Header Ads

ZOMBE MAMBO MAZITO

*Makele aukana ushahidi wa Zombe
*Adai aliwakuta marehemu wakiwa hai

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA wa tatu katika kesi ya mauji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi mmoja, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Polisi Urafiki, Mrakibu wa Polisi (SP), Ahmed Makele (45), ameieleza mahakama kuwa aliwashuhudia marehemu walikamatwa wakiwa hai na kuhifadhiwa katika ukuta wa Posta Sinza, jijini Dar es Salaam.

Wakati mshitakiwa wa pili, Christopher Bageni akihojiwa na wakili wa mshitakiwa wa kwanza, Jerome Msemwa, mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Abdalah Zombe alikuwa na kazi ya ziada ya kuandika maswali kwenye karatasi na kumpa wakili wake ambaye alikuwa akilazimika kwenda kwa Zombe na kuchukua maswali na kisha kumuuliza Bageni ambaye juzi wakati akitoa ushahidi wake, alionyesha kumdidimiza Zombe.

Makele ambaye alianza kutoa ushahidi wake jana saa nane mchana, akiongozwa na wakili wake, Majura Magafu, alidai kuwa Januari 14 mwaka 2006, saa moja jioni, alifika Sinza C’ eneo la ukuta wa Posta kwa ajili ya kusaka watuhumiwa wa ujambazi waliopora fedha za BIDCO.

Alidai wakati anafika eneo hilo, ghafla mshitakiwa wa sita (Morris Nyangerela) ambaye ameachiwa huru wiki iliyopita, alikuwa ameshika bunduki aina ya SMG, alimtaka asimamishe gari alilokuwa amepanda na kumtaka ashuke.

Alidai kuwa aliposhuka, alimkuta askari huyo, akiwa na askari wengine ambaye alimwambia waliwakamata watu wanne wanaowashuku kuwa ni majambazo wa tukio la BIDCO.

“Baada ya kunilieza hivyo mimi niliwaamuru askari hao wa Kituo cha Chuo Kikuu, wawachukue watuhumiwa hao wanne pamoja na sh milioni tano na bastora, waende nazo kwani si vyema kuwahoji watuhumiwa hao kwenye umati wa watu ambao walikuwa wamekusanyika katika eneo hilo,” alidai Makele.

Alidai kuwa baada ya kutoa agizo hilo, Nyangerela alichukua fedha hizo na kutaka kumkabidhi mshitakiwa wa tano (Jane Andrew) ambapo alidai alikataa kwa madai kwamba makabidhiano ya vielelezo havipaswi kukabidhiana barabarani,” alidai Makele.

