Header Ads

ZOMBE ATAMBA MAHAKAMANI

*Ajitangazia ushindi mapema nje ya Mahakama Kuu
*Adai korti itamwachia uhuru kwa kukosa kesi ya kujibu

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe, ametamba kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania itamwachia huru kwa kuwa hana kesi ya kujibu.

Zombe, alitoa tambo hizo baada ya mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo huku ikiwataka mawakili wa utetezi kuwasilisha hoja za kuomba mahakama iwaachie huru wateja wao kabla ya mahakama kutoa uamuzi wake.

Mshitakiwa huyo alieleza hayo huku akionyesha kablasha alilodai kuwa leo na wakili wake, Jerome Msemwa atalitumia kuiomba mahakama imuachilie uhuru, kwani hana kesi ya kujibu.

“Nyie waandishi wa habari pigeni picha hili kablasha nililobeba kwani kesho(leo)ndiyo wakili wangu atawasilisha mahakamani, ili niachiliwe uhuru kwani sina kesi ya kujibu” alijigamba Zombe huku akicheka na kuonekana mwenye furaha muda wote na kisha kuingia kwenye basi la mahabusu.

Akiahirisha kesi hiyo jana, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Salum Masati, alisema mawaliki hao wanapaswa kuwasilisha hoja hizo kama wanazo baada ya upande wa mashitaka ya kufunga ushahidi wake kwa kuita mashahidi 37.


“Kwa sababu hiyo naamuru kesho(leo), mawakili wa upande wa utetezi kama mnataka kuwasilisha hoja ya kwamba wajeta wenu hawana kesi ya kujibu muwasilishe….kwa sababu ushahidi wa upande serikali natamka rasmi kwamba umefungwa leo (jana),” alisema Jaji Masati.

Kabla ya uamuzi huo, Wakili wa Kujitegemea, Msafiri ambaye anamtetea mshitakiwa wa 11, Rashid Lema, alidai mteja wake ni mgonjwa na ameshindwa kuketi kizimbani kwa sababu ya afya yake ni mbaya, licha amekaa kwenye mahabusu ya mahakama hivyo.

Msafiri alieleza kwa sababu hiyo anaiomba mahakama hiyo iendelee na kesi hiyo chini ya kifungu cha 197(b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985, kinachoruhusu kesi kuendelea bila mshitakiwa kuwepo mahakamani.

Ombi hilo lilikubaliwa na Jaji Masati ambapo alimtaka shahidi wa 22, Mrakibu wa Polisi (SP),Juma Bwire(40), toka Kitengo cha Uchunguzi wa Silaha cha jeshi hilo,J kupanda kizimbani kujibu maswali ya wakili wa utetezi Majura Magafu.

Ifuatayo ni sehemu ya maswali ya kati ya Wakili Magafu na shahidi:

