Header Ads


Na Happiness Katabazi

UPANDE wa serikali katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.1 wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu(BoT)umesema unatarajia kuleta mashahidi 23 katika kesi hiyo pindi itakapoanza kusikilizwa.

Wakili Kiongozi wa Serikali Boniface Stanslaus, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,Waliyawande Lema,wakati akiwasomewa maelezo ya awali washtakiwa watano katika kesi hiyo ambapo alidai mashahidi wote watatumia anwani ya Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai(DCI).

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Bahati Mahenge,Manase Makale,Davis Kamungu,Godfrey Mosha na Eda Makale.

Wakili Stanslaus alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka tisa likiwemo kosa wizi,kula njama, kujipatia ingizo kwenye akaunti yao,kughushi ,kuwasilisha nyaraka za uongo.

Akisoma maelezo hayo, wakili huyo alidai washtakiwa wote ni wakazi wa jijini na kwamba mshitakiwa 2 na 5 ni wanandoa na kwamba Desemba 23 na Oktoba 26 mwaka 2005 wote walifanya makubaliano ya kuibia Benki Kuu ya Tanzania.

Alidai ilikukamilisha lengo hilo mshitakiwa wa kwanza Mahenge,alisaini Memorandum Form namba moja enye namba 14 na 15 kwajina la Samson Mapunda ,jina ambalo ni la kufikirika.

Na aliweka katika fomu hizo taarifa za uongo kuhusu anwani ya makazi,eneo la kampuni na taarifa hizo kampuni ya Changanyikeni Residential Complex ilisajiliwa na BRELA na kwa namba 47792.

“Vile vile mshitakiwa wa kwanza alisaini kadi ya benki ya CRDB pamoja General Terms of Condition poamoja na fomu ya kufungulia akaunti kwa jina la kufikirika la Samson Mapunda” alidai Boniface.

Aliendelea kudai washtakiwa hao walifungua akaunti CRDB Tawi la Kijitonyama na Agosti 31 mwaka 2005, Mahenge alisaini fomu nyingine kwa jina hilo la kufikirika na fomu hiyo ilionyesha kufanyika makubalino kati ya kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan na Changanyikeni Residential Complex na katika makubaliano alidai kwamba Changanyikeni imepewa kibali cha kukusanya deni la kampuni ya Marubeni.

Aidha alidai Oktoba 26 mwaka 2005 akaunti ya Changanyikeni iliingiziwa sh 1,186,534,303.27 na baadaye fedha hizo zilianza kuchukuliwa ama kwa keshi au hundi.

Wakili Stanslaus kwa njia ya onyo, Mahenge alikubali kuhusika katika uhalifu na aliwataja wenzake ambao ni washtakiwa katika kesi hiyo.

Na wakili huyo aliomba mahakama imruhusu awasilishe hati hiyo ya onyo mahakamani hapo kama upande wa utetezi utamruhusu.

Wakili wa utetezi, Gabriel Mnyere alipinga ombi hilo la upande wa mashtaka kuwasilisha hati hiyo ya onyo,kuwasilishwa mahakamani hapo kwasababu upande wa mashtaka ulipaswa kuwapatia mapame hati hiyo mawakili wa utetezi waipitie ndiyo ikabidhiwe mahakama.

Hata hivyo wakili Stanslaus aliinuka na kudai kwamba nachotakiwa wakili wa utetezi ni kupinga au kutopinga ombi lake na siyo kutoa maelezo mengine.

Hakimu Lema aliairisha kesi hiyo hadi Machi 12 mwaka huu, ambapo itakuja kwaajili ya kupangiwa tarehe.




Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Februali 21 mwaka 20009.

No comments:

Powered by Blogger.