Header Ads

WATANZANIA,WAKATI WA KUIWAJIBISHA SERIKALI UMEFIKA

Na Happiness Katabazi

MOJA ya dhamira ya uwepo wa vyama vingi duniani kote ni kupanua wigo wa demokrasia, hasa kwa wananchi kuchagua viongozi na vyama wanavyovipenda lakini pia kuwawajibisha viongozi wanaokwenda kinyume cha ahadi walizoahidi wakati wakiomba kura za wananchi.

Serikali iliyopo madarakani inaweza kuwajibishwa na wananchi ambao kimsingi ndio waliotoa ridhaa kwa chama au viongozi fulani kuingia serikalini bila kujali itikadi za dini au siasa za wananchi husika.

Katika siasa suala la utekelezaji wa ahadi ni jambo muhimu sana na ndiyo mwelekeo wa serikali ijayo, hapa nchini mwaka 2005 katika uchaguzi mkuu serikali iliyo chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania.

Waratibu wa kampeni wa Rais Jakaya Kikwete walimpamba mgombea wao kwa picha zenye taswira mbalimbali huku wakidai kuwa ni mkombozi wa kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Ahadi hizo kwa kiasi kikubwa ndizo zilizofanikisha kuchaguliwa kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye hivi sasa anaonekana kuelemewa na ahadi zake za kuleta maisha bora.

Kwa binadamu mwenye utashi na lengo zuri la kuangalia mustakabali wake wa maisha ni vema akafanya tathmini wa kile alichoahidiwa na serikali wakati wa kampeni.

Leo ni miaka mitatu tangu serikali iingie madarakani, Watanzania tujiulize imefanikiwa kutufikisha pale tulipopataka pamoja na kutimiza ahadi zake?
Leo hii mwananchi wa kawaida kauli ya maisha bora ni sawa na kitendawili kilichokosa mteguaji kwa kuwa kila siku zinavyokwenda ndivyo ugumu wa maisha unavyozidi.
Maisha yanaendelea kuwa magumu kila kukicha kama leo ni njaa kesho ni ukosefu wa maji kesho kutwa ni mgao wa umeme, mtondogoo kupanda kwa bei ya mafuta, unga, mchele, nyama, sukari, maharage hata mchicha.
Kwa hali ilivyo hivi sasa kwa mwananchi wa kawaida hakuna siku inayompa faraja au tumaini hasa kutokana na kuzongwa na matatizo ambayo mengine yanatokana na viongozi kusimamia vibaya rasilimali za nchi na kuweka mbele maslahi binafsi.
Tumeona pia jinsi ambavyo ahadi ya kupatikana kwa ajira milioni moja ilivyotekelezwa. kujengwa kwa jengo la wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga Complex), kuongezeka kwa baa na nyumba za kulala wageni mitaani ndizo ajira mpya ambazo serikali ya CCM imewatengenezea Watanzania.
Hakuna taifa linaloweza kuendelea kwa kuwaelekeza vijana kuuza peremende, karanga au kuwa wahudumu kwenye baa na migahawa ambayo vipato haviwatoshi hata kupata milo mitatu kwa siku.
Tumeona pia jinsi ambavyo suala la uwezeshwaji wa wananchi kuwa wajasiriamali linatekelezwa. Mabilioni ya Kikwete tumeyasikia lakini hakuna mwananchi wa kawaida anayeweza kutoa ushuhuda kwamba fedha hizo zimemfikia na kumwezesha kuzalisha mali zaidi kwenye ufugaji, utengenezaji wa bidhaa za viwandani au kilimo.
Mwelekeo ni kujenga taifa la wachuuzi, wafanyabiashara wanaouza bidhaa duni na chafu kutoka China. Tanzania imegeuzwa jalala la bidhaa zisizo na viwango zinazochafua mazingira na kuhatarisha afya za wananchi kutoka kila pembe ya dunia.
Ukweli ni kwamba hatuoni kasi ya ujengaji wa viwanda vipya zaidi ya kuona vile vilivyojengwa enzi za uongozi wa Baba wa Taifa hayati Julius Nyerere. Hatuoni mashamba mapya yakilimwa kwenye mfumo wa umwagiliaji na hata yale mashamba aliyotuachia Nyerere yanayotumia umwagiliaji, ama tumeyauza au hatuyaendelezi.
Tumeshindwa sasa kuwa na Shirika la Ndege kwa ajili ya kutoa huduma bora za usafirishaji, hatuna shirika la meli, reli nayo tumebinafsisha kwa wawekezaji wasio na mtaji wa kutosha kuiendeleza na tumejikuta tukimpa kodi zetu aiendeleze.
Hatukuwa makini katika kumchagua mwekezaji hasa kwa kutokuangalia historia yake na nchi anayotokea kama ina teknolojia ya kisasa ya reli, serikali imeshindwa kudhibiti madini yanayochimbwa na kampuni ya kigeni .
Serikali imeshindwa kuwabana kisheria wawekezaji wanaochimba kupora madini yetu ambayo hayatunufaishi kiasi cha kutosha badala yake huwaneemesha wawekezaji na nchi zao.
Tabia ya kuunda Tume ya Kuchunguza Mikataba ya Madini, hatujaona manufaa yake.Vivyo hivyo serikali hii imeshindwa kulipatia taifa nishati ya kuaminika licha ya kuingia mkataba na IPTL, na baadaye kuikodisha menejimenti ya Netgroup Solution kuliongoza Shirika la Tanesco na hata kampuni ya kufua umeme wa dharula ya Richmond nayo ilishindwa kutatua tatizo.
Watanzania tupo pale pale hatujapiga hatua bali tuna matapeli lukuki kwenye sekta hii ya Nishati na kero ya kukatikiwa umeme ipo pale pale.Tunalipa umeme ghali kuliko nchi zote za Afrika Mashariki na Kati na bado tupo gizani.
Kana kwamba hayo hayatoshi serikali yetu sasa imeharibu kabisa sekta ya elimu, iliahidi kuwa hakuna mtoto wa maskini atakayefukuzwa chuo kwa kukosa karo.Tujiulize sasa hawa watoto waliofukuzwa vyuo vikuu hivi karibuni ni Banyamulenge au Wazambia? Je, si Watanzania hawa?
Mbona Rais Kikwete mwenyewe ndiye aliyewaahidi katika mkutano wake na wanachuo hao pale Dimond Jubilee au serikali imegeuka haiongozwi tena Rais Kikwete?
Sisi tunachokiona ni kwamba serikali imeshindwa kuwa na kipaumbele katika utendaji wake badala ya kutambua umaskini wa wananchi na shida tulizonazo, wenzetu wamo kwenye bahari ya anasa.
Wananunua magari mapya na wameshabadilisha magari ya Ikulu.
Hivi ni maskini gani anabadilisha magari kila mwaka? Wamejipangia marupurupu ya kutisha kwa kila afisa anayesafiri nchi za nje analipwa zaidi ya dola 400 kwa siku bila kujali anakwenda hata Burundi.
Hivi hili ni taifa maskini kweli? Au tunadanganyana.Viongozi wakiugua wanapelekwa ng’ambo kutibiwa. Je, sisi wa kawaida tupelekwe wapi?
Nihitimishe kwa kusema kuwa ni wakati muafaka kwa kila mpiga kura kujiuliza kama alichokifanya katika uchaguzi mkuu mwaka 2005 ndicho atakachokifanya pia katika uchaguzi mkuu wa mwakani?
Kama sivyo tuanze leo katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na Vitongoji ili mwakani pawe na mageuzi ya kweli. Tanzania tusipoondoka kwenye ubabaishaji tukaingia kwenye mageuzi ya kweli, tutaishia kuzuia Shirikisho la Afrika Mashariki kwa kuwa wenzetu wanatuzidi kimaendeleo na sisi tunarudi nyuma kila mwaka.
Uoga wa kumezwa kwenye shirikisho na kugeuzwa wapagazi na vibarua, hautoisha kwa kuwa serikali yetu yenyewe imetutelekeza kama watoto wasio na mama wala baba.

Mungu Ibariki Afrika,Mungu Ibariki Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Februari 11 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.