Header Ads

DC MNALI NI ZAO LA KIKWETE

Na Happiness Katabazi

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Rais Jakaya Kikwete, alimfukuza kazi Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Vijijini (DC), Albert Mnali, kwa kitendo chake cha kuwacharaza bakora walimu, kwa madai kuwa wameshusha kiwango cha elimu katika wilaya yake.


Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa serikali imepokea kwa masikitiko makubwa kitendo hicho cha udhalilishaji wa walimu na kwamba DC huyo amekiuka kanunu za utumishi wa umma.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hiyo Rais Kikwete imetokana na uchunguzi wa kina uliofanywa na kuthibitishwa na Mnali mwenyewe kwamba alifanya hivyo kutokana na uchungu alionao katika suala la elimu.

Taarifa hiyo ilisema kuwa mtumishi yeyote ana haki zake za msingi na kamwe hawezi kufikia hatua ya kudhalilishwa kwa kupigwa kama njia ya kusisitiza uwajibikaji wake kazini.

Wakati taarifa ya Ikulu ikieleza hivyo, mimi napenda kutumia fursa hii kumpongeza Kanali mstaafu, Albert Mnali, kwani ameonyesha uungwana na ushujaa wa hali ya juu kwa kitendo chake cha kukubali hadharani kwamba ni kweli aliamuru walimu wale wacharazwe bakora kutokana na uchungu alionao katika suala la elimu.

Nimelazimika kumpongeza katika eneo hilo la kukiri ukweli ambao umeokoa mamilioni ya fedha za walipa kodi ambayo endapo DC huyo angekana tuhuma hizo, yangetumika kuunda tume kama tulivyozoeshwa na Serikali ya Awamu ya Nne ambayo bila shaka ingechunguza tuhuma hizo. Nampongeza sana kwa ujasiri wake wa kukubali ukweli ambao umesababisha kuvuliwa madaraka.

Nampongeza pia Rais Kikwete kwa uamuzi wa kumtimua kazi Mnali. Kwani ni dhahiri kitendo kilichofanywa naye kimeivunjia heshima Tanzania ambayo inajinasibu kila kukicha kwamba ina viongozi wanaojua wanachokifanya.

Ifahamike kwamba mkuu huyu wa wilaya hakuwa bosi wa wale walimu alioamuru wacharazwe bakora. DC huyu mamlaka yake ni ya kisiasa tu ya Wilaya ya Bukoba Vijijini aliyokuwa akiiongoza. Mamlaka yake hayana uhusiano na wala hayashabihiani na kazi za watendaji na kitaalamu.

Pia mkuu huyu wa wilaya ameonyesha hajui kanuni za adhabu kwa watumishi wa umma, kwa sababu hiyo alikuwa hajui nani anawajibika kwa nani kwani kanuni ya adhabu inatoa adhabu kwa mtu aliyekosea.

Kwa kitendo hicho cha kuamuru walimu wacharazwe bakora, nitakuwa sijakosea nikisema Mnali ni ‘kadikteta ka kijijini ambako kanafikiri’ mtu akikosea bakora ndiyo funzo!

Hatua ya Rais Kikwete kumtimua Mnali ni ya kupongeza, lakini tujiulize, rais wetu alimpata wapi mtu wa aina hii? Kwa sababu watu wa aina hii wanatoa picha ya rais tuliye naye.
Mkuu wa wilaya anamwakilisha rais wa nchi katika wilaya anayoingoza.

Hii inatutisha kidogo na kutufanya tuanze kuamini yale maneno yasomekayo hivi: “Rais Kikwete anaongoza serikali kishikaji.” Maneno haya yalibandikwa kwenye mabango na baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka jana wakati walipogoma kuingia madarasani
Kumfukuza tu mkuu huyu wa wilaya haitoshi, pia anatakiwa achukuliwe hatua zaidi kwani amewajeruhi walimu hao na kuwasababishia maumivu makali katika sehemu zao za mwili.

Pia nilitegemea wazazi wajitokeze wawatetee walimu, lakini hawajajitokeza hadi leo. Hili linaonyesha kuwa nchi yetu bado inahitaji elimu ya uraia na si tu itolewe kwa wananchi bali kwa viongozi wetu pia.

Namshauri rais wetu kwamba awe anaangalia watu wanaofaa kuteuliwa kuwa viongozi. Hatutaki kuanza kumtilia wasiwasi rais wetu kwa sababu huchaguliwa na wananchi lakini hatujawaona wananchi wakijitokeza kumuunga mkono kwa hatua aliyochukua dhidi ya udhalilishwaji wa walimu hawa.

Hata hivyo tusiishie kunyosheana vidole, tunapaswa kutambua kuwa jamii nzima ina matatizo kwani katika masuala ya msingi hatuna mshikamano wa kweli; kwa mfano wanafunzi wa vyuo vikuu wamefukuzwa vyuoni kwa sababu ya kupinga sheria ya uchangiaji, lakini wazazi ambao wengine huumia kutoa hizo karo hawajajitokeza kuwaunga mkono wanafunzi hao!

Nihitimishe kwa kusisitiza kuwa jamii nzima ina matatizo; yatupasa kubadilike na pale kwenye madai ya msingi ambayo yana masilahi kwa taifa wanachi walio wengi tuwe na mshikamano.

Hata hivyo, tunapaswa kujiuliza wepesi huu wa Rais Kikwete kumtimua kazi DC ulitoka wapi?
Ni kwa nini wepesi huu ulishindwa kumjia siku chache zilizopita wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipovunja Katiba aliyoapa kuilinda kwa kusema atakayekutwa ameua albino naye auwawe?

Je, amemfukuza haraka mkuu huyu wa wilaya kwa sababu walimu wa Bukoba walisema watagoma na wangeliandamana au alitoa uamuzi huo kwa sababu tunakaribia kuingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo walimu ndiyo wasimamizi wa uchaguzi huo?
Natoa hoja.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano ,Februali 18 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.