Header Ads

MSHTAKIWA KESI YA ZOMBE YU HOI

* Ashindwa kufika mahakamani kujitetea
* Kesi yasitishwa kumpa nafasi apone
* Ni yule mwenye ushahidi muhimu
* Watu wafurika kusikiliza ushahidi wake

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ililazimika kusitisha usikilizaji wa kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja kutokana na mshtakiwa wa 11, Rashid Lema, kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi wake, kwa sababu ya afya yake kuwa mbaya.


Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Massati, alisitisha usikilizaji wa kesi hiyo ambayo kwa mujibu wa ratiba ya vikao kesi za mauaji iliyotolewa na kesi hiyo ilikuwa umalizike leo.

Jaji Massati wakati akiahirisha kesi hiyo, alisema anakubaliana na hoja za wakili wa mshtakiwa wa 11 na 12 (Rashid Lema na Rajabu Bakari), Denis Msafiri na kusema kwamba hoja zake ni nzito.

Alisema kwa sababu kikao hicho kinakwisha (kesho) leo na kwa mujibu wa ratiba hakiwezi kuendelea hadi kibali cha Jaji Mkuu, alisema utetezi wa washtakiwa waliosalia utasikilizwa katika kikao kingine.

“Tutaendelea na utetezi hadi kikao cha kesi hii kitakapopangwa na Msajili wa Mahakama na pia naagiza upande wa utetezi upewe mwendo wa kesi hii,” alisema Jaji Massati.

Awali, wakili wa mshtakiwa 11 na 12, ambapo jana Lema alikuwa atarajiwa kuanza kutoa ushahidi wake ambao ulikuwa unasubiriwa kwa shauku na umati wa watu, aliomba mahakama iahirishe kesi hiyo, kwani juzi alienda gerezani kumuona Lema na kuona afya yake haimruhuu kufika mahakamani kutoa ushahidi.

“Mtukufu Jaji kama nilivyoomba juzi kwenda kumuona Lema gerezani, nilikwenda nikaongea naye, hawezi kutoa ushahidi leo (jana) wala kesho, kwani hali yake kiafya hamruhusu. Naomba kesi hii iarishwe,”alidai wakili Msafiri.

Jaji Massati alipomuuliza ni kwa nini mshtakia wa 12, asiendelee jana kutoa ushahidi wake, wakili huyo alidai ni muhimu Lema atoe ushahidi wake kwanza ambao utatoka kwenye kinywa chake ndipo mshtakiwa wa 12 afuate kutoa ushahidi.

Aidha, Jaji Massati alipomuuliza wakili wa mshitakiwa 13, (Festus Gwabusabi), Myovela ni kwanini mshitakiwa wake asijitete, alidai hawakuwa wamejiandaa kutoa ushahidi kwa kuwa kuna baadhi ya nyaraka ambazo wangezitumia wakati mshitakiwa huyo akijitