemu wapelekwe kwa mshitakiwa wa pili (Christopher Bageni) alipo?
Zombe: Si kweli, ila kama nyie mawakili wa serikali mnataka kuanzisha kesi nyingine dhidi yangu mi nipo tayari. Hayo ni maneno ya washtakiwa waliyofundishwa na DPP Shaidi na si vinginevyo.
Wakili: Twende kwenye pistol ya marehemu waliyokamatwa nayo. Wewe kama kachero uliyebobea uliifanyia uchunguzi?
Zombe: Elewa mimi si mtaalamu wa silaha na kama nilivyoeleza jana (juzi) wakati huo nilikuwa kwenye ziara ya Rais Jakaya Kikwete. Na ikumbukwe wakati huo IGP alikuwa ameishaunda tume ya kuchunguza malalamiko ya wananchi kuhusu mauaji ya watu hao wanne, hivyo mimi ni mtu mdogo kwa IGP, hivyo ningechunguza nini wakati jambo hilo limeundiwa tume ya kuchunguza?
Wakili: Ulisema lini uliitisha mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia mwendelezo wa tukio hili?
Shahidi: Januari 15 mwaka huo (2006).

Wakili: Utakubaliana na mimi terehe hiyo tume ya Mgawe ilikuwa bado haijaanza kufanya kazi?
Zombe: Ni kweli, katika kikao changu na waandishi wa habari nilikuwa natumia taarifa ya OCD.
Wakili: Pistol hiyo hiyo ambayo hukuifanyia uchunguzi ndiyo ulionyesha waandishi wa habari kwamba ni ya majambazi. Ni kwa nini ulishindwa kuipeleka kitengo husika ikatambuliwe kama ni ya jambazi au inamilikiwa kihalali?
Zombe: Nimekwambia muda ulikuwa mchache. We bwana vipi.
Wakili: Unakumbuka Januari 15 mwaka 2006, ulitoa press release (Taarifa kwa vyombo vya habari) ukisema Januari 14 mwaka huo kulikuwa na matukio mangapi ya uhalifu yalitokea?
Zombe: Sikumbuki, kwani nimekaa jela muda mrefu.
Wakili: Hii hapa Press Release, unaitambua?
Zombe: Jaji, hii si press release niliyoitoa, kwani wakati ule polisi ilikuwa ikitumia Typewriter na hii imeandikwa kwa kompyuta.
Wakili: Unakumbuka mapambano ya majambazi na polisi yalifanyika wapi?
Zombe: Kwa mujibu wa taarifa za askari wangu waliniambia mapambano yalifanyika Sinza ‘C’ ukuta wa Posta na nilifika eneo hilo kukagua.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili wa Serikali, Jasson Kaishoni na Zombe:
Wakili: Kuna siku umeshawahi kutilia mashaka maamuzi ya DPP Shaidi?
Zombe: Sana tena sana. Nina ushahidi wa mashaka yangu upo kwenye kesi ya waliokuwa wafanyakazi wa BIMA ambayo ina miaka 10 katika Mahakama ya Kisutu, katika kesi hii, Shaidi alimchoma mkwe wake, kesi bado ipo mahakamani haina kichwa wala miguu.
Wakili: Si kweli kama siku zote za juma ulikuwa kwenye msafara wa rais?
Zombe: Ndiyo, si kweli hasa Jumamosi na Jumapili, lakini kila wakati askari anakuwa kazini.
Wakili: Januari 14-15 mwaka 2006 ambazo ndiyo tarehe za tukio la mauaji kutokea, ulikuwa wapi?
Zombe: Nilikuwa kwenye shughuli zangu. Sikuwa kwenye msafara wa rais. Nilikuwa kazini.
Wakili: Januari 12, msafara wa Rais Kikwete ulikwenda wapi?
Zombe: Sikumbuki, nimekaa sana jela.
Wakili: Jana ulisema wakati tukio hilo linatokea ulikuwa Hospitali ya TMJ mkeo alikuwa anaumwa na leo (jana) unasema ulikuwa ofisini na ukamtuma SSP Charles Mkumbo?
Zombe: Rudia swali tafadhari.
Wakili: Katika utaratibu wa kipolisi OCD na RPC nani mkubwa?
Zombe: RPC.
Wakili: OCD anaweza kumwita RPC ofisini kwake?
Zombe: Ikibidi anaweza kumwita.
Wakili: Katika ushahidi wako ulioutoa jana (juzi) ulisema ulipofika Urafiki ulikuta askari wangapi?
Zombe: OCD wa Magomeni, SSP Isuto Mantage, Makele, Ndaki, Mkumbo.
Wakili: Kwa njia unazojua wewe ulitumia simu yako ya mkononi kutoa amri watu hao wauawe?
