Header Ads

MALUMBANO YASITISHA KESI YA EPA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ililazimika kisitisha kuendelea kusikiliza ushahidi uliokuwa ukitolewa na shahidi wa sita Mrakibu wa Polisi(SSP) Salum Kisai(45), katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 katika Benki Kuu(BoT), kufuatia kuibuka malumbano makali ya kisheria kati ya upande wa serikali na utetezi.

Naibu Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Cypiriana William ambaye anasaidiana Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Phocus Bambika na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Saul Kinemela, alisema amekubalina na hoja ya Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface na kwamba anasitisha usikilizaji wa ushahidi wa shahidi huyo hadi leo.

Baada ya malumbano hayo ya kisheria, Boniface aliiomba mahakama kuwa iwepo kesi ndani ya kesi ili wakili wa utetezi, Majura Magafu aweze kuleta mashahidi na vielezo ambavyo vitaunga mkono pingamizi lake la kuiomba mahakama hiyo isipokee maelezo ya onyo aliyochukuliwa mshitakiwa wa pili Farijara Hussein kwenye Kikosi Kazi(Task Force), kwasababu mshitakiwa huyo ameyakana maelezo hayo, saini siyo yake,na kwamba anachokifahamu mteja wake ni kwamba aliandika maelezo ya onyo akiwa na watu wa nne na siyo watu wawili kama ilivyodaiwa na shahidi huyo.

“Jopo hili linakubalina na hoja msomi Boniface na kwasababu hiyo kwamba kuwepo na kesi ndani ya kesi na kwasababu hiyo jopo hili haliwezi kuendelea kusikiliza ushahidi wa shahidi huyu hadi kesho(leo) ambapo wakili Magafu atakapokuja kuleta ushahidi utakaoonga mkono pingamizi lake la kutaka jopo hili lisipokee maelezo ya onyo kama kielelezo” alisema William.

