Header Ads

'ZOMBE ALITUPONGEZA KWA KAZI'

*Watuhumiwa wadai hawakujua kwa nini wanapongezwa

Na Happiness Katabazi

WASHTAKIWA wawili katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja wamedai mahakamani kuwa walishangazwa na kitendo cha kupewa mkono wa pongezi kwa kazi nzuri waliyofanya na aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Abdallah Zombe.


Washtakiwa hao, Emmanuel Mabula (49) na Michael Shonza (45), walidai zaidi hawakujua pongezi hizo zilikuwa za kazi gani.

Wote wawili walikuwa wakifanyakazi Kituo cha Polisi, Chuo Kikuu, cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani.
Mbali na washtakiwa hao, mshtakiwa wa tano katika kesi hiyo, Jane Andrew (31), wa kituo cha Urafiki, naye alitoa ushahidi wake mahakamani hapo jana mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Massati.
Kwa upande wa Mabula na Shonza, wamedai mahakamani hapo kwamba Januari 15, 2006 walipelekwa na mkuu wa kituo chao cha kazi, Sebastian Masinde, ofisini kwa Zombe; walipofika Zombe aliwapa mkono wa pongezi kwa kazi nzuri waliyokuwa wameifanya.
Katika maelezo yao ya ushahidi, walidai kuwa siku hiyo walishangazwa na kitendo cha wao kupewa mkono wa pongezi kwa sababu hawakuwa wamejua wamefanya kazi gani hata kustahili kupelekwa kwa RPC ili kupongezwa.
“Mtukufu Jaji ni kweli siku hiyo tulipewa mkono wa pongezi na Zombe kwa maelezo kwamba tulifanya kazi nzuri lakini hata hivyo nilishangaa ni kazi ipi nzuri niliyofanya hadi nipewe pongezi,” alidai Mabula.
Kwa upande wake Jane Andrew yeye amedai kwamba hakwenda kupongezwa. Lakini hata hivyo baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka walidai kuwa siku ya tukio (Januari 14 , 2006), walimshuhudia Jane akigombea mfuko wa fedha za marehemu; hata hivyo alikana tuhuma zote zilizoelekezwa kwake.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili Majura Magafu, Jane alikana kuandika maelezo katika Tume ya ACP Mgawe na Tume ya Jaji Kipenka Mussa, licha ya Wakili wa Serikali, Jasson Kaishozi, kumuonyesha maelezo yake aliyoyaandika katika nyaraka za tume hizo kwa nyakati tofauti kabla hajafikishwa mahakamani.
“Mtukufu Jaji hizo ‘statement’ toka Tume ya Mgawe na Jaji Kipenka sizijui, nashangaa wakili huyu ananing’angania kwamba niliziandika mimi. Nimesema siyo zangu…mimi nilihojiwa kwenye tume moja tu ya shahidi wa 36, Sidyen Mkumbi.
“Hivyo hizo statement sijui kabisa na wala usinipe nizisome kwani siyo zangu. Na hili tukio la mauji ambalo limesababisha nishtakiwe kwenye kesi hii mimi silijui na ninaomba mahakama hii itende haki,” alidai mshtakiwa huyo.
Hata hivyo, wakili Kaishozi alimhoji kwamba awali alipoanza kutoa ushahidi wake alidai aliandika maelezo kwenye tume moja ya Mkumbi lakini baadaye akasema alipata taarifa za tukio la mauji ya watu hao alipoitwa kwenye Tume ya Kipenka. Baada ya kuulizwa swali hilo mshtakiwa alijibu kwa sauti ya juu, “Mtukufu Jaji nimeishamweleza huyu wakili wa serikali kuwa mimi nilihojiwa kwenye tume moja tu hivyo hizo statement anazodai zina melezo yangu siyo zangu,” alidai Jane kwa ukali.
Jane aliendelea kudai mahakamani kuwa alisoma na kuishia kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Sangu-Mbeya na aliijiunga na Jeshi la Polisi mwaka 2000 kwa sababu alikuwa na sifa ya kuwa mwanamichezo.
Ifuatayo ni mahojiano kati ya wakili Majura Magafu na mshtakiwa wa saba, Emmanuel Mabula.

Wakili: Uliajiriwa na Jeshi la Polisi lini?

Mabula: Mwaka 1982 na mwaka 1987 nikahamishiwa Kituo cha Polisi Urafiki hadi matatizo haya yananikumba.

Wakili: Januria 14 mwaka 2006 ulikuwa wapi?

Mabula: Kuanzia asubuhi nilikuwa nyumbani hadi saa 12 kasorobo jioni.

Wakili: Ulipofika muda huo ulielekea wapi?

Mabula:Nilivaa sare za kazi nikaelekea ofisini.

