JE MAHAKAMA ILIYUMBA KWENYE DHAMANA YA LIYUMBA?
Na Happiness Katabazi
TUME ya Jaji Joseph Warioba iliyochunguza mianya ya rushwa nchini Tanzania, ilisema kwamba moja ya taasisi za dola ambazo zimegubikwa na rushwa ni Mahakama.
Ibara ya 107-B ya Katiba ya nchi, inayolinda uhuru wa Mahakama ina lengo la kuhakikisha kwamba mahakama haziingiliwi wala kutishwa na mtu au taasisi yoyote wakati zinapotekeleza wajibu wake wa kutoa haki na kutafsri sheria.
Tamko la Tume ya Jaji Warioba limekuwa likiangaliwa katika upeo huo, kwamba pamoja na tuhuma za rushwa, isije ikatokea vita dhidi ya rushwa na ufisadi vikatoa mwanya kwa Mahakama kuingiliwa na kutishwa.
Matukio yaliyotokea kwenye kesi ya jinai namba 27 ya mwaka 2009, Jamhuri dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Mradi wa Benki hiyo, Deogratius Kweka, iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi Hadija Msongo, yamenishtua sana.
Mahakama ya Kisutu ndiyo iliyoanza kusikiliza ombi la dhamana la Liyumba kwa kuweka masharti ya dhamana hiyo Januari 27, mwaka huu.
Masharti hayo yalieleza kuwa watuhumiwa wanapaswa kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali, kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani, kila Ijumaa kuripoti ofisi za Takukuru, kutoa fedha taslimu au hati zenye thamani ya sh bilioni 55 kila mmoja.
Lakini Jumanne iliyopita, nilishangaa kusoma katika vyombo vya habari kuwa Liyumba aliwasilisha hati yenye thamani ya sh milioni 882, hati ya kusafiria ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, huku wadhamini wawili wakiwa hawana barua zilizosainiwa na mwajiri wao kama masharti ya dhamana yalivyotolewa na mahakama hiyo ili Liyumba apewe dhamana.
Licha ya Wakili wa Serikali, Justas Mlokozi, kupinga kwa nguvu zote uamuzi huo, Hakimu Msongo, aliweka pamba masikioni na kutupilia mbali madai ya upande wa wakili Mlokozi na kumwachia Liyumba kwa dhamana huku akiagiza upande wa utetezi kujipanga kukamilisha masharti ya dhamana wakati mtuhumiwa akiwa nje.
Ikumbukwe kuwa masharti hayo ya dhamana katika kesi hiyo yalibishaniwa Mahakama Kuu mbele ya Jaji Projestus Rugazia, na jaji huyo Februari 13, mwaka huu, akitoa uamuzi wake alithibitisha masharti hayo yaliyotolewa na Mahakama ya Kisutu, isipokuwa sharti moja linalomtaka mshitakiwa kuripoti Takukuru kila Ijumaa.
Kwa kuwa masharti yote yalithibitishwa na Mahakama Kuu na hapakuwa na rufaa iliyokatwa dhidi ya masharti hayo, ulikuwa ni wajibu sasa wa Mahakama ya Kisutu kuhakikisha kwamba dhamana inatolewa mara tu mtuhumiwa anapotimiza masharti yaliyowekwa.
Hata hivyo, hilo halikutokea na badala yake Mahakama ya Kisutu ilipitia upya masharti hayo na kubadilisha kwa namna ambavyo inaweza kulinganishwa na kula matapishi yake. Hivyo sivyo sheria inavyotaka.
Si tu kwamba Kisutu haikuwa na mamlaka ya kuyabadili masharti yale kwa vile yalikuwa yameshabishaniwa Mahakama Kuu na kufanyiwa maamuzi na mahakama hiyo ya juu, bali pia hapakuwa na ombi la kuomba marejeo (review) ya uamuzi huo wa Mahakama Kuu, hata kama ombi hilo lingekuwepo lisingepelekwa Mahakama ya Kisutu, lingepelekwa Mahakama Kuu.
Kumbe basi, kioja kilichotokea kinaleta utata na wasiwasi mwingi kuhusu uwezo wa Hakimu Mkazi, Hadija Msongo na Mahakama ya Kisutu kwa ujumla katika kufanya maamuzi katika shauri hili, kwa kuwa mahakama hii haionekani kuwa na weledi wa kutosha katika tasnia ya sheria.
Katika hali hii, yawezekana kabisa raia wasio na taaluma ya sheria kuchanganyikiwa wanapoisoma Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayosema watu wote ni sawa mbele ya sheria.
Kama wale watuhumiwa wa kesi za EPA walikabwa koo na Mahakama ya Kisutu na hawakupewa dhamana hadi walipotimiza kila kipengele cha masharti ya dhamana na wakafanya hivyo, iweje sasa Liyumba alegezewe masharti na kisha akaachiwa na kuambiwa masharti mengine akatimize akiwa nyumbani kwake?
Kwani Liyumba na hao washtakiwa wa EPA, Basil Mramba, Daniel Yona, wezi wa mabeseni na hata kuku, wanatofauti gani mbele ya sheria?
Lakini pia ni vyema tujiulize kama Mahakama ya Kisutu ilifanya hivyo kwa nia njema bila shinikizo.
Tukumbuke maneno ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Said Mwema, kwamba ‘mafisadi ni watu wenye nguvu kubwa.’
Watanzania tunauliza kama nguvu hiyo ya kifisadi imeikumba Mahakama ya Kisutu.
Sisi raia wa kawaida hatushabikii sheria mbaya zinazoweka masharti makali ya dhamana kwa watuhumiwa, lakini ili mradi hatujazibadili sheria hizo ili tuwe na masharti nafuu, kwa kila mtuhumiwa, ni vyema kila raia atendewe sawa mbele ya sheria.
Kitendo kilichofanywa na Hakimu Msongo cha kumpatia dhamana Liyumba wakati hajatimiza masharti ambayo Januari 27 mwaka huu, ni yeye aliyeyaweka na yakasisitizwa na Mahakama Kuu, kimetia doa mhimili mahususi wa Mahakama nchini, kuhusu uwezo wa kusimamia haki na usawa mbele ya sheria.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Februali 25 mwaka 2009

1 comment:
KWA NINI KESI NYINGI ZINAZOHUSU WANAWAKE ZIKIPELEKWA KWA MAHAKIMU MAJAJI WNAWAKE ZINASHINDA? JE HAKI INAFUATWA KWELI. TAZAMA KESI NYINGI ZA MAJAJI WA KIKE ZINAZOHUSU WANAWAKE.
Post a Comment