Ifuatayo ni mahojiano kati ya wakili Majura Magafu na Makele;
Wakili: Ni lini ulikuwa Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Urafiki?
Makele: Juni 2005 hadi napata hii kesi.
Wakili: Ni lini ulikamatwa kuhusu tukio hili lililotuleta hapa mahakamani?
Makele: Machi 3 mwaka 2006.
Wakili: Tukio hili la mauaji lilitokea lini?
Makele: Januari 14 mwaka 2006.
Wakili: Wewe umesema ulikamatwa Machi tatu, tangu Januari 14 mwaka huo, ulikuwa wapi?
Makele: Nilikuwa Misri kwenye mafunzo ya Crime Operation Combate.
Wakili: Mashitaka yaliyopo hapa mahakamani wewe una husika katika mauaji ya wafanyabaishara wa tatu na dereva taksi mmoja, wewe unasemaje?
Makele: Si kweli.
Wakili: Tueleze unafahamu nini kuhusu tukio hilo?
Makele: Nakumbuka saa 12:30 jioni, siku hiyo nilikuwa Katini kituoni Urafiki, nikapata taarifa toka kwa Control Room kwamba kuna tukio la ujambazi, walitangaza kwenye redia Call kwamba Barabara ya Samnujoma kuna tukio la ujambazi limetokea.
Wakili: Baada ya kusikia hiyo taarifa, watu wa Control Room walikuambia nini wewe?
Makele: Waliniambia uenda majambazi hao wakawa wamekimbilia Mwenge au Sinza. Nikafika kituoni ili nichukue askari wa CID na gari ili niende eneo la tukio.
Wakili: Ulipofika kituoni ulifanya nini?
Makele: Mtukufu Jaji nilipata shida sana kwani sikuwakuta askari kanzu (CID).
Wakili: Ukachukua hatua gani?
Makele: Nilikaamua kuchukua askari wawili waliovalia sare za polisi ambao wapo kaunta ya polisi (RCO).
Wakili: Baada ya kufuchukua askari hao ulifanya nini?
Makele: Sote tuliingia kwenye gari, kabla hatujaingia barabara ya Morogoro, nikawaona washitakiwa (Coplo Abeneth na Jane Andrew) ambao ni CID.
Wakili: Baada ya kuwaona askari hao wawili, ulifanya nini?
Makele: Niliwaamuru wapande kwenye gari nililopanda na askari wale wenye sare na kuwaambia wawe makini na gereji bubu tutakazopita kwani kuna tukio la ujambazi limetokea.
Wakili: Baada ya hapo mlielekea wapi?
Makele: Tuliingia na gari letu kwenye barabara ya Morogoro kisha tukaingia barabara ya Shekilango tulipofika Mugabe, tukaingia kushoto tukaanza kuifuata barabara ya vumbi huku tukiwa tumepunguza mwendo na redio call nimempa, Coplo Abeneth ashike kwa sababu mimi ndiye niliyekuwa naendesha gari.
Wakili: Baada ya kufika eneo la Mugabe, mlielekea wapi?
Makele: Tuliingia ndani kwenye barabara ya vumbi mbele kidogo ukuta wa Posta nikakuta kundi la watu ilikuwa saa moja usiku, nikawasha za gari nikawa nasogeza gari polepole. Nikiwa nakaribia kufikia, lile kundi la askari, mmoja wao (mshitakiwa) alikuwa ameshika SMG, akanisimamisha.
Wakili: Je ulisimama?
Makele: Nilisimama na kushuka na nikajitambulisha kuwa mimi ni Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Urafiki.
Wakili: Baada ya kujitambulisha askari huyo alikueleza nini?
Makele: Aliniambia walikuwa wakifuatilia tukio la BIDCO, lililotokea Samnujoma.
Wakili: Kingine alikueleza nini?
Makele: Aliniambia gari moja nyeupe lilikimbia lakini walifanikiwa kulizuia gari moja yenye rangi ya Blue. Nikawasogelea wale askari, wakaniambia wamewakamata watu wanne na wamewahoji wakawa wanababaika na kwamba wamewakuta na sh milioni tano, wengine wakaniambia ni milioni sita.
Wakili: Sasa wewe kwa nafasi yako baada ya kuelezwa hayo, ulifanya nini?