Kabla ya malumbano hayo kuibuka , Wakili Boniface alimwongoza Kisai kutoa ushahidi wake.Na ifuatayo ni mahojiano kati ya wakili huyo wa serikali na shahidi;
Wakili:Shahidi iambie mahakama unafanyakazi wapi?
Shahidi:Jeshi la Polisi.
Wakili:Kama nani?
Shahidi:Kama mpelelezi toka Makao Makuu ya Upelelezi.Na nina cheo cha Mrakibu wa Pilisi.
Wakili:Ulijiunga na jeshi hilo lini?
Shahidi:1982.
Wakili:Si vibaya ukiambia mahakama kiwango chako cha elimu?
Shahidi:Shahada ya Sheria toka Chuo Kikuu Huria.
Wakili:Huko kwenye Idara ya Upelelezo kutoka kitengo maalum unashughilikia nini?
Shahidi:Wizi uhausiana na masuala ya kughushi.
Wakili:Kuna kitu kinaitwa Kiloloma &Brothers unakifahamu?
Shahidi:Ndiyo.
Wakili:Lini?
Shahidi:Wakati naendelea na Upelelezi wa kesi za EPA.
Wakili:Upelelezi wa Kesi za EPA ulinaza lini?
Shahidi:Ulianza Januari 2008.
Wakili:Huu upelelezi uliusisha watu gani?
Shahidi:Uliusisha kikosi kazi(Task Force).
Wakili:Iliundwa na Taasisi gani?
Shahidi:Polisi, Takukuru na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wakili:Ofisi za Task Force zilikuwa wapi?
Shahidi:Mikocheni.
Wakili:Na hii Kiloloma &Brothers Enterprises uliifahamu vipi?
Shahidi:Niliifahamu wakati wa upelelezi wa kesi za EPA.
Wakili:Upelelezi wenu ulionyesha Kiloloma&Brothers, wamiliki wake ni wakina nani?
Shahidi: Ulionyesha wamilikiwa wake ni washtakiwa waliopo kizimbani,Farijara Hussein na Rajabu Maranda.
Wakili:Upelelezi huo huo ulionyesha nini kuhusu Kiloloma&Bros, nani ni wamilikiwa wake?
Shahidi:Ulionyesha jina la biashara lililosajiliwa rasmi na BRELA.
Wakili:Vipi kuhusu Kiloloma &Bros nani alikuwa mmiliki wake?
Shahidi:Charles Issac ndiyo mmiliki wake.
Wakili:Sasa ulipogundua Kiloloma&Bros imesajiliwa kihalali na Kiloloma&Brothers haijasajiliwa kihalali ulifanya nini?
Shahidi:Nilitafuta wamiliki wake.
Wakili:Utafutaji wa wamiliki hao uliishia wapi?
Shahidi:Niliwatafuta washtakiwa ambao wapo leo(jana) kizimbani.
Wakili:Mahakama inangependa kujua ni namna gani uliwapata?
Shahidi:Tulitumia Anwani zao na kuwapata,kama mshitakiwa wengine tunavyowapata.
Wakili:Washtakiwa hawa tafadhari ulipataje?
Shahidi:Nilitumia namba zao za simu na mshitakiwa wa kwanza Maranda, ilikuwa ikipatikana.Nilimpigia simu hakapatikana na nikamjulisha anaitajika polisi.
Wakili:Yeye alifanya nini baada ya kumweleza hivyo?
Shahidi:Aliitikia wito akataka kujua nipo wapi,nikamwambia anatakiwa Task force na nikamjulisha afike karibu na Karibu Hoteli , ataona mimi na wenzangu tumeegesha gari pembeni.
Wakili:Mshitakiwa alifanya hivyo?
Shahidi:Ndiyo.
Wakili:Mlikuwa wangapi kati hilo gari?
Shahidi:Wanne.Maofisa wa polisi wawili na yaani mimi na SSP-Sifael Mkonyi na maofisa wa Takukuru wawili, Wandwe na Mushi.Tulijitambulisha kwa mshitakiwa tukamtaka aongozane na sisi kwenye ofisi za Kikosi Kazi(Task Force) zilizopo Mikocheni.
Wakili:Mlipofika Mikocheni mlifanya nini?
Shahidi:Nilianza kumhoji kwmaba yeye anaishi wapi.
Wakili:Ebu tuje kwenye mmiliki mwingine wa Kiloloma &Brothers, Farija, mlipataje?
Shahidi:Wakati tunamtafuta alikuwa hapatikani kwenye simu na hata nyumbani kwake.
Wakili:Sasa mlifanyaje?
Shahidi:Tuliendelea kumtafuta kupitia serikali za mtaa anaoishi bila mafanikio.Na kumbuka siku moja tarehe nimeisahau Farijara alijitokeza na kujisalimisha pale Makao Makuu ya Polisi.
Wakili:Ilikuwaje alivyojisalikisha?
Shahidi:Alipofika Polisi alikutana maofisa wa polisi, na walitujulisha yule mtuhumiwa tuliyekuwa tukimtafuta kajisalimisha.Nikamfuata pale Makao Makuu ya Polisi na akajitambulisha kwamba anaitwa Farijala Shaban Hussein.Alisema ameamu kujisalimisha kwasababu amekuwa akitafutwatafutwa sana.
Wakili:Aliendelea kubaki polisi?
Shahidi:Hapana, nilimchukua nikampeleka kwenye ofisi ya Kikosi Kazi Mikocheni.
Wakili:Ebu ieleze mahakama Oktoba 3 mwaka 2008 asubuhi ulikuwa wapi?
Shahidi:Nilikuwa ofisini Mikocheni nikiendelea na kazi ya Uchunguzi.
Wakili:Siku hiyo kati ya washtakiwa hao alifika ofisini hapo?
Shahidi:Alifika Farijara Hussein na alifika mbele yangu.
Wakili:Ulifanya nini?
Shahidi:Nilianza rasmi kujitambulisha kwake kuwa mimi ni ofisa wa Polisi na nilimtaadhalisha nataka kuchukua maelezo yake ya onyo kuhusiana na tuhuma zonazomkabili za kughushi maandishi, kutoa taarifa za uongo.Nilimtaadharisha pia maelezo atakayotoa ayatoe kwa hiari yake na kwamba yataweza kutumika mahakamani.
Wakili:Yeye alikujibu nini?
Shahidi:Alinijibu yupo tayari kwa hiari yake kabisa kutoa maelezo hayo ya onyo.
Wakili:Wakati huo wewe ulikuwa na nani?
Shahidi:Nilikuwa mimi nay eye tu kwenye chumba maalum kwaajili ya kuchukulia maelezo ya watuhumiwa wa EPA.
Wakili:Ulivyomaliza kuandika maelezo yake ulifanyaje?
Shahidi:Niliandika muda wa kumaliza kuandika maelezo hayo na nilidhibitisha maelezo hayo niliandika kwa usahihi kama alivyonieleza.
Wakili:Tazama hilo kabla ni la nini?
Shahidi:Hili ni kablasha la hati ya onyo la Farijala niloandika maelezo yake mimi.
Wakili:Unapenda ulitoe mahakamani kama kielelezo?
Shahidi:Ndiyo.
Baada ya kusema hayo, Magafu alinong’onezana na mteja wake Farijala na kisha alisimama na kupinga maelezo hayo yasipokelewe na jopo hilo kwasababu mteja wake siku alipohojiwa kuliwa na watu wa nne akiwemo wakili wa serikali Biswalo Mganga ambaye jana alikuwa ni miongoni mwa mawakili wa serikali waliokuwa wakimsaidia Stanslau Boniface.

Na kwamba Farijala aliwahi kuitwa na kusaini maelezo ambapo hadi leo hii hajawahi kuitwa kusomewa.Kesi hii itaendelea leo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Februali 24 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.