Header Ads

MAKELE:ZOMBE AMENIPONZA

*Amshangaa kumsingiza, adai hana ugomvi naye
*Akana kupambana na majambazi waliouawa

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA wa tatu katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, aliyekuwa Mkuu wa Polisi Kituo cha Urafiki, Mrakibu wa Polisi (SP), Ahmed Makele (45), amedai mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Abdallah Zombe, ndiye aliyembambikia kesi hiyo ya mauaji.
Sambamba na hilo, hali ilikuwa tofauti kwa Zombe ambaye jana tangu aingie mahakamani muda mwingi alionekana kuwa kimya, tofauti na siku za nyuma ambapo alikuwa akionekana mtu mwenye furaha na kuzungumza na watu.
Makele ambaye jana alikuwa akihojiwa na mawakili wa serikali na mawakili wa utetezi, alieleza hayo alipokuwa akijibu swali la wakili wa mshitakiwa wa kwanza, Jerome Msemwa, ambalo alimuuliza kama anakubaliana na maelezo ya Zombe aliyoyatoa kwenye Tume ya Jaji Kipenka Mussa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Zombe katika tume hiyo, Makele alikuwa ni miongoni mwa askari waliopambana na watu wanne walioshukiwa na polisi kuwa ni majambazi.
“Maelezo ya Zombe kwenye tume hiyo ni ya uongo na Zombe ndiye amenibambikia kesi hii. Na mtukufu jaji, huyu Zombe ameniletea mzigo mbaya mimi,” alidai Makele.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Msemwa na Makele:
Wakili: Zombe katika ushahidi wake alidai wewe ni miongoni mwa washitakiwa waliomwandikia barua DPP. Unasemaje kuhusu hilo?
Makele: Si kweli.
Wakili: Unafahamu kwamba ikibainika mahabusu akiandika barua bila kupitia kwa mkuu wa gereza adhabu yake ni kifungo cha miezi sita, faini au vyote kwa pamoja?
Makele: Nimekwambia sijawahi kuandika barua.
Wakili: Ukiwa gerezani hujawahi kukutwa na simu ya mkononi?
Makele: Sijawahi.
Wakili: Wakati upo gereza la Ukonga ulikuwa unaishi eneo gani na je, sehemu hiyo ilikuwa na mahali pa kuchaji simu?
Makele: Nilikuwa nakaa selo hakuna pakuchaji simu.
Wakili: Ukiwa gerezani hujawahi kukamatwa na simu yenye vocha yenye thamani ya sh 135,000?
Makele: Iwe na vocha, haina vocha sijawahi kukamatwa nayo.
Wakili: Kwenye simu hiyo hujawahi kuingiziwa vocha yenye thamani ya sh 200,000?
Makele: Sijawahi.
Wakili: Unamfahamu Andrew Nyiti?
Makele: Namfahamu.
Wakili: Unamfahamu vipi?
Makele: Nilikuwa shahidi katika kesi ya kughushi aliyoishitaki Kampuni ya Tanzania Afgem, katika mahakama hii na ilikuwa mbele ya Jaji Agustino Shangwa.
Wakili: Kwenye kesi hiyo wakili Hurbet Nyange ambaye ndiye wakili wa gazeti la Tanzania Daima alikuwepo?
Makele: Ndiyo.
Wakili: Maelezo ya Zombe aliyoyatoa kwenye Tume ya Kipenka unasemaje?
Makele: Maelezo yake ni ya uongo na yamesababisha Tume ya Kipenka kuniona mimi ni muuaji. Huyu Zombe ndiye kanibambikia kesi na amenibebesha mzigo mbaya. Amenishangaza sana anavyodai kwamba mimi nilikuwa miongoni mwa askari waliopambana na majambazi siku hiyo. (Watu wakaangua kicheko).
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili wa Serikali Mugaya Mutaki na Makele:
Wakili: Januari 16 mwaka 2006 ulipata taarifa saa ngapi za tukio la uporaji katika duka la BIDCO?
Makele: Saa 12 jioni ya siku hiyo.
Wakili: Co sign yako ilikuwa ni ngapi?
Makele: 158.
Wakili: Ijumaa wakati ukitoa ushahidi wako ulisema siku hiyo uliondoka Kituo cha Polisi Urafiki na askari wawili, ni kina nani hao?
Makele: Ni mshitakiwa wa 10, Koplo Abeneth na mshitakiwa wa tano, Jane Andrew.
Wakili: Gari ulilotumia kwenda nalo kwenye tukio lilikuwa ni mali ya Jeshi la Polisi?
