Header Ads

ZOMBE AGEUKWA

*Mshitakiwa adai alimuelekeza aeleze uongo
* Aeleza Zombe alivyowaandalia sherehe

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA wa pili katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP), Christopher Bageni (45), ameieleza mahakama kuwa, maelezo ya uongo aliyoyatoa kwenye Tume ya Jaji Kipenka Mussa aliyatoa kwa maelekezo ya mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Abdallah Zombe.

Bageni ambaye alianza kujitetea saa 4:31 asubuhi hadi 9:32 alasiri, alitoa maneno hayo baada ya kubanwa na wakili wa serikali Angaza Mwipopo.

Alidai maelezo aliyoandika kwenye Tume ya Jaji Kipenka yalitokana na maelekezo ya Zombe, ambaye alidai alikubaliana naye kwa ajili ya kuwasaidia askari wadogo ambao anashtakiwa nao kwenye kesi hiyo.

“Mtukufu Jaji, niliona huruma nikaamua kuwasaidia askari hao waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji. Na Zombe aliniambia nikiandika maelezo yale Jaji Kipenka atasaidia kuokoa jahazi, kwani amesoma naye Songea Boys,” alidai Bageni.

Alidai Januari 15 mwaka 2006, walipofika ofisini kwa Zombe, alikuta askari wanne wa Chuo Kikuu ambao walikuwa wakifanyiwa sherehe na Zombe ambaye pia aliamuru askari hao wajaziwe fomu za kupewa zawadi au kupendekezwa waongezewe vyeo.

“Nilimuuliza Zombe ni kwanini washtakiwa askari hao ambao wapo chini ya wilaya yangu wajaziwe fomu za kupewa zawadi au vyeo alinijibu ni kwa ajili ya kuweka mambo sawa,” alidai Bageni na kusababisha watu kuangua vicheko huku Zombe akionekana kubadilika sura.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili wa utetezi, Ishengoma na Bageni;
Wakili: Umejiunga lini na Jeshi la Polisi?
Bageni: Mwaka 1988.
Wakili: Ulifanya kazi wapi na kama nani?
Bageni: Kati ya mwaka 1993-1994, nilikuwa Mwendesha Mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kilimanjaro. Kati ya 1994-1996 Mkuu wa Kituo cha Majengo-Moshi na mwaka 2002 niliamishiwa Dar es Salaam kuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala (OCCID) na kati ya mwaka 2004-2006 niliamishiwa na kuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni hadi kesi hii inanikumba.
Wakili: Wewe kama OCCID majukumu yako ni nini?
Zombe: Kusimamia upelelezi wa makosa ya jinai ndani ya wilaya yangu.
Wakili: Tuzungumzie Wilaya ya Kinondoni uliyokuwa ukiiongoza ilikuwa na vituo vingapi vya polisi?
Bageni: Kijitonyama, Kawe, Chuo na Wazo Hill. Na katika hivi vituo kuna msaidizi wangu ambaye anawajibika kwangu.
Wakili: Ukishapata taarifa toka kwa hao wasaidizi wako wewe unapeleka taarifa hizo wapi?
Bageni: Kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kinondoni.
Wakili: Hapa mahakamani, katika kesi hii tumekuwa tukizungumzia tukio la BIDCO, ulishawahi kulisikia?
Bageni: Ndiyo, kwani lilitokea eneo ninalilongoza.
Wakili: Unaweza kuileza mahakama kuhusu tukio hilo?
Bageni: Januari 14 mwaka 2006, saa 1:30 usiku wakati nimerudi ofisini nikitokea kwenye site yangu Pugu, nilielezwa na DC Sajenti Mkushavu kuwa kuna tukio la ujambazi lililotokea barabara ya Sam Nujoma na kwamba waathirika wa tukio la BIDCO tayari wapo kwenye vyumba vya wapelelezi kituoni hapo.
Wakili: Baada ya kuletewa hao Victim kwako ulifanya nini?
Bageni: Niliwahoji kwa dakika tano na wakaniambia wao ni wafanyakazi wa BIDCO na kwamba saa 12 jioni wakati wanatoka kwenye mauzo wakiwa barabara ya Sam Nujoma-Konoike ya zamani, ghafla waliona gari aina ya Saloon inawazuia na walitoka majambazi wanne na walianza kuwatishia kwa bastola na kuwapora sh milioni tano.