Wakili: Unaweza kukumbuka kuna siku yoyote uliwahi kupata vielelezo(sampo) toka Kituo cha Polisi Oysterbay?
Shahidi: Nakumbuka.
Wakili: Unakumbuka Januari 27 mwaka 2006 uliweza kuandika barua kwa ajili ya kupeleka hizo sampo kwa Mkemia Mkuu?
Shahidi: Nakumbuka.
Wakili: Unaweza kukumbuka hiyo barua yako ilikuwa na refence namba ngapi?
Shahidi: ID/ORAB/10/2006.
Wakili: Ilikuwa inaenda wapi?
Shahidi: Kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Wakili: Kichwa cha habari cha hiyo barua kilikuwa kinasemaje?
Shahidi:Yahusu Maombi ya kufanyiwa uchunguzi wa vielelezo vya kesi namba OB/ID/670/2006.
Wakili: Hiyo kesi ilihusiana na mambo gani hasa?
Shahidi: Ni kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Wakili: Unaweza kuisoma kwa sauti hiyo barua jinsi ilivyokuwa inaelekeza?
Shahidi: Ndiyo. Mnamo Januari 14 mwaka 2006 kulitokea mauaji ya watu wanne na udongo wenye damu ulichukuliwa katika maeneo manne tofauti kulingana na vielelezo hivyo kuna kielelezo vilipewa majina A,B,C na D.
Wakili: Baada ya kutuma vilelezo hivyo kwa Mkemia Mkuu, mlipata majibu yake?
Shahidi: Ndiyo na majibu hayo yalitolewa kwa Timu Uchunguzi iliyoongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Mgawe.
Wakili: Hebu soma hiyo ripoti unaikumbuka?
Shahidi: Siikumbuki.
Wakili: HEbu tizama aliweka saini katika ripoti hii kuna mtu umfahamu hapo?
Shahidi: Kuna saini ya Issack, huyu namfahamu anafanyakazi Ofisi ya Mkemi Mkuu wa Serikali. Saini nyingine siijui.
Wakili: Wewe binafsi uliwahi kuisoma hiyo ripoti?
Shahidi: Sijawahi.
Wakili:Kwenye hiyo ripoti niliyokupa uisome imeandikwa nini?
Shahidi: Imetoka kwa Mkemia Mkuu inakwenda Jeshi la Polisi na iliandikwa Januari 31 mwaka 2006.
Wakili: Hiyo ripoti ya Mkemia Mkuu inahusiana na ripoti yako?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Januari 27 mwaka 2006 ulipokea vifurushi vya vielelezo A,B,C na D toka kwa Mkemia Mkuu, matokeo ya uchunguzi wa vielelezo hivyo yalikuwaje?
Shahidi: Kielelezo A; ni mchanga wenye damu na makundi ya damu hayakutoa majibu.
Wakili: Eeh kielelezo B; matokeo yake yalikuwaje?
Shahidi: Ni damu za watu ila uchunguzi umeshindwa kugundua ni makundi gani ya damu.
Wakili: Kielelezo C?
Shahidi: Ni mchanga na damu, uchunguzi wa kundi la damu haukufanyika kutokana na damu kuwa kidogo.
Wakili: Na kielezo D uchunguzi umebaini nini?
Shahidi: Kilelezo hiki hakikuwa na damu ya binadamu, bali kilikuwa mchanga.
Wakili: Kwenye barua yako kwenda kwa Mkemia MKuu ulisema kesi hii ni kesi gani vile?
Shahidi: Unyang’anyi wa kutumia silaha.
Wakili: Wewe leo hii unatoa ushaidi katika kesi ipi?
Shahidi: Kesi ya mauaji.
Wakili: Ulisema wewe unafanyakazi katika kitika Kitengo cha Uchunguzi wa Silaha, ilikuwaje barua hiyo ya kupeleka vielelezo hivyo kwa Mkemia Mkuu ikafika kwako?
Shahidi: Januari 27 mwaka 2006 nakumbuka nikiwa ofisini alikuwa Inspekta Mwakajinga, alikuja na vielelezo hivyo na maelezo mafupi kwamba aliambia na viongozi wake, akatembelee eneo la tukio ndipo akamapata vilelezo na akaambiwa vielelezo hivyo avilete kwenye kitengo chetu cha Uchunguzi wa Silaha, ili viandikiwe barua kwenda kwa Mkemia Mkuu ndipo mimi nilipopewa barua hiyo nakuipeleka kwa kwa Mkemia Mkuu.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Mzee wa Baraza na Shahidi:
Mzee wa Baraza: Vielelezo hivyo vilitolewa wapi?
Shahidi: Vilidaiwa kutolewa eneo la tukio Sinza.
Mzee wa Baraza: Unataka kuiambia mahakama kwamba vielelezo vinatokana na uchunguzi wa kina wa ACP-Mgawe?
Shahidi: Kabisaa.

Kuitwa tena kwa shahidi huyo mahakamani kulitokana Wakili Magafu, Septemba 26 mwaka jana, kudai kuwa kwa niaba ya washtakiwa wanaotetewa na kwa mujibu wa kifungu cha 147(4) cha Sheria ya Ushahidi , upande wa utetezi uliomba shahidi Bwire, aitwe tena, ili atatue utata uliojitokeza katika ushahidi wa Mkemia Mkuu Daraja la Pili.

Aidha, baada ya kuairishwa kwa kesi hiyo waandishi wa habari walimshuhudia mshitakiwa Rashid Lema akiwa hawezi kutembea mwenyewe, kwani alikuwa ameshikiliwa na kutembezwa taratibu na kupandishwa kwenye basi la mahabusu kuelekea Gereza Keko. Mshitakiwa huyo alionekana akiwa amenyoa upara na kichwa kimevimba kutokana na kuwa na majipu kadhaa.

Mbali na Zombe na Bageni washitakiwa wengine ni Ahmes Makelle, Noel Leonard, Jane Andrew,Moris Nyangerela,Emmanuel Mabula na Felix Cedrick.

Wengine ni Koplo Michael,D.2300 Abeneth, Koplo Rajabu, Rashid Leman a Festus Chenge.

Washtakiwa hao wanadaiwa Januari 14,mwaka 2006 katika msitu wa Pande uliopo huko Mbezi Louis, nje ya Jiji la Dar es Salaam, waliwaua Ephraim Chigumbi,nduguye Sabinus Chigumbi , Mathias Lukombe na Juma Ndugu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Februari 4 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.