Header Ads

LIYUMBA APONZA WADHAMINI WAKE

*Hati zao zenye utata zapelekwa kwa DCI Kuchunguzwa

Na Happiness Katabazi

HATI za watu 10 waliojitokeza awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kutaka kumdhamini aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, anayekabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, zimeanza kuchunguzwa na Jeshi la Polisi, imefahamika.

Hati za wadhamini hao kumi, zenye thamani ya sh bilioni 55, ndizo zilizotumika kujaribu kumdhamini Liyumba, mara ya kwanza, lakini zilikataliwa baada ya kubainika kuwa zilikuwa na kasoro kubwa za kisheria, huku nyingine zikidaiwa kuwa ni za kughushi.

Miongoni mwa watu wanaomiliki hati hizo zilizobainika kuwa na upungufu kisheria ni pamoja na aliyekuwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Jamila Nzota, ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya rushwa katika Mahakama hiyo ya Kisutu.

Hati nyingine ni ya Cecil Chiwango, Abubakar Ogunda, Avogiti Chiwando, Mikidadi Mtumbati, Selemani Kaboke, Justas Samson, Gideon Chipange, Hashimu Mwinyimvua na John Ngutilo, ambaye amewasilisha hati mbili na kufanya thamani ya hati hizo 10, kufikia sh bilioni 55 ambazo zingetosha kumtoa Liyumba katika mahabusu ya Keko, alikorejeshwa wiki iliyopita baada ya kufutiwa dhamana iliyozua utata ya hati ya sh milioni 882.

Vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, vinaeleza kuwa hati hizo zilitoka mahakamani hapo juzi na kupelekwa siku hiyo hiyo katika ofisi ya Makao Makuu ya Upelelezi ambapo zilipokewa na kuanza kufanyiwa kazi.

Kwa mujibu wa habari hizo, tayari uchunguzi wa kujua uhalali wa hati hizo unaofanywa na Idara ya Utambuzi wa Maandishi kwa umakini mkubwa, umeanza mara moja na utakapokamilika, utarejeshwa katika Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kutolewa taarifa.

“Hati hizo ziliondoka Kisutu juzi, na ofisa mmoja kutoka mahakamani hapo ndiye alizipeleka ofisini kwa DCI, ili zifanyiwe uchunguzi kama zimeghushiwa au la, na ninakuhakikishia DCI ameishawaagiza vijana wake waanze kuzifanyia kazi mara moja na pindi watakapokamilisha uchunguzi huo utakabidhiwa katika Mahakama ya Kisutu,” kilidai chanzo chetu.

Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, alikiri kupokea hati hizo na kwamba ameishaagiza Idara ya Utambuzi wa Maandishi izifanyie uchunguzi wa kitaalamu.

“Ni kweli hati hizo tumezipokea jana (juzi) na tayari nimeishaagiza idara husika zianze kuzifanyia uchunguzi kama ilivyoamriwa na mahakama na kwamba tayari idara yetu husika imeishaanza kazi mara moja ya kuchunguza hati hizo na uchunguzi ukikamilika, tutaupeleka Mahakama ya Kisutu,” alisema Manumba.

Hata hivyo, Manumba alisema ni mapema kuahidi muda ambao uchunguzi huo utakuwa umekamilika, lakini alisisitiza kuwa utakapokamilika majibu yatapelekwa mahakamani, kwani mahakama ndiyo iliyotoa amri ya hati hizo kupelekwa polisi.

Jumanne wiki hii, Februari 24, wakati akitangaza kufuta dhamana ya Liyumba, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Hadija Msongo, alizungumzia hati 10 zilizotumika kumdhamini mshitakiwa huyo awali kuwa zina kasoro za kisheria.

Alisema mahakama imegundua hati ya Avogiti Chiwando, ambayo inaonyesha ilitolewa na Ofisa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakati hakuna mtu kama huyo wizarani hapo na hati ya Abubakar Ogunda, ilionyesha kuwa ana mali kama kuku na ng’ombe haikubaliki, kwani sharti la dhamana lilitaka kuwasilisha hati ya mali zisizohamishika.

“Kwa ujumla hati zote 10 zinazoonyesha nyumba na viwanja katika maeneo mbalimbali zina kasoro, kwani majengo katika hati hizo yanaonekana kufanana.

“Na hati hizo ambazo zinaonyesha ziligongwa muhuri na Mtathimini wa Gharama za Majengo, Thomas Antabe, hazikubaliwi na mahakama, kwani muhuri wa mtu huyo hauonyeshi mahali ilipo ofisi yake, hivyo mahakama inaona mshitakiwa hajatimiza masharti ya dhamana.

“Kwakuwa masharti ya dhamana hayajatimizwa, mahakama hii inatoa amri ya kumfutia dhamana mshitakiwa na hati hizo kumi zipelekwe Jeshi la Polisi, ili ziweze kufanyiwa uchunguzi wa kimaandishi na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 10, mwaka huu,” alisema Msongo.

Hakimu huyo akisisitiza kuhusu uamuzi wake wa kumfutia dhamana Liyumba, alisema amelazimika kumfutia dhamana baada ya kubaini mshitakiwa huyo aliidanganya mahakama.

Mahakama ya Kisutu ndiyo iliyoanza kusikiliza ombi la dhamana la Liyumba kwa kuweka masharti ya dhamana hiyo Januari 27, mwaka huu.

Masharti hayo yalieleza kuwa watuhumiwa wanapaswa kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali, kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani, kila Ijumaa kuripoti ofisi za Takukuru na kutoa fedha taslimu au hati zenye thamani ya sh bilioni 55 kila mmoja.

Lakini Februari 17, mwaka huu, Liyumba aliwasilisha hati yenye thamani ya sh milioni 882, hati ya kusafiria ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, huku wadhamini wawili wakiwa hawana barua zilizosainiwa na mwajiri wao kama masharti ya dhamana yalivyotaka, na alifanikiwa kutoka kwa dhamana.

Mbali na Liyumba, mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Meneja Mradi wa BoT, Deogratius Kweka, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februari 27 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.