Makele: Ilikuwa ni mali yangu.
Wakili: Ilikuwa na namba gani ya usajili?
Makele: Sikumbuki.
Wakili: Je, siku hiyo ulikuwa unakwenda kwenye tukio, ulikwenda na silaha yoyote?
Makele: Siku zote nilikuwa nabeba bastola.
Wakili: Hao askari uliowabeba walikuwa na silaha?
Makele: Ndiyo.
Wakili: Mlivyotoka Kituo cha Urafiki mlielekea wapi?
Makele: Tuliingia Barabara ya Morogoro kisha tukaingia Barabara ya Shekilango tukafika Shule ya Mugabe tukaingia kwenye barabara ya vumbi kuingia kushoto.
Wakili: Mlivyofika hapo kushoto mlienda wapi?
Makele: Tuliiipita mitaa miwili mbele kidogo tukakuta umati wa watu nikausogelea. Nikasimamishwa na askari aliyekuwa amevalia sare za polisi, Koplo Nyangerela, ambaye ameachiwa huru, akanieleza watu wanne wamekamatwa na akanieleza yeye anaendelea kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.
Wakili: Hao watuhumiwa walivyokamatwa walipakizwa kwenye gari gani?
Makele: Pick Up na wote walikuwa hai na niliwaelekeza askari hao wa Chuo Kikuu ambao ndio waliwakamatwa watuhumiwa hao wawapeleke kwenye kituo chao, kwani ndiyo kituo husika ambapo tukio limetokea.
Wakili: Katika tukio hilo kulikuwa na skari mwenye cheo cha juu kuliko wewe?
Makele: Sijui, kwani nilimuona Koplo Nyangerela, siku hiyo alikuwa na askari wengine walikuwa wamevalia nguo za kiraia.
Wakili: Na hii gari ya Pick Up iliyobeba watuhumiwa uliitambua ni ya wapi?
Makele: Ni ya Kituo cha Polisi Chuo Kikuu na niliitambua kwa sababu ina namba SU na mara kwa mara ilikuwa ikitumiwa na Mkuu wa Kituo cha Chuo Kikuu, Masinde.
Wakili: Mbali na watuhumiwa kupakiwa kwenye hilo gari, ulibahatika kuona vielelezo vingine?
Makele: Niliona begi ambalo askari mmoja wa Chuo Kikuu alikuwa akitaka kumkabidhi Jane Andrew, nikamkatalia.
Wakili: Wewe ulibaini begi hilo lilikuwa na nini ndani yake?
Makele: Sikuweza kubaini.
Wakili: Hukupewa fedha wewe wala bastola na askari wa Chuo Kikuu?
Makele: Sikukabidhiwa chochote.
Wakili: Hao watuhumiwa uliwashuhudia walikamatwa wakiwa hai, walikuwa wangapi?
Makele: Wanne.
Mawakili: Hao watuhumiwa kabla ya kukamatwa na polisi walikuwa na gari gani?
Makele: Gari aina ya Saloon lenye rangi ya light blue na niliikuta eneo la tukio pale Sinza Palestina.
Wakili: Askari walivyowabeba hao watuhumiwa kwenye gari la polisi, gari la watuhumiwa liliendeshwa na nani?
Makele: Koplo Nyangerela.
Wakili: Nani alikuwa akiendesha Pick Up ya Chuo Kikuu ambayo ilibeba watuhumiwa?
Makele: PC Noel ambaye naye ulimuachia huru wiki iliyopita.
Wakili: Wewe ulikwenda eneo la tukio na kushuhudia mapambano ya risasi?
Makele: Hapana sikwenda na sikuona mapambano ya risasi.
Wakili: Kwa hiyo unataka kuiambia mahakama hii kwamba uliwaona watuhumiwa walivyokamatwa waliondoka eneo la tukio wakiwa salama?
Makele: Ndiyo, waliondoka wakiwa salama.
Wakili: Naomba usome kwa sauti kielelezo D10 ambacho kimeishapokelewa na mahakama hii?
Makele: Haya ni maelezo ya Abdallah Zombe aliyoyatoa kwenye Tume ya Jaji Mussa ambayo anadai kwamba yeye alisikia tukio la mauaji kwenye redial call, Makele alisema alikuwa ni miongoni mwa askari waliopambana na majambazi na wakafanikiwa kukamata sh milioni tano na bastola.
Wakili: Je, hayo maelezo ya Zombe uliyoyasoma ni sahihi?
Makele: Mtukufu jaji hayo maelezo anayajua aliyeyaandika (Zombe).