Wakili: Ulipofika kituoni nini kilitokea?

Mabula: Nilimkuta na Mkuu wa Upelelezi wa kituo hicho, Station Sajenti James Masota, ambaye aliitisha foleni na alitoa maelekezo kwamba tupande Pick Up rangi ya bluu.

Wakili: Unakumbuka idadi ya askari uliokuwa nao kwenye hilo gari?

Mabula: Nane.
Wakili: Majina yao unayakumbuka?

Mabula: Naweza kuyakumbuka. DC. James Masota; mshtakiwa wa nne, sita na nane (PC Noel Felix na Koplo Moris Nyangerela) ambao wameachiwa huru; na Koplo Festus, PC Michael Shonza na mimi.

Wakili: James aliwaelekeza muelekee wapi?

Mabula: Gari liliwashwa tukaelekea Changanyikeni halafu likaelekea Makongo juu na James alikuwa amekaa mbele akatoa shingo na kusema yeye na Michael watelemke ambapo Michael Shona alikuwa na bunduki.

Wakili: Kuna maelekezo mengine aliyatoa?

Mabula: Alituambia sisi eneo letu la doria ni Makongo na hayo maelekezo alitupea pale pale Makongo.

Wakili: Mlifanya doria hadi saa ngapi?

Mabula: Saa 11 alfajiri tukaanza safari ya kurudi ofisini na tulifika saa 12 asubuhi.

Wakili: Katika eneo lenu la doria hakukutokea tukio lolote?

Mabula: Hakukutokea tukio lolote.

Wakili: Mlipofika kituoni mliona nini?

Mabula: Michael Shonza alirudisha bunduki lakini hata hivyo haikuwa imetumika.

Wakili: Baada ya kurudisha bunduki nini kilifuata?

Mabula: Mimi na Michael tulirudi majumbani kwetu kupumzika.

Wakili: Hili tukio la Sinza ambalo limetufikisha mahakamani hapa ulilifahamu lini?

Mabula: Nililisikia kwa aliyekuwa mshtakiwa wa nane ambaye ameachiliwa huru Felix, Januari 15 mwaka huo.
Aliniambia naitwa kwa Mkuu wa Kituo chetu, SSP Masinde na niliitikia wito na kwenda.

Wakili: Ulipofika Masinde alikuambia kitu gani?

Mabula: Akatuambia askari wote tuliokuwa kwenye doria jana yake tupande kwenye Pick Up; na kwenye hilo gari kulikuwa na askari wengine ambao niliwataja kwa majina awali pamoja na mimi isipokuwa James.

Wakili: Baada ya kupanda gari mlielekea wapi?

Mabula: Mi sikujua tunaelekea wapi ila tulipofika Ubungo niliwauliza askari wenzangu tunaenda wapi? Ndipo mshtakiwa wa sita Koplo Morris Nyangerela ambaye ameachiwa huru alisema Mkuu wa Kituo chetu ameagiza tupelekwe ofisini kwa kaimu RPC-Zombe.

Wakili: Uliwahi kuhoji kwa RPC mlikuwa mnaenda kufanya nini?

Mabula: Nilimuuliza Nyangerela akasema mkuu wa kituo anasema jana yake tulikuwa tumekamata majambazi.

Wakili: Mlipofika kwa RPC mkaambiwa nini?

Mabula: Nilikuta maofisa wa mkoa lakini niliyemtambua ni OCD wa Kinondoni, Maro.

Wakili: Wakati huo Kaimu RPC alikuwa Zombe alikuwepo ofisini mlivyoenda?

Mabula: Alikuwepo.

Wakili: Kilizungumzwa nini?

Mabula: Nilimsikia Zombe akituambia vijana mmefika njooni niwape mkono wa pongezi.

Wakili: Mbali ya kusema njooni niwape mkono wa pongezi alisema nini?

Mabula: Mbali na hilo sikumbuki alisema nini tena kwani nilikuwa na usingizi kwa vile jana yake nilikuwa nimekesha kwenye doria.

Wakili: Nini kilifuata?

Mabula: Tulitolewa nje na kurudishwa Kituo cha Chuo Kikuu.

Wakili: Hapo awali wakati umenza kutoa ushahidi ulidai kwamba Nyangerela alikwambia jana yake walikamata majambazi wanne , waliwakamatia eneo gani?

Mabula: Sinza.

Wakili: Nyangerela hakuwahi kuwaambia kama kulikuwa na mapambano ya silaha na watu hao?

Mabula: Hakuwahi kuniambia.

Wakili:Suala la mauji ya watu hawa ulianza kulijua lini?

Mabula:Nililijua kupitia Redio Free kwa sababu magazeti yalikuwa yakisomwa kwamba polisi wapambana na majambazi.

