Header Ads

MAWAKILI WAHAHA KUMUOKOA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

MAWAKILI wanaomtetea Amatus Liyumba, Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), anayekabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kusababisha hasara ya sh bilioni 221, wamewasilisha ombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakitaka mteja wao aachiliwe huru.

Mbali na Liyumba, mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ambayo siku za hivi karibuni imevuta hisia za watu wengi, ni Meneja Mradi wa BoT, Deogratius Kweka. Washitakiwa wote wapo rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya sh bilioni 55 kila mmoja au hati za mali zisizohamishika zenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Mawakili hao waliwalisha maombi hayo mahakamani hapo juzi chini ya hati ya kiapo iliyosainiwa na wakili Profesa Gamaliel Mgongo Fimbo.

Kwa mujibu wa hati hiyo, mawakili hao wanapinga uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi, wa kuwafungulia mashitaka watuhumiwa hao kwa madai kuwa una dosari za kisheria.

Hati hiyo, inataka shitaka la tatu katika kesi ya jinai namba 27 ya mwaka huu linalosomeka kuwa washitakiwa wote waliisababishia serikali harasa ya sh bilioni 221 lifutwe, kwa madai kuwa haliweki wazi kisheria kosa lililofanywa na washitakiwa hao.

“Kwa sababu hiyo, shitaka hilo la tatu halijaandaliwa kisheria kama kifungu cha 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, inavyotaka…na kwa sababu hiyo tunataka uamuzi uliotolewa na DPP wa kuwashitaki wateja wetu ufutwe,” alidai Profesa Mgongo Fimbo.

Hata hivyo, Hakimu Hadija Msongo aliutaka upande wa serikali kujibu ombi hilo Machi 2 na upande wa utetezi ujibu kwa maandishi Machi 4 mwaka huu. Januari 27 washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na mashitaka matatu.

Mashitaka hayo ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma, kuidhinisha ujenzi wa minara pacha (Twin Towers) bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi ya BoT na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.Washitakiwa wote walikana shitaka.

Msongo alisema ili mshitakiwa apate dhamana, ni lazima atoe hati au fedha taslimu sh bilioni 55, kusalimisha hati ya kusafiria na kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi serikalini.

Februali 17 hakimu Msongo - kwa mshangao wa wengi - alimpatia dhamana mshitakiwa huyo baada ya kuwasilisha hati zenye thamani ya sh milioni 882, badala ya sh bilioni 55 na hati ya kusafiria iliyokuwa imekwisha muda wake.

Hata hivyo, juzi Msongo alilazimika kufuta dhamana ya Liyumba, baada ya kubaini mshitakiwa huyo aliidanganya mahakama kwa kudai kuwa hakuwa na hati mbili za kusafiria wakati anazo.

Pia mahakama ilibaini hati 10 zilizoletwa na wadhamani wake zilikuwa na upungufu wa kisheria. Alitoa amri ya kutaka hati hizo zipelekwe katika Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 10, mwaka huu, kwa ajili ya kusikiliza ombi hilo la mawakili wa Liyumba.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 26 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.