Makele: Niliwambia hawawezi kuwahoji watu hao sehemu ya wazi kama pale nikawaambia waende nao kituoni kwao Chuo Kikuu wakawahoji.
Wakili: Ulisema hao askari waliokusimamisha walikuwa na Pick Up?
Makele: Ndiyo walikuwa na Pick Up nyeupe.
Wakili: Huyo askari aliyekusimamisha anaitwa nani?
Makele: Morris Nyangerela (ambaye ameachiwa huru wiki iliyopita). Pia nakumbuka siku hiyo askari walikuwa wengi.
Wakili: Wewe ulisema ulielekeza wachukue maelezo ya watuhumiwa hao kwenye umati wa watu, ni kitu gani kingine uliwaelekeza askari hao?
Makele: Kwanza walitaka kumkabidhi fedha mshitakiwa wa tano (Jane) nikakataa nikawaambia hizo ni fedha wazipeleke kwenye kituo chao Chuo Kikuu, wakafanye makabidhiano.
Wakili: Kipolisi eneo la Sinza ni la wilaya gani Kipolisi?
Makele: Ni la Kinondoni. Mimi naongoza eneo la Magomeni ila nilikwenda kwa sababu mimi nilikuwa ni Ofisa.
Wakili: Ulivyotoa amri wapeleke fedha kituoni kwao nini kiliendelea?
Makele: Askari wale wa Chuo Kikuu walipanda gari lao la Pick Up, wengine wakapanda gari la watuhumiwa lenye langi ya Blue na mimi na askari wangu niliotoka nao Urafiki, tuliingia kwenye gari tulilokuja nalo na tukaondoka.
Wakili: Mlivyoondoka na Jane na Abenth, mlielekea wapi?
Makele: Nilichukua Radial Call nikajulisha Control Room kwmaba skari wa UDSM wamekamata watu wanne na fedha sh milioni tano na pisto.
Wakili; Wakati huo ilikuwa ni saa ngapi?
Bageni: Saa moja usiku ila kulikuwa na mwanga wa kutosha kwakuwa nilishawajulisha Control Room kuhusu tukio hilo nilipofika Ubungo Terminal, nikawashusha Jane na Abenth ili warudi ofini kuendelea na kazi hadi asubuhi.
Wakili; Ulielekea wapi?
Makele: Nilielekea Mabibo kule kwenye kituo cha Polisi Kigogo Luhanga, nikarudi Urafiki.
Wakili: Baada ya kufika kituoni ulikuta nini?
Makele: Nilimkuta OCD wa Magomeni-SSP, Isunto Mantage amekaa nje ya kituo nikamsalimia, nikamwuliza vipi akasema anamsubiri afande ambaye akumtaja jina amkabidhi vielelezo.
Wakili: Baada ya OCD kukueleza hivyo ulifanyaje?
Makele: Niliingia ofisini kwangu baada ya dakika 20 nikatoka nje nikakaa kwenye benchi, nikaanza kuzungumza na CID wa zamu .
Wakili: Baadaye kilitokea nini?
Makele: Nilimuona OCS Juma Ndaki, SSP Charle Mkumbo wakiingia kwenye ofisi ya Mkuu wa Kituo hicho.
Wakili; Ulifanyaje?
Makele: Kwasababu walikuwa ni mabosi wangu, Mantage aliniambia niende (CRO) wanipe mkoba.
Wakili; Wewe ulijua huo mkoba unanini ndani yake?
Makele: Sikujua nilikabidhi ofisini ambapo wakubwa wangu walikuwa wamekaa.
Wakili: Nini kilitokea?
Makele: Mkumbo alifungua mkoba akatoa bastora .
Wakili; Zile fedha zilihesabiwa?
Makele: Ndiyo, zilikuwa zikihesabiwa na Mantage na zilikuwa zimefungwa na raba bendi.
Wakili: Zilikuwa kiasi gani baada ya kuhesabiwa?
Makele: Sh. milioni 2.7
Wakili: Mantage alifanya nini?
Makele: Alimkabidhi Bageni sh milioni 2.7 na bastola na bageni alikuwa anakataa kuzipokea kwani OCD Maro alimweleza ni sh milioni tano.
Wakili: Baada ya Bageni kuonyesha kusita, Mkumbo na Mantage walifanyanini?
Makele: Mantage alimuita ‘ulinzi 2’ RCO-Zombe kupitia Radial Call kwamba aje kituoni hapo na mshitakiwa wa kwanza alikuja baada ya muda mfupi.
Wakili: Zombe alipofika alitoa maelekezo gani?
Makele: Kitu alichokifanya Zombe alipofika akasema ‘Mantage umeshindwa kazi’ akafunga mlango akaondoka akatuacha kwenye kikao hicho.