Wakili: Ni lini ulikuja kufahamu wewe unahusishwa na mauji haya?

Mabula: Mwishoni mwa Januari mwaka 2006, nikiwa katika mahakama ya Kawe nilipata ujumbe toka kwa Inspekta Omary kwamba natakiwa Makao Makuu ya Upelelezi.

Wakili: Je, ulitekeleza wito huo?

Mabula: Nilikwenda Makao Makuu ya upelelezi saa tano asubuhi na nilikutana na afande Omar mwenyewe akachukua maelezo yangu ya jinsi tulivyowakamata wale watu.

Wakili: Alikwambia nini?

Mabula: Aliniambia askari wote wa UDSM waliokuwa doria siku ya Jumamosi ya Januari 14 mwaka huo wameandika maelezo isipokuwa mimi.

Wakili: Nani aliandika maelezo yako?

Mabula: Inspekta Omar na nilimweleza mimi sitambui mauji ya watu hao.

Wakili: Baada ya kumwambia wewe hutambua mauji hayo, nini kiliendelea?

Mabula: Aliniambia kama sitambui , siku hiyo nilipangiwa wapi, nikamweleza Makongo Juu.

Wakili: Mahakama ilielezwa kwamba IGP-Said Mwema aliunda Tume chini ya ACP Mgawe, pia kulikuwa na tume ya Mkumbi na ya Jaji Kipenka, ulishawahi kuhojiwa katika tume hizo?

Mabula: Mi nafikiri maelezo niliyotoa kwa Inspekta Omar ndiyo tume ya Mgawe na tume hizo nyingine zote nilihojiwa na kutoa maelezo yangu.

Wakili: Katika tume hizo, waliokuhoji waliwahi kukuambia kwa nini wanataka kuandika maelezo yako?

Mabula: Waliniambia wanataka maelezo yangu wapeleke mahakamani.

Wakili: Unapafahamu msitu wa Pande, Bunju na Sinza Ukuta wa Posta?

Mabula: Kwa mara ya kwanza nimepafahamu wakati mahakama hii ilipotembelea huko. Na ninaomba mahakama hii inihukumu kutokana na ushahidi uliotolewa.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili wa Serikali Alexender Mzikila na Mabula;

Wakili: Ni kwa nini hukuhoji ulipopewa mkono wa pongezi?

Mabula: Sikuuliza kwani kijeshi askari mdogo ni mwiko kumhoji askari aliyekuzidi cheo kwa sababu unaweza kufukuzwa kazi na unapoambiwa jambo na mkubwa wako hakuna kusema hapana.

Wakili: Kwa nini ulishindwa kumuuliza ni kazi gani mlifanya hadi mpongezwe?

Mabula: Ni kosa la jinai kumhoji afande.

Wakili: Hebu angalia maelezo yako uliyoyaandikwa kwenye tume ya Mama Mkumbi, ni yako kweli?

Mabula:Mmh kuna baadhi ya maelezo ni yangu mengine siyo yangu.

Wakili: Vipi maelezo haya uliyoyaandika kwenye tume ya ACP Mgawe?

Wakili: Jaji mimi nilihojiwa na Inspekta Omar lakini leo naona maelezo haya yamesainiwa na SSP Mayala na hata saini hii siyo yangu.

Wakili: Ushahidi wako uliotoa leo unatofautiana na ushahidi ulioutoa kwenye tume hizo tatu?

Mabula: Ndiyo.

Wakili: Lakini kwa mujibu wa maelezo uliyoandika kwa inspekta Omar yanaonyesha wewe ulikuwa miongoni mwa askari walikuwepo kwenye eneo la mapambano na kwamba ulisikia milio ya risasi?

Mabula: Nimekwambia Omar alinihoji na Mkumbi alinihoji lakini hiyo statement nyingine ya Mkumbi imesainiwa na mtu mwingine ambaye hakunihoji kabisa na wala simfahamu.

Wakili: Kuna ushahidi ulitolewa wewe ulikamata washtakiwa na ulifika pande ambapo mauji yalifanyika, unasemaje?

Mabula: Sipajui Pande.

Ifuatayo ni mahojiano kati ya Mzee wa Baraza, Magreth Mossi na Mabula:

Wakili: Ni mara ya ngapi kupewa mkono wa pongezi na viongozi wako?

Mabula: Siku hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kupewa mkono wa pongezi.

Wakili: Wewe ukishangaa ni kwa nini?

Mabula: Hata mimi nilishangaa.

Hata hivyo mshtakiwa wa tisa, Shonza ushahidi wake umefanana na Mabula ambapo alimaliza kutoa ushahidi wake na Jaji Massati akaahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo upande wa serikali utaanza kumuuliza maswali.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano ,Februali 18 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.