Wakati nikiendelea na mahojiano niliitwa na OCD wa Kinondoni, SSP Edward Maro, nikaenda nilipofika nikaanza kumweleza yale niliyoolezwa na wafanyakazi hao, lakini Maro alionyesha kufahamu tukio hilo kuliko mimi. Aliniambia majambazi waliohusika wameishakamatwa akaniambia niende Kituo cha polisi Urafiki, ili nikachukue kielelezo cha sh milioni tano na bastola kwa kuwa vielelezo vilikuwa kwa RCO-Zombe.

Wakili: OCD Maro hakukwambia hao majambazi walikamatwa wakiwa na hali gani?
Bageni: Hakuniambia.
Wakili: Unaweza kukumbuka ilikuwa saa ngapi wakati unafika Urafiki?
Bageni: Saa 11:45 jioni.
Wakili: Maro hakukuambia hao watuhumiwa ni kina nani?
Bageni: Hakuniambia.
Wakili: Wewe ulikwenda Urafiki kama ulivyoagizwa?
Bageni: Ndiyo saa 2:05 usiki nilifika Urafiki na nikamkuta OCD wa Magomeni SSP Isunto Mantage, SSP Charles Mkumbo ambaye kwa sasa ni ZCO wa Dar es Salaam.
Nikiwa nje ya kituo hicho, OCD wa Magomeni alikuja kunipokea alifikiri mimi ni OCD Maro. Tukaongozana kwenye Ofisi ya Mkuu wa Kituo cha Urafiki SSP JUma Ndaki ambaye aliitisha kikao baadaye akaongezeka mshitakiwa wa tatu, ASP Ahmed Makele na baada ya Makele kufika OCD huyo alimtuma Makele akalete vielelezo.
Wakili: Baada ya kuvileta nini kiliendelea?
Bageni: SSP Mantage akafungua mkoba akatoa zile fedha na bastola na alipozihesabu zikawa sh milioni 2.7. Baada ya kutaka kunikabidhi mimi hizo fedha nilimuuliza Mantage mbona ananikabidhi kiasi hicho kidogo cha fedha tofauti na nilichoelezwa na OCD Maro. Niliivyomuuliza hivyo alichukua redio call na kumuita RCO Zombe na baada ya nusu saa Zombe alikuja.
Wakili: Baada ya Zombe kufika nini kiliendelea kwenye hicho kikao chenu?
Bageni: SSP Mantage alimweleza kuhusu upungufu wa fedha hizo.
Wakili: Baada ya hapo?
Bageni: Zombe alikasirika na alitoa amri kwamba ifikapo kesho yake asubuhi kiasi cha fedha kilichopotea katika sh milioni tano kiwe kimepatikana.
Wakili: Zombe alipofika kulikuwa na mahojiano yoyote?
Bageni: Kijeshi, Kamanda akishafisha eneo husika hakuna mahojiano tena. Alitoa amri zipatikane hizo fedha na hakuchukua hata dakika tano akaondoka. SSP Mantage akanikabidhi sh milioni 2.7 na bastola nikarudi navyo ofisini kwangu Oysterbay.
Baada ya muda walikuja askari wa Stand Bay wakanieleza Kijitonyama kuna ujambazi umetokea. Nikachukua Defender nikaongozana na askari wa kitengo cha kupambana na ujamabazi tukaenda Anne Grocery iliyopo Kijitonyama. Tukawahoji watu wakatueleza majambazi waliwavamia na kuwapora vitu vyao na kumjeruhi mmoja wa risasi ambaye alipelekwa Hospitali ya Mwananyamala.
Wakili : Baada ya kupata taarifa hizo ulichukua hatua gani.
Bageni: Nilienda katika hospitali hiyo na askari wangu kwa ajili ya kumjulia hali majeruhi, lakini tukaambiwa yupo Theatre. Dokta akanieleza majeruhi huyo hakupata majeraha makubwa sana kwani risasi haikugusa kwenye mfupa.
Wakili: Baada ya kutoka Hospitali ya Mwananyamala saa 4 usiku ulienda wapi?
