Header Ads

LIYUMBA KUIBUKIA MAHAKAMANI LEO

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba, ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kusababisha hasara ya sh bilioni 221, leo anatarajiwa kuibukia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Tanzania Daima imeelezwa.

Kwa mujibu wa watu wa karibu na Liyumba, wamesema ataibukia mahakamani leo.
Vyanzo hivyo vilikanusha madai kwamba Liyumba alikuwa ametoroka na kubainisha kwamba aliamua kuzima simu yake ya kiganjani ili aweze kupumzika, baada ya kusota rumande kwa siku 22.

“Tunashangaa sana huu uvumi kwamba Liyumba katoroka, kimsingi ajatoroka, yupo hapa hapa jijini, kajichimbia na alizima simu zake ili aweze kupumzika na kuhakikisha anakamilisha masharti ya dhamana, kwani tayari kuna taarifa kuwa mahakama itabatilisha taratibu zilizotumika kumpatia dhamana, hivyo atatakiwa aanze upya kuomba dhamana.

“Nakuhakikishia kesho (leo), Liyumba ataibukia Mahakama ya Kisutu, kwani ndiyo tarehe ya kesi yake inayokuja kwa ajili ya kutajwa na haya ninayokueleza, vyombo vya ulinzi na usalama vinajua kwamba yupo na ana fanya nini.

“Navishangaa sana vyombo vya habari vinavyoandika Liyumba ametoroka, nyie andikeni wee lakini ukweli ni kwamba Liyumba ajatoroka, yupo hai na hivyo vyombo vya dola vilivyopewa amri na mahakama ya kumkamata Liyumba, vinafahamu kwamba yupo wapi, anafanya nini na anaishi wapi,” kilisema chanzo chetu.

Mbali na Liyumba, mshitakiwa mwingine ni Meneja Mradi wa BoT, Deogratius Kweka, ambaye hadi sasa anaendelea kusota rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Alhamisi ya wiki iliyopita, uvumi ulizagaa jijini Dar es Salaam kwamba mshitakiwa huyo ametoroka.

Kutokana na uvumi huo, mahakama ililazimika kutoa hati ya dharura ya kukamatwa kwa mshitakiwa huyo na wadhamini wake wawili.

Hata hivyo vyanzo vyetu vya habari vilidai kuwa mshitakiwa huyo aliitwa kwa hati ya dharura mahakamani, huenda kutokana na mazingira ya utata wa dhamana yake, kwani alidhaminiwa kwa hati ya mali ya sh milioni 882, badala ya mali zenye thamani ya sh bilioni 55.

Siku hiyo, saa sita mchana, wadhamini wake wawili ambao ni wafanyakazi wa BoT, Otto Agatoni, Ofisa Usalama wa Ndani ya benki hiyo, na Benjamin Ngulugunu, ambaye ni mhasibu, walikamatwa na kuswekwa katika mahabusu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuanzia majira ya saa sita mchana hadi saa 10:32 jioni, walipopandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo.

Msongo alisema kesi hiyo itatajwa leo kama ilivyopangwa awali na kwamba wadhamini hao nao wanatakiwa kufika pamoja na mshitakiwa.

Liyumba na Kweka, wanakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuidhinisha ujenzi wa minara pacha ya BoT, maarufu kama ‘Twin Towers’ na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Februali 24 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.