Header Ads

MASIKINI ZOMBE

*Korti yasema ana kesi ya kujibu, kuanza kujitetea leo
*Kuleta mashahidi sita akiwemo ACP Masindoki
*Watatu waachiwa huru, hawaamini kilichowatokea

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imesema aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini, ana kesi ya kujibu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji wa Mahakama ya Rufaa nchini, Salum Masati, alipokuwa akitoa uamuzi kwa washitakiwa 13 katika kesi hiyo iwapo kama wana kesi ya kujibu au la.

Wakati Zombe na wenzake tisa katika kesi hiyo wana kesi ya kujibu, Jaji Masati aliwachia huru washtakiwa watatatu katika kesi hiyo ambao ni F.5912PC Noel Leonard, D.6440 Koplo Nyangelera Moris na E.6712 Koplo Felix Cedrick.

Alisema washitakiwa hao wameachiwa huru baada ya ushahidi wa upande wa mashitaka uliotolewa mahakamani hapo, kutowagusa.

“Pamoja na kuwaachia huru washitakiwa hawa, pia nimebaini washitakiwa hawa walishiriki kuwakamata marehemu, lakini hawakwenda msitu wa Pande ambapo tukio la mauji linadaiwa kutendeka na kielelezo cha 13, 16 na 22 kimedhibitisha hilo,” alisema Jaji Masati.

Jaji Masati ambaye alianza kutoa uamuzi huo saa 4:28 hadi saa 5:37 asubuhi katika chumba namba moja ambacho kilifurika watu, alisema baada ya kupitia kwa kina hoja za mawakili wa utetezi amebaini yafuatayo kwa kila mshitakiwa.

Kuhusu Zombe, Jaji alisema alikuwa anafuatilia tukio hilo na anafahamu mazingira yaliyosababisha mauaji hayo ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa kuonyesha kwamba alikuwa akipewa taarifa za mara kwa mara na askari wake.

“Lakini kufika kwake katika Kituo cha Polisi cha Urafiki baada ya mshitakiwa pili na watatu (Christopher Bageni na (ASP) Ahmed Makele na kuwaulizia fedha za marehemu, hiyo inaonyesha Zombe alikuwa na mawasiliano na washitakiwa wengine,” alisema Jaji Masati.

Alisema nafasi yake (Zombe) kama RCO na Kaimu RPC ilimuweka katika nafasi nzuri ya kujua nini kilikuwa kinaendelea na kutoa amri kuwa marehemu wakamatwe.

“Kitendo cha Zombe cha kuwaita maofisa wake waliowakamata marehemu na kuwapongeza ni dalili kwamba alikuwa akijua kilichotokea kwa marehemu,…kwa sababu hizo mahakama imeona ni vizuri Zombe akapewa nafasi ya kueleza mahakama kuhusu tukio hilo,” alisema Jaji Masati.

Jumanne iliyopita, Zombe alitamba kuwa mahakama hiyo itamwachia huru kwa kuwa hana kesi ya kujibu.

Kwa upande wa mshitakiwa namba mbili Bageni, Jaji alisema mahakama imeona ana kesi ya kujibu kwa sababu ushahidi ulidai kulikuwa na umuhimu wa kuwapo kwa mapambano ya risasi, hivyo anapaswa kutoa maelezo kwani yeye ndiye aliongoza kikosi cha kuwaua marehemu.

Kuhusu mshitakiwa 11 na 12 (D. 9321 DC Rashid Lema na D.4656D/Koplo Rajabu Bakari), Jaji alisema hafikirii itakuwaje washtakiwa hao kutokuwa na kesi ya kujibu ingawa maelezo ya washitakiwa hao hayaendani na kosa linalowakabili.

“Washtakiwa hawa wawili kwa mujibu wa maelezo waliyoyatoa kwa polisi na mlinzi wa amani, ingawa hayaendani na vipengele vyote vinavyohusiana na kosa linalowakabali, mahakama imebaini kuna vipengele vinawahusisha kuwepo msitu wa Pande na kubeba maiti za marehemu hao na ushahidi huo unaungwa mkono na shahidi wa 30, 31 na 36,” alisema Jaji Masati.