Bageni: Nilirudi Oystebay polisi nikamkuta Maro nikamweleza tukio la Kijitonyama, lakini naye aliniambia kuwa amepata habari mpya kuwa waliopora BIDCO wameuwawa.
Nilimuuliza wameuwawa wapi, akaniambia wakati wanapambana na askari Sinza-Palestina.
Wakili: Baada ya hapo?
Bageni: Nilimshauri OCD Maro tukafungue jalada
Wakili: Baada ya kufunguliwa jalada nini kilifuata?
Bageni: Yeye Maro alirudi ofisi kwake na nikiwa ofisi saa 5 usiku wa siku hiyo niilitwa Control Room 999 na kujulishwa ujambazi umetokea Msasani Tirdo. Niliondoka na askari wa ‘Stand By’ kwenda kwenye eneo la tukio na tulipofika tulikuta gari aina ya Corolla limegonga nguzo na gari hilo limeumia vibaya na pembeni kuna mtu ametoka utumbo nje.
Wakili: Hebu tueleze nini kilijiri Januari 15 mwaka huo?
Bageni: Siku hiyo nilipigiwa simu na OCD Maro kwamba nijiandae, ili niende naye kwa mshitakiwa wa kwanza (Zombe). Badaa ya muda mfupi alinipitia na tulipofika akanikabidhi ule mkoba wa vilelezo, ili nibebe tupandishe ngazi kwenye kwenye ya Zombe.
Wakili: Wakati mpo kwenye gari na bosi wako ulimuuliza zile fedha nyingine zilipatikana?
Bageni: Ndiyo, Maro aliniambia hivi ‘wewe unamchezea Zombe’ fedha zilipatikana usiku ule ule.
Wakili: Mlipofika ofisini kwa Zombe mlikuta nini?
Bageni: Tulimkuta na ma-OCD toka wilaya za jiji hili (Dar es Salaam).
Wakili: Baada ya kuingia ofisini kwake nini kilifuata?
Bageni: Niliwakabidhi ule mkoba wenye zile fedha na bastola na baada ya kumkabidhi aliniambia nipeleke kwa OC99 kwa sababu ndiye alikuwa akiaanda Press Conference.
Wakili: Huko OC 99 ulimkabidhi nani?
Bageni: Tawete ambaye ndiye OC 99.
Wakili: Ulisema aliyekwambia watu wanne waliokufa ni Maro, mbona Zombe juzi wakati akitoa utetezi wake alisema taarifa za tukio hilo za kimaandishi alizipata kwako?
Bageni: Kwanza taarifa yenyewe ya kuhusu tukio hilo sijawahi kuiona.
Wakili; Hebu ione hii taarifa (anampa)
Bageni: Mtukufu Jaji, hii si taarifa niliyopeleka kwa RCO Zombe, kwani niliyopeleka kwake inaonyesha nilikabidhiwa sh milioni 2.7 na bastola, wakati hii inaonyesha sh milioni tano na bastola.
Wakili: Ulivyotoka kwa Tawete ulienda wapi?
Bageni; Nilirudi ofisini kwa Zombe namkuta OSS wa Magomeni ameongezeka na skari wengi wa Chuo Kikuu wakipongezwa kwa kazi waliyoifanya.
Wakili: Kazi gani nzuri waliyoifanya?
Bageni: Sikujua ni kazi gani. Wakati huo Zombe alinieleza anakwenda kuzungumza na waandishi wa habari. Wakati nashuka ngazi nilimwuliza OSS wa Chuo Kikuu, Masinde kwanini walipongezwa, alinijibu wao ndiyo walifanikisha kupatikana kwa zile fedha iliyopungua. Nikashtuka nikampigia James Masota nikimtaka afike ofisini haraka na anipeleke eneo la tukio.
Wakili: Alikupeleka?
Bageni: Mtukufu Jaji alinipeleka pale Sinza C ukuta wa Posta, tukakuta matundu sita ya risasi ukutani tukarudi ofisini na tulifika nikamwambia andike maelezo ya eneo hilo.
Wakili; Alikuwa askari gani wa Chuo Kikuu waliokuwepo?
Bageni: Yeye, Mabula, Festo, Nyangelela, Felix na askari wengine waliokuwa wamepangwa Makongo Juu.