Wakili: Kama unayakana maelezo hayo ya Zombe inamaana alikusingizia?
Makele: Sana tena, ndiyo maana nipo jela na sijui ni kwanini aliamua kuandika hivyo wakati mimi sina ugomvi naye.
Wakili: Wewe unakataa hayo maelezo ukuyasema kwenye redial call?
Makele: Ijumaa iliyopita wakati nikitoa ushahidi wangu nilisema habari za tukio la BIDCO nilizipata kupitia Control Room.
Wakili: Kituo cha Urafiki kipo kwenye wilaya gani ya kipolisi?
Makele: Magomeni?
Wakili: Kituo cha Chuo Kikuu kipo chini ya wilaya gani ya kipolisi?
Makele: Kinondoni.
Wakili: Eneo walilokamatiwa watuhumiwa lilikuwa wilaya gani?
Makele: Kinondoni.
Wakili: Katika ushahidi wako wa juzi ulisema vielelezo kama fedha na bastola vilipelekwa Urafiki, watuhumiwa kadiri ya maelezo yako ulisema walipelekwa Chuo Kikuu, sasa kwa nini hivyo vielelezo visingepelekwa Chuo Kikuu badala yake vikapelekwa Urafiki, hebu iweke wazi mahakama.
Makele: Sijui ni kwanini.
Wakili: Tukio la uporaji katika duka la BIDCO ulilishuhudia?
Makele: Hapana.
Wakili: Lile gari la watuhumiwa lililetwa siku hiyo ya Januari 14 mwaka 2006 Kituo cha Urafiki?
Makele: Hapana, lililetwa kesho yake.
Wakili: Nisaidie ni kwa nini tukio hili lilitokea wilaya ya kipolisi Kinondoni na kwa nini likaletwa wilaya ya kipolisi Magomeni?
Makele: Sijui na hata hivyo jalada la tukio hilo halikufunguliwa Kituo cha Urafiki.
Wakili: Je, mshitakiwa wa kwanza (Zombe) alifika Urafiki siku hiyo?
Makele: Ndiyo alifika saa mbili usiku.
Wakili: Mshitakiwa wa pili (Christopher Bageni) naye siku hiyo alifika kituoni na alifika kwa sababu gani?
Makele: Ndiyo alifika, kwani alifuata vielelezo na awali alikuwa akikataa kupokea vielelezo hivyo.
Wakili: Unafikiri ni kwanini Bageni alikuwa anakataa kupokea?
Makele: Kwa sababu OCD wake Maro, alimwambia fedha ni sh milioni 5, lakini OCD wa Magomeni, Isunto Mantage, alimwambia zipo sh milioni 2.7 na bastola.
Wakili: Uliweza kufahamu zile ndiyo zilikuwa fedha za tukio la Sinza?
Makele: Sikujua.
Wakili: Mwaka 2006 hujawahi kumiliki simu yenye namba 0744 302226?
Makele: Sijawahi kabisa.
Wakili: Unaifahamu hiyo namba?
Makele: Siifahamu.
Wakili: Soma hiki kielelezo kwa sauti ambacho ni statement yako uliyoitoa kwenye Tume ya ACP-Mgawe.
Makele: Inasomeka hivi, haya ni maelezo ya Ahmed Makele (mimi) kwamba Januari 14 mwaka huo, nilikuwa eneo la tukio na kusikia milio ya risasi eneo la Sinza ukuta wa Posta na kushuhudia miili ya watu wanne ikiwa imekufa.
Wakili: Nakuuliza hayo ni maelezo yako?
Makele: Si maelezo yangu kabisa. Kwanza maelezo hayo yaliandikwa Makao Makuu ya Upelelezi na mimi sijawahi kuandika maelezo hadi nafikishwa mahakamani.
(Watu wakaangua kicheko).
Wakili: Hebu angalia hii statement uliyoitoa kwenye Tume ya Sidyen Mkumbi, ni yako?
Makele: Eeh mtukufu jaji, haya si maelezo yangu kabisa, kwani maswali niliyoulizwa na Mkumbi humu hayamo.
Wakili: Na hiyo saini iliyowekwa mwisho wa hiyo Statement pia si yako?
Makele: Saini hii si yangu (watu wakaangua kicheko).
Wakili: Shahidi wa 36, Sidyen Mkumbi na ACP-Mgawe ambao ni maofisa wako wakubwa, una ugomvi nao?
Makele: Hapana.
Kesi inaendelea kusikilizwa leo ambapo mshitakiwa wa tano, Jane Andrew ataanza kutoa utetezi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Februari 17 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.