Header Ads

LIYUMBA ATOWEKA

*Korti yatoa hati ya dharura kumkamata
*Polisi, Takukuru wamsaka bila mafanikio
*Wadhamini watiwa mbaroni, hatima yao leo

Na Happiness Katabazi

UVUMI umezagaa jijini Dar es Salaam kuwa mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kusababisha hasara ya sh bilioni 221, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba, ametoroka.


Mbali na Liyumba, mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Meneja Mradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka, ambaye hadi sasa bado yuko rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Kutokana na uvumi huo, juzi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ililazimika kutoa hati ya dharura ya kukamatwa kwa mshitakiwa huyo na wadhamini wake wawili.

Hata hivyo vyanzo vyetu vya habari vilidai kuwa mshitakiwa huyo aliitwa kwa hati ya dharura mahakamani, huenda kutokana na mazingira ya utata wa dhamana yake, kwani alidhaminiwa kwa hati ya mali ya sh milioni 882, badala ya mali zenye thamani ya sh bilioni 55.

Vyanzo vya habari kutoka serikalini, viliiambia Tanzania Daima jana asubuhi kuwa vilipata taarifa kwamba, Liyumba alikuwa amepanga njama za kutoroka, huku vyanzo vingine vikidai kwamba alikuwa amepanga njama za kusingizia kuumwa, kwani alipata taarifa kuwa upande wa serikali umechukizwa na jinsi taratibu zilivyokiukwa za kumpatia dhamana na upande wa mashitaka ulikuwa umepanga kuwasilisha hoja ya kutengua dhamana yake.

“Hizo taarifa tumezisikia na tunazifanyia kazi kwa karibu, ila nakuhakikishia hati yake ya kusafiria iliwasilishwa mahakamani jana (juzi), kwani serikali imekerwa na jinsi taratibu zilivyokiukwa kumpatia dhamana na hadi sasa jalada la kesi yake limeitishwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kupitiwa.

“Kwa hiyo jalada likirudishwa Kisutu, mambo yatabadilika juu yake, kwani dhamana yake imeshtua wengi, wakiwemo maofisa wa juu wa mahakama,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Hata hivyo, jana saa sita mchana wadhamini wake wawili ambao ni wafanyakazi wa BoT, Otto Agatoni, Ofisa Usalama wa Ndani ya Benki hiyo na Benjamin Ngulugunu, ambaye ni mhasibu, walikamatwa na kuswekwa katika mahabusu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuanzia majira ya saa sita mchana hadi saa 10:32 jioni, walipopandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo.

Wakili wa Liyumba, Hudson Ndusyepo, alimweleza Hakimu Msongo kuwa licha ya mahakama kutoa hati ya dharura kukamatwa kwa mteja wake, hakufika mahakamani, lakini hakutoa sababu za Liyumba kutofika mahakamani hapo.

Kwa upande wake, wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Tabu Mzee, alidai kuwa walipokea hati ya dharura ya kukamatwa kwa Liyumba na wadhamini wake wawili jana na taasisi hiyo ilifanikiwa kuwakamata wadhamini hao, lakini jitihada za kumtafuta Liyumba kwa siku nzima ya jana, zilishindikana.

“Tulipokea hati ya mahakama ya kumkamata mshitakiwa Liyumba na wadhamini wake. Tumefanikiwa kuwakamata wadhamini hao, lakini jitihada zetu za kumkamata Liyumba zilishindikana baada ya kumtafuta kwa njia zote, ikiwamo ya simu ya mkononi bila mafanikio,” alidai Tabu.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Msongo aliwaeleza wadhamini wa Liyumba kuwa yeye ndiye aliyetoa amri ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo, lakini alisema hawezi kuzungumzia chochote kwa sababu jalada la kesi yao limeitishwa Mahakama Kuu.

“Mahakama hii ndiyo imetoa amri ya kukamatwa kwenu na kwa sababu jalada la kesi ya msingi limeitishwa Mahakama Kuu, siwezi kuzungumza chochote leo, naahirisha hadi kesho (leo), saa nane mchana na nyie wadhamini mfike bila kukosa,” alisema Hakimu Msongo.

Kutokana na uamuzi huo, wadhamini hao waliachiwa huru kurudi majumbani kwao, huku wakionekana kutoamini kilichowatokea.

Kabla ya kupewa dhamana, Liyumba, alikwenda Mahakama Kuu kuomba alegezewe masharti ya dhamana hiyo iliyomtaka atimize masharti ya hati za mali au fedha taslimu sh bilioni 55, wadhamini wawili, kuwasilisha hati ya kusafiria, kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama na kila Ijumaa kuripoti katika Ofisi ya Takukuru.

Hata hivyo, Mahakama Kuu, Ijumaa iliyopita, chini ya Jaji Projestus Lugazia, ilitupilia mbali ombi hilo, kwa madai kuwa haoni sababu za kutengua masharti ya dhamana yaliyowekwa na Mahakama ya Kisutu.

Baada ya maombi hayo kutupwa, Liyumba Jumatatu wiki hii, aliwasilisha hati za dhamana zenye thamani ya sh bilioni 55, ambazo hata hivyo zilipingwa na mawakili wa serikali, kwa madai kuwa zilikuwa na kasoro.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda, alipinga hati hizo kwa madai kuwa zina makosa mbalimbali, hivyo zinapaswa kurekebishwa kabla ya mshitakiwa huyo kupatiwa dhamana.

Alizitaja kasoro nyingine kuwa hati za mali hizo, zimechanganywa kati ya mali zinazohamishika na zisizohamishika, hivyo kuwafanya washindwe kujua ukweli wa thamani zake.
Pia alidai baadhi ya hati zina jina moja la mmiliki na kusababisha kutoziamini.

Hata hivyo, Jumanne wiki hii, Hakimu Msongo kwa mshangao wa wengi, alimpatia dhamana mshitakiwa huyo baada ya kuwasilisha hati zenye thamani ya sh milioni 882, badala ya sh bilioni 55.

Liyumba na Kweka, wanakabiliwa na matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuidhinisha ujenzi wa minara pacha ya BoT, maarufu kama ‘Twin Towers’ na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 20 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.