Kuhusu mshitakiwa wa tatu, alisema kuna baadhi ya mashahidi toka eneo la Sinza Palestina ambao waliieleza mahakama kwamba marehemu hao wanne walikamatwa wakiwa hai, lakini kesho yake Polisi ikasema watu hao walikamatwa wakiwa wamekufa, hivyo mahakama inataka mwanga zaidi katika hilo.

Hata hivyo, Jaji Masati alitupilia mbali hoja za mawakili wa utetezi ya kutaka washitakiwa waachiwe huru kwa sababu hakufanyika gwaride la utambuzi wa washitakiwa na kusema hakuwa na umuhimu wa kufanyika hivyo kwa sababu upelelezi ulifanywa na polisi wenyewe.

Baada ya kutoa uamuzi huo, Zombe alibadilika sura ingawa alijikaza akijikaza kiume, huku Jaji Masati akiamuru washitakiwa aliowaachia huru kutoka mahakamani.

Washitakiwa hao walioachiwa huru pamoja na jamaa zao waliokuwapo mahakamani hapo walionekana kububujikwa na machozi ya furaha, kukumbatiana, huku wakionekana kutoamini kilichowatokea mahakamani hapo.

Baada ya kuondoka washitakiwa hao, Jaji Masati alisema washitakiwa waliobaki wanaweza kukaa kimya, kujitetea wenyewe au kuwaita mashahidi, ndipo wakili wa Zombe, Jerome Msemwa alisimama na kudai Zombe yupo tayari kujitetea hata leo (jana) na kwamba mshitakiwa huyo atatoa ushahidi chini ya kiapo. Pia ataleta mashahidi sita.

Kwa upande wa wakili wa Bageni, Ishengoma alidai mteja wake atajitetea chini ya kiapo na kwamba ataleta mashahidi wa tatu. Mshitakiwa wa tatu, ataleta shahidi mmoja, mshitakiwa tano, Jane Andrew ataleta shahidi mmoja, mshitakiwa wa 10, ataleta shahidi mmoja, wa 11 hatakuwa na shahidi wakati mshitakiwa wa 12, ataleta shahidi mmoja.

Hata hivyo, Jaji Masati alikataa ombi la Zombe la kuataka kuanza kujitetea jana kwa madai kuwa Wakili Majura Magafu anayemtetea wa tatu, tano, saba na kumi, hakuwepo mahakamani hapo kwani angeweza kumuuliza maswali, hivyo kuahirisha kesi hadi leo ambapo Zombe ataanza kujitetea.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, washitakiwa tisa wakati wakipanda gari la Jeshi la Magereza kupelekwa gereza la Keko, Zombe aliwasisitiza waandishi wa habari kuwa kesho (leo) wafike mahakamani kujifunza ‘Sharia’ kwa sababu ushahidi wake utaweza kuwafunza wananchi na waandishi wa habari.

“Mahakama Kuu ni mahakama kubwa ambayo inatafsiri sheria, hivyo kesho (leo) mfike kwa wingi kujifunza sheria pale nitakapopanda kizimbani kutoa ushahidi wangu,” alisema Zombe na kusababisha umati wananchi ambao walikuwa wamefurika kwenye lango la mahakama hiyo kucheka.

Wakati huo huo, baada ya washitakiwa watatu kuachiwa huru mmoja wa hao, D 6440 Koplo Nyangelera Moris ambaye alikuja kulakiwa na mke wake, alitimua mbio mahakamani hapo na kwenda karibu na Hoteli ya Kempsink na kukodi teksi na kabla ya kupanda gari hilo, alisema amefurahishwa na uamuzi huo na ataendelea na kazi ya upolisi na kukabiliana na majambazi.

Mbali na Zombe, Bageni na Makele, washitakiwa wengine waliopatikana na kesi ya kujibu ni WP 4593 PC Jane Andrew, D1406 Koplo Emmanuel Mabula, D8289DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari, D.1317D/XP; Festus Gwabusabi na D9321 DC Rashid Lema ambaye afya yake ni mbaya na hakuwepo mahakamani jana

Washtakiwa hao wanadaiwa Januari 14, mwaka 2006 katika msitu wa Pande uliopo huko Mbezi Louis, nje ya Jiji la Dar es Salaam, waliwaua wafanyabiashara wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro, Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe na dereva teski Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Februari 10 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.