Wakili: Kwa hiyo hata Zombe akuridhika na upotevu huo wa fedha?
Makele: Ndiyo.
Wakili: Baada ya ulinzi mbili 2 (Zombe) kuondoka nini kilitokea?
Makele: Mantage alimkabidhi hivyo vielelezo bageni na akaondoka.
Wakili: Hili suala la BIDCO limekuja lini, ebu tueleze unavyojua wewe?
Makele: Januari 16 mwaka 2006. Binafsi nililisoma kwenye magazeti, nilimuona afande Zombe kashika bastola na fedha, ndiyo nikaanza kujiuliza ‘askari walipambana na risasi na watu hao na nikashangaa kwani watu hao siku hiyo walikamatwa wakiwa hai’.
Wakili: Wewe hujawahi kuhojiwa na tume ya IGP iliyokuwa inaongwa na ACP-Mgawe?
Makele: Sijawahi kuitwa.
Wakili (Jana) juzi mshitakiwa wa pili (Bageni) wakati anatoa ushahidi wake alionyesha kuwa na wewe uliitwa kwenye tume ya IGP, ukatoa maelezo?
Makele: Mtukufu Jaji sijawahi kuitwa kwenye tume hiyo kuhojiwa.
Wakili: Unazungumza nini kuhusu Statement yako iliyopo kwenye tume ya Mgawe?
Makele: Sijawahi kuchukuliwa maelezo na polisi.
Wakili: Ujawahi kuhojiwa na Tume ya Jaji Kipenka Mussa?
Makele; Sijawahi na wala sijui na hata hiyo statement uliyonionyesha leo eti ni yangu, si yangu nasema.
Wakili: Kwa ujumla unazungumziaje hili tukio?
Makele: Minasema kuna mchezo nimefanyiwa aidha ni kwenye Tume ya Jaji Kipenka na hata sijawahi kuchukuliwa maelezo.
Wakili: Imeelezwa kuna askari walifanyiwa sherehe ofisini kwa Zombe, wewe uliudhuria?
Makele: Sikuudhuria na wala sijaambiwa kama askari wangu waliudhulia.
Wakili: Ilielezwa hapa mahakamani, Mkuu wa Kituo cha urafiki Juma Ndaki, aliudhuria sherehe hiyo wewe hukujua?
Makele: Sijui.
Wakili: Kuna Statement iliyoandikwa na mshitakiwa wa 12 (Coplo Rajabu) imekutaja wewe ni miongoni mwa askari waliokwenda kwenye tukio la mauji ya watu hao?
Makele: Si kweli hata huyo Rajabu, nimeanza kumfahamu tulivyokuwa jela. Hivyo hayo maelezo yake ni ya uongo na uenda ndiyo yaliyosababisha mimi kuunganishwa kwenye kesi hii. Kwani hakuna askari wa Urafiki aliyehusika katika tukio hili.
Wakili: Zombe alisema wewe ni miongoni mwa washitakiwa walioandika barua kwa DPP, kweli?
Makele: Si kweli na wala sijawahi kabisa kuandika barua kwa DPP.
Wakili: Wewe kama wewe unazungumziaje upungufu wa fedha uliotokea urafiki?
Makele: Sikuhusika na hivyo vielelezo ila niliambiwa nivitoe hivyo vielelezo ofisi ya CRO na kuleta kwa OCD Mantage, pale Urafiki.
Wakili: Wewe kama wewe unaiomba mahakama ikufanyie nini?
Makele: Naomba mahakam itende haki na maelezo yangu niliyoyatoa kuhusu tukio la BIDCO na si mauaji ya watu hao.
Hata hivyo Jaji Salum Masati baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake saa kumi jioni, aliamuru kesi hiyo iahirishwe hadi Jumatatu asubuhi na mawakili wa upande wa serikali wataanza kumuuliza maswali mshitakiwa huyo.

Akimalizia kutoa ushahidi wake Bageni ambaye alikuwa akiulizwa maswali na wakili Jerome Msemwa, alidai kwamba maelezo aliyoyatoa kwenye tume ya Jaji Kipenka alikuwa akitii amri halali ya kamanda Zombe.

Bageni alidai kwamba mshitakiwa wa 11(Rashid Lema) alivunja Slot Mashine kwenye kantini ya Polisi Oysterbay na kuiba sh elfu 60 wakati juzi mshitakiwa wa kwanza alidai alimuru Lema ashtakiwa kwa kosa la kunja mashine hiyo na kuiba sh milioni tano.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Februari 15 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.