Zombe: Si kweli, hayo maneno yamepangwa na DDP Shaidi, Sidyen Mkumbi alivyokuja kutoa ushahidi hapa mahakamani alisema hajui namba yangu ya simu ya mkononi. Kwa hiyo unataka kuiambia mahakama mimi nilitumia njia ya uchawi kuwasiliana. Hayo mabarua na simu za washtakiwa kwenda kwa DPP ndiyo yanayowafanya nyie mawakili wa serikali leo hii mjifanye mning’ang’anie. Poleni sana.

Wakili: Kwenye Tume ya Jaji Mussa Kipenka ulivyohojiwa mbona hukueleza ulikuwa kwenye ziara ya rais?
Zombe: Sikumbuki. Mimi ni binadamu naweza kusahau. Mimi ni kamanda ambaye ndiye nilikuwa naongoza msafara wa rais, msafara wa rais hauwezi kuongozwa na askari wa chini ya cheo changu wakati mimi mwenye cheo cha juu nilikuwepo.
Wakili: Unaufahamu msitu wa Pande?
Zombe: Nimeufahamu kwa mara ya kwanza msitu huu mwaka jana wakati mahakama hii tukufu ilipotembelea msitu ule.
Wakili: Ukiwa ni RCP na Kaimu RPC huoni huo ni uzembe?
Zombe: Si kweli, kwani hata rais wa nchi hawezi kujua vijiji vyote vilivyo kwenye ardhi ya taifa analoliongoza.
Wakili: Hapa kuna kitu unakificha na leo (jana) lazima utakisema tu?
Zombe: Narudia tena hiyo mibarua yenu ya washtakiwa wenzangu wa nne waliyomwandikia DPP, ndiyo inayowachanganya nyie mawakili wa serikali.
Wakili: Una ugomvi na mshitakiwa wa 11, Rashid Lema?
Zombe: Sina ugomvi naye, ila ninachojua mimi wakati nikiwa RCO, nililetewa taarifa kwamba Lema alivunja na kuiba kwenye kantini ya polisi Oysterbay, nikaamuru ahojiwe na kisha ashitakiwe kijeshi.
Wakili: Shahidi wa 36, ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Sidney Mkumbi una ugomvi naye?
Zombe: Nasema hivi, Mkumbi ni Bad Woman kwani naye ameshiriki kuniangamiza katika kesi hii.
Wakili: DPP na RCO nani ni mkubwa kicheo?
Zombe: DPP
Wakili: Sasa unadhani DPP anaweza kuchukua cheo chako cha RCO?
Zombe: DPP anaweza kuchukua rushwa kwenye magazeti, ili aniharibie kesi sita za madai ya kukashfiwa nilizozifungua mahakamani hapa.
Wakili: Machi 6 mwaka 2006 ulikuwa umeishazifungua kesi hizo?
Zombe: Hapana, ila nakumbuka wakili wangu, Jerome Msemwa, alikuwa katika hatua za mwisho za kuandaa kesi hizo.
Wakili: Kwa hiyo ulikuwa unatishia nyau?
Zombe: Mtu mzima hawezi kutishiwa nyau. (Watu wakaangua kicheko). Na kwa kifupi nieleze kesi hii ni ya kupangwa na kikundi cha watu, ili waniangamize mimi.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili Majura Magafu na Zombe:
Wakili: Kuna ofisa yeyote wa ngazi ya juu katika Jeshi la Polisi aliwahi kukuita akakwambia tukio halijawahi kutokea Sinza, bali lilitokea Pande?
Zombe: Sijawahi kuitwa na kuulizwa hilo.
Wakili: Wewe ni kachero mzoefu, zoezi la upelelezi wa kesi za jinai linaishia wapi?
Zombe: Pale upelelezi unapokamilika.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya mzee wa baraza na Zombe:
Mzee wa Baraza: Katika tukio hili zima nani alaumiwe?
Zombe: Naiachia mahakama iamue. Zombe akawa amefunga kutoa ushahidi wake huku akiwa ameloa jasho kutokana na hewa kuwa nzito mahakamani hapo.
Baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo wakili mwandamizi wa serikali, Mgaya Mtaki, alimuomba Jaji Salum Msati kuahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo mshitakiwa wa pili, Christopher Bageni ataanza kujitetea.
Wakati washtakiwa hao wakipanda basi la Magereza, ghafla lilitokea kundi la wanafunzi zaidi ya 70 wa shule mbalimbali za msingi, waliolizonga lango la Mahakama Kuu na walipomuona Zombe walimpungia mikono huku wengine wakisikika wakisema: “Zombe tunakuombea Mungu atakusaidia.”
“Zombe, Zombe yule pale kwenye basi, Zombe omba Mungu atakusaidia,” walisikika wakisema wanafunzi hao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 12 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.