Header Ads

SHAHIDI KESI YA EPA MATATANI

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayomkabili Shabani Maranda na mwenzake, umewasilisha ombi la kutaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, itoe amri ya kukamatwa shahidi wa saba kutokana na kushindwa kufika mahakamani hapo kutoa ushahidi.

Ombi hilo liliwasilishwa jana na wakili wa serikali, Timon Vitalis, mbele ya jopo la Mahakimu wa Kazi watatu - Cypriana William, Saul Kinemela na ahidi huyo kuwa ni wakili wa kujitegemea, Abdallah Kihule.

Vitalis alidai wamefikia uamuzi wa kuwasilisha ombi hilo baada ya shahidi huyo jana kushindwa kutokea mahakamani kutoa ushahidi bila kutoa taarifa za udhuru.

Vitalis alidai Februali 23 walimpelekea hati ya kuja kutoa ushahidi jana na shahidi huyo aliipokea hati hiyo na kuisaini, lakini cha kushangaza ameshindwa kutokea mahakamani.

Hata hivyo, Hakimu Mkazi William alipokea ombi hilo, lakini alisema jopo lake haliwezi kutoa hati ya kukamatwa kwa shahidi huyo kwa sababu hati hiyo ya wito wa kuitwa mahakamani kwa shahidi huyo haikuwa imewasilishwa.

Wakati huo huo, jopo hilo lilitupilia mbali pingamizi la wakili wa utetezi, Majura Magafu, lililokuwa likitaka maelezo ya onyo ya mshitakiwa Rajabu Maranda yasipokelewe na mahakama hiyo kama kielelezo.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu William alisema baada ya kupitia kwa makini hoja za pande mbili, wamebaini hoja za Magafu hazina msingi na badala yake wamekubaliana na hoja za Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, kwamba waliokuwa wajumbe wa timu ya Rais ya kuchunguza wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), kwamba nyadhifa zao hazikuwa zimekoma wakati walipokuwa wajumbe wa timu hiyo.

“Magafu ameshindwa kuonesha ni kifungu gani cha sheria kinatamka kuwa kazi za wajumbe wale zilikoma wakati walivyokuwa wajumbe wa timu ile…hivyo mahakama imeona shahidi wa sita, Mrakibu wa Polisi (SSP) Salum Kisai, alikuwa na uhalali wa kuchukua maelezo ya Maranda kwa sababu ni ofisa wa polisi,” alisema William.

Alisema kuhusu hoja maelezo ya onyo ya Maranda na Farijala kufanana, anatupilia mbali hoja hiyo ya Magafu na kukubaliana na wakili Boniface kwamba kuna maelezo yanafanana, kama miaka ya washitakiwa, kiwango cha elimu na makazi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Februari 28 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.