Header Ads

UMEME WAKWAMISHA KESI YA EPA

• TANESCO yatoa sababu ya kukatika

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi, Kisutu Dar es Salaam, jana ilishindwa kuendelea kusikiliza kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (EPA), inayomkabili Farijala Hussein, kutokana na tatizo la umeme.

Kesi hiyo pia inamhusisha Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kigoma, Rajab Maranda.

Naibu Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Cypriana William anayesaidiana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Phocus Bambikya na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Saul Kinemela, walikubaliana na hoja ya Mwanasheria Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, ya kutaka kuahirishwa kwa kesi hiyo namba 1161/2008, baada ya kutokea kwa tatizo la umeme.

Awali, Stanslaus aliomba jopo hilo liahirishe kesi hiyo kutokana na mfumo wa kompyuta na vipaza sauti vinavyotumia umeme wakati wa kuendesha kesi hizo kwa lengo la kurekodi mwenendo wake kushindwa kufanya kazi.

“Naiomba mahakama iahirishe kesi hii kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme ambao umekuwa ukisaidia kompyuta na vipaza sauti kurekodi mwenendo mzima wa kesi hii, tangu ilipoanza, hivyo naomba ihairishwe hadi kesho,” Boniface Stanslaus alitoa ombi hilo.

Wakili wa utetezi, Majura Magafu, alikubaliana na ombi hilo na kutoa udhuru kwa jopo hilo kwamba leo atakuwepo Mahakama Kuu katika kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe, na yeye ni miongoni mwa mawakili wa utetezi katika kesi hiyo.

Majura aliomba kesi hiyo iahirishwe hadi Ijumaa wiki hii, ombi ambalo lilikubaliwa na hatimaye kesi hiyo kuahirishwa hadi siku hiyo.

Jana shahidi wa tano, ambaye ni mchunguzi wa maandishi, Maabara ya Upelelezi Kitengo cha Forensic Bureau ya Jeshi la Polisi nchini, C. 8565 Station Sergeant Othuman (49) alifika kwa ajili ya kuhojiwa na wakili wa upande wa utetezi. Mashahidi watano kati ya 17 wameishatoa ushahidi wao.

Katika kesi hiyo, Farijala na Maranda kati ya mwaka 2003-2005, wanadaiwa kuiibia BoT jumla ya sh bilioni 1.8 kwa kutumia kampuni yao ya Kiloloma & Brothers kwa madai kuwa Kampuni ya B.C Cars Export Ltd ya Mumbai-India, imeiruhusu kampuni yao kukusanya madeni.

Licha ya kesi hiyo, Maranda anakabiliwa na kesi nyingine ya wizi wa sh milioni 207 mali ya BoT.

Kesi hiyo ambayo imeshaanza kusikilizwa, inamhusisha pia Iman Mwakosya, Ester Komu na Bosco Kimela, wote wakiwa maofisa wa BoT na katika kesi ya tatu, anakabiliwa na mashtaka ya wizi, kughushi na kujipatia jumla ya sh bilioni 2.2.

Wakati Mahakama ya Kisutu ikisimamisha kesi ya EPA kutokana na kukatika kwa umeme, Shirika la Umeme nchini (TANESCO), limesema hali hiyo iliyolikumba Jiji la Dar es Salaam jana, ilitokana na hitilafu ya kiufundi iliyotokea katika kituo cha kupokelea umeme cha Ilala, anaripoti Mwandishi, Deogratius Temba.

Taarifa iliyotolewa jana na Meneja Mawasiliano wa shirika hilo, Badra Masoud, ilisema kituo hicho kinachopokea umeme kutoka katika mitambo ya Ubungo, kilipata hitilafu hiyo jana asubuhi na kusababisha baadhi ya maeneo ya jiji kukosa umeme kwa muda mrefu.

Alisema hitilafu hiyo imesababisha baadhi ya vifaa kuungua na hadi jana jioni chanzo cha hitilafu hiyo kilikuwa hakijajulikana licha ya mafundi wa TANESCO, kuendelea kutengeneza mitambo hiyo ili umeme uweze kurejea katika hali yake ya kawaida.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Februari 3 mwaka 2009
..Kesi ya Zombe imeanza leo Mahakama Kuu.

No comments:

Powered by Blogger.