Header Ads

MAPYA YAIBUKA KESI YA EPA

Na Happiness Katabazi

WAKILI wa upande wa utetezi katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8, katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Majura Magafu, amepinga kupokewa kwa maelezo ya onyo ya mteja wake, Rajabu Maranda, kwa madai kuwa yalichukuliwa na wajumbe wa timu ya rais ya kuchunguza wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ambayo kisheria haina mamlaka ya kuendesha kesi mahakamani.

Magafu alitoa pingamizi hilo muda mfupi baada ya shahidi wa sita, Mrakibu wa Polisi (SSP) Salum Kisai (45), kutoa maelezo ya onyo aliyochukua kwa Maranda, Oktoba 3 mwaka jana, kwenye ofisi ya timu hiyo, Mikocheni, Dar es Salaam.

Magafu alidai kuwa kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, inalitaka Jeshi la Polisi kuendesha kesi hiyo badala ya timu ya rais.

Alidai licha ya shahidi huyo kuwa ni ofisa wa polisi, alikuwa mjumbe wa timu hiyo iliyoongozwa na Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika, alikiuka sheria kuchukua maelezo ya mshitakiwa huyo ambayo jana aliyaleta mahakamani hapo na kutaka kuyatoa kama kielelezo.

“Kisheria timu ya rais haina mamlaka ya kuendesha kesi mahakamani, sasa timu ile ya rais ambayo huyu shahidi alikuwa mmoja wa wajumbe wa fani mbalimbali, wakiwemo watu wa Idara ya Usalama wa Taifa, alichukua maelezo ya Maranda wakati kufanya vile ni kinyume cha sheria na kwa sababu hiyo, napinga maelezo ya Maranda ambayo yanataka yatolewe kama kielelezo mahakamani hapa,” alidai Magafu.

Akijibu hoja za wakili huyo, wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, aliomba mahakama ipokee maelezo hayo kwa madai kuwa timu ile ilikuwa na polisi na Takukuru, ambao ni wachunguzi na wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo Naibu Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Cypiriana William, ambaye anasaidiana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Phocus Bampikya na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Saul Kinemela, alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kuahirisha shauri hilo hadi leo ambapo atatoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo.

Awali kabla ya kuwasilisha pingamizi hilo, Bampikya alitupilia mbali pingamizi la wakili Magafu aliloliwasilisha wiki Jumanne iliyopita la kutaka jopo hilo lisipokee maelezo ya onyo la mteja wake, Farijara Hussein, ambaye ni mshitakiwa katika kesi hiyo kwa madai kuwa si la msingi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 27 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.