Wakili: Kwa nini ulishtuka alivyokwambia hata askari wako walikuwepo kwenye tukio?
Bageni: Nilishtuka kwani Januari 15 walikuwa mapumziko. Askari hao ni mshitakiwa wa 11 na 12, Coplo Saadi na DC Frank ambao wametoroka. Kesho yake niliwaita na kuwahoji kwa nini walikuwepo kwenye tukio la kupambana na majambazi wa BIDCO halafu hawakunipa taarifa.
Wakili: Saad na Frank walikueleza nini kuhusu tukio hilo?
Bageni: Walisema walikuta magari ya 99, lakini hawakunieleza nani aliwauwa kwa risasi marehemu wale wanne.
Wakili: Baada ya kupata hilo jalada ulifanya uchunguzi ?
Bageni:Nilikagua maganda ya risasi siku ya kwanza hakunikabidhi. Kesho yake Saad alikuwa mapumziko na simu yake haipatikani nikaja kumpata baada ya siku nne na nilikabidhiwa na mshtakiwa wa 12 Rajabu.
Wakili: Msitu wa Pande unaujua?
Bageni: Sipajui nilikenda kwa mara ya kwanza na mahakama hii. Hata hivyo msitu huo haupo chini ya eneo langu ipo chini ya wilaya ya kipolisi Magomeni na ningetaka kwenda huko Kikazi ni lazima ningemjulisha mhusika, ili akisikia risasi zinalia eneo hilo asishtuke.
Wakili: Ulivyoenda Ukuta wa Posta ulikwenda na SSP Mmari?
Bageni: Si kweli sikuonana na Mmari. Februari 18 nikiwa kituo cha Salender Brigde ambapo nilikuwa nimekamatwa, Mmari walikuja kwa ajili ya kuandika maelezo yangu niliwakatalia kwa sababu siku hiyo nilikuwa nimepata taarifa za msiba wa dada yangu ambaye alifariki baada ya kusikia nimekamatwa (akaangua kilio).
Wakili: Mmari alivyotoa ushaidi wake alidai alichukua maelezo yako Februa 19 unasemaje kuhusu hilo?
Bageni: Si kweli, kwani asubuhi ndiyo nilikwenda kukabidhi ofisi Oyestebay na RPC-Alfred Tibaina alisema nikabidhi ofisi kwa SP Ramadhani Mkumbi na Inspekta Madaraka.
Wakili:Una ushahidi wa makabidhiano hayo?
Bageni; Ndiyo kwa mujibu wa PGO tunatakiwa kuandika kitu kinaitwa handingover. Ninaomba niitoe kama kielelezo.
Wakili: Wewe mahakamani ulifikishwa lini?
Bageni: Februari 20 mwaka 2006.
Wakili: Maelezo yako ulichukuliwa na nani?
Bageni: Afande Kabere pale Salender Bridge alikuja na kuniambia kesho natakiwa nipelekwe mahakamani, hivyo anataka kuchukua maelezo, pia alinipiga picha.
Wakili: Unazizungumziaje hizi tuhuma kwambe wewe ndiye uliyeamuru askari wawapige risasi marehemu?
Bageni: Ni uongo sana. Kama nilitoa amri kulikuwa na haja gani mimi kuomba nipewe maganda ya risasi?
Wakili: Kuna ripoti ya Tume ya ACP Mgawe ilikuwa na kazi gani?
Bageni: Kurekodi maneno tuliyokuwa tunahojiwa sisi watuhumiwa.
Wakili: Hii ndiyo statement yako uliyoiandika kwenye Tume ya Mgawe. Unaitambua?
Bageni: Mtukufu Jaji, hii si statement yangu.Inaonyesha nimeandika mimi, lakini maelezo yangu yalikuwa katika tume hiyo yalikuwa yanachukuliwa na maofisa wa tume hiyo na wala haina saini yangu. Maelezo yangu yaliandikwa na ACP Essaka Mugasa.
Wakili: Hapa mahakamani ilikuwa inazunguzmiwa ripoti ya Jaji Kipenka Mussa ulishawahi kwenda kutoa maelezo yako?
Bageni: Nilitoa.
Wakili: Statement ya mshitakiwa 11 na 12 (Rashid Lema na Rajabu) walizotoa walisema wewe ndiyo uliyewaongoza kwenda msitu wa Pande. Unasemaje?
Bageni: Jaji nashangaa kabisa, hao watuhumiwa wana nia gani na mimi.
Wakili: Ulishawahi kukwaruzana na washtakiwa hawa?
Bageni: Hapana, Ila Lema aliwahi kuwa dereva wangu na nilikuwa namtuma sokoni kununua nyanya na mwaka 2005 tulitofautiana nikamtoa kwenye udereva.
Nilitofautiana naye kwa sababu alivunja kantini ya pale ofisini na kuiba fedha na nikamfungulia jalada .Kesi yake ilikuwa na ushahidi wa tukio alilolifanya nikamshauri OCD Maro amchukulie hatua za kinidhamu kisha afikishwe mahakamani. RCO Zombe alikuwa na taarifa za tukio lake.
Jalada la kesi yake lilikaa kwa muda mrefu kwa OCD bila kumchukulia hatua na Septemba 2005 akalirudisha kwangu akisema anastaafu hataki kugombana na watu. Mimi sikukubali nikalichukua lile jalada na kulipeleka kwa RCO kwa sababu hatuawezi kukaa na askari jambazi kwenye jeshi letu.
Wakili: Lema na Rama katika maelezo yao walidai walikusikia ukisema ndiyo afande, ndiyo afande ulikuwa unamaanisha nini?
Bageni: Mimi natumia gari binafsi, na siku hiyo wala sikuwa nao nashangaa sana Mtukufu Jaji.
Wakili: Mwisho unaiambia nini mahakama?
Bageni: Mtukufu Jaji, naomba nihukumiwe kwa niliyoyasema hapa. Hayo maneno mengineni cooking story.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili wa Serikali Angaza Mwipopo na Bageni;
Wakili: Taarifa za BIDCO ulizipata wapi?
Bageni: Nilizipata Januari 14 kwa Inchaji wa Standbay, Mkama Mshapu.
Wakili: Juzi Zombe aliambia mahakama fedha alizozikuta kituoni zilikuwa sh milioni 4, milioni moja imepotea akaagiza ipatikane, wewe leo (jana) unasema tofauti. Tuwaelewaje?
Bageni: Mimi ndiyo nazungumza siku ile zilikuwa ni sh milioni 2.7, hayo aliyosema Zombe siyajui.
Wakili; Juzi Zombe alitumbia tukio la BIDCO alisikia saa moja jioni wewe unasema saa mbili usiku tumwamini nani?
Bageni: Yeye alisema na mimi ninasema.
Wakili: Tueleze hilo tukio la kukamatwa majambazi wanne walikamwatwa wapi?
Bageni: Sinza Palestina.
Wakili: Ulikwenda kuchukua vielelezo Urafiki kwanini hukwenda kuwaona majeruhi hao wanne wa ujambazi?
Bageni: Nisingeweza kwenda kuwaona au kuwachukua watuhumiwa hao kwa sbabu tayari nilishachukua maelezo ya victim wa tukio la BIDCO na kwa kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na kuhifadhiwa katika kituo cha Polisi Magomeni.
Wakili: Je hukuona jambo la ajabu ulivyoambiwa watuhumiwa walikamatwa kisha usiku huo huo unaambiwa wameuwawa?
Bageni: Ndiyo, nilishangaa.
Wakili; Kesho yake ulikwenda kuona maiti hizo?
Bageni: Sikwenda.
Wakili: OCD Maro alikwambia watu hao wanne wameuwawa wapi?
Bageni: Eeeh.. sikumuuliza.
Wakili: Wewe ulikuwa OCCID hukuona umuhimu wa kujua ni kwanini waliuwawa?
BAgeni: Mmm…siku hiyo nilikwenda kwenye matukio mengine na ndiyo maana kesho yale niliwaita askari wanipeleke eneo la tukio Sinza C ‘ukuta wa Posta.
Wakili:Usiku ule uliposikia tukio la Kijitonyama, Msasani ulienda kwanini uliposikia watu hao wanne wameuwawa hukwenda..jibu swali tafadhali?
Bageni: Tukio hilo la mauaji ya watu hao liliripotiwa kwa COD Maro, mimi nikaenda kwenye matukio mengine ambapo tuliambiwa kuna mapambano ya risasi.
Wakili: Mbona barua yako hii inaonyesha wewe uliandika Januari 14 mwaka 2006 kwenda kwa OCS 999 lakini wewe unasema uliandika Januari 16?
Bageni: (Kimya…..) ngoja niseme ukweli. Maelezo niliyoyaandika kwenye Tume ya Jaji Kipenka niliandika kwa maelekezo ya Zombe, kwani aliniambia Kipenka ni classmate wake, amemwambia kwa siri tupeleke hayo maelelezo ambayo yatasaidia vijana wake. Niliandika barua hii kwa maelekezo.
Wakili; Kwani nini uliandika maelezo hayo ya uongo kwenye Tume ya rais ya Jaji Kipenka wakati wewe ni mwadilifu na ulitoa maelezo hayo chini ya kiapo?
Bageni: Niliandika barua hiyo kwa ajili ya kusaidia askari wadogo, kwani niliona huruma
Wakili: Unasema kwanini uliona huruma?
Bageni:Niliona huruma ya kuwasaidia kwa sababu askari hao wadogo walikuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji.
Wakili; Tume iliundwa na rais kwa ajili ya kutafuta ukweli, kwa nini wewe ulienda kutoa ushahidi wa uongo na hata leo (jana) inamaanisha unatoa ushahidi wa uongo?
Bageni:Taarifa hiyo niliombwa na mtu nimuandalie.
Wakili: Huyo mtu ni nani mtaje haraka?
Bageni: Ujue jeshini mkubwa akisema ni amri.
Wakili: Ulisema nini kuhusu mauaji ya watu wanne kwenye Tume ya Kipenka?
Bageni: Nilisema nilipokea taarifa toka kwa OCD Maro wale watu waliuwawa.
Wakili; Pale Central Police ulisema ulikuta askari walikuwa wanapongezwa na Zombe ni kina nani?
Bageni: Ninaowakumbuka ni PC Noel, Nyagelela hawa wameachiwa wengine nimewasahau.
Wakili;Wakati wa sherehe hiyo Zombe alisema nini kwa askari hao?
Bageni: Aliagiza askari hao wajaziwe fomu za kupewa zawadi au kupendekezwa wapandishwe vyeo.
Wakili; Tume ya Mgawe iliwasingizia?
Bageni: Maelezo hayo si yangu, kwani yaliandikwa na ACP Mugasa.
Wakkili: Soma hayo maelezo uliyoyatoa kwenye tume ya Mgawe?
Bageni: Jaji, nayasoma haya maelezo, lakini si yangu.Yanasema mimi Christopher Bageni nilipata taarifa za BIDCO kwenye redial Caal na siyo kwa OCD Maro.
Wakili: Katika statement hii ni yapi uliyaeleza katika tume ya Mgawe?
Bageni: Sikusema kitu.
Wakili: Vipi kuhusu tukio la BIDCO hukulieleza kwenye tume ya Mgawe?
Bageni: Niliiambia tume hilo(watu wakacheka).
Wakili: Sasa kwanini unaidanganya mahakama wakati hiyo statement yako inaonyesha ulieleza tukio la BIDCO?
Bageni: Kimya.
Wakili: Zombe, Sidyen Mkumbi, waliambia mahakama kwamba wewe ndiye uliyeongoza mapambano na kuamuru askari wako wako watumie nguvu ya risasi?
Bageni; Sikweli, sijaongoza wala kuamrisha mapambano na Mkumbi hajawahi kunihoji. Mimi nilionyeshwa Sinza ukuta wa posta .
Wakili: Hiyo brief ya kuonyeshwa ukuta wa Posta ulieleza kwenye tume ya Mgawe?
Bageni: Kwa hiyo huyo Zombe na wenzake sijawaambia kwamba mimi ndiye niliyeamuru mapambano.(Zombe alitikisa kichwa na kujiinamia chini).
Wakili: Nikikwambia wewe umekuja hapa kudanganya. Unasemaje?
Bageni: Wewe wasema.
Kesi hiyo inaendelea leo

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februari 13 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.