Header Ads

SHAHIDI AKIRI RIPOTI KUWA NA DOSARI

Na Happiness Katabazi

MCHUNGUZI wa Maandishi, Maabara ya Upelelezi Kitengo cha Forensic Bureau ya Jeshi la Polisi nchini, C.8565 Station Sajent, Othuman (49), ambaye ni shahidi wa tano katika kesi ya wizi wa sh biloni 1.8 za EPA, inayomkabili Farijala Hussein na Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma, Rajab Maranda, jana alikiri kwamba ripoti yake ina dosari za kisarufi.

Othuman alifikia uamuzi huo wa kukiri baada ya wakili wa utetezi Majura Magafu kumhoji ni kwanini katika ripoti yake imetaja namba tano na saba wakati hazipo kwenye ripoti hiyo.

“Ndugu shahidi kwa makosa hayo huoni kwamba itasababisha tushindwe kuimani ripoti yako kwa sababu wewe mwenyewe umekiri mbele ya mahakama kwamba ina dosari hizo za kisarufi,” alihoji Magafu.

Shahidi huyo alisema: “Nakiri makosa yametokea katika uchapaji wa ripoti hiyo na kuwepo kwa makosa hayo hakuwezi kuondoa maana nzima ya ripoti niliyoiandaa. Ninaomba hayo masahisho yafanyike kwani hata mimi ndiyo nimekuja kuyabaini hivi sasa,” alidai Othuman.

Aidha, katika hatua nyingine Magafu alihoji kitendo cha Ofisa wa Polisi, Salum Kisai kupeleka majalada yenye picha za washtakiwa na majina yao kwa shahidi ambaye ndiye alikuwa akichunguza saini iliyowekwa kwenye hati ya usajili wa kampuni ya Kiloloma & Brothers kama ni ya Afisa Mtendaji Mkuu wa (BRELA), Esteriano Mahingira au la.

Magafu alidai kwa mujibu wa sheria ya ushaidi na General Police Order inakataza mchunguzi kujua majina au kuona picha za watuhumiwa ambao wanatuhumiwa kughushi maandishi na kueleza kwamba Othuman alipewa vitu hivyo na wapelelezi wa kesi hiyo jambo alilodai limekwenda kinyume na sheria hizo.

Alidai hali hiyo inasababisha aone majibu ya ripoti ya shahidi huyo yanaendana na maelekezo aliyopewa na Kisai, jambo ambalo lilipingwa na shahidi huyo kwamba kwa mujibu wa sheria ya kazi yake utambuzi huwa anashughulika na maandishi yanayopishaniwa na siyo picha wala majina ya watuhumiwa.

Naibu Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Cypiriana William ambaye anasaidiana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Phocus Bambikya na Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Saul Kinemela aliahirisha kesi hiyo hadi Febriari 23 mwaka huu, ili kumpa nafasi Wakili Magafu kuhudhuria kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake 12.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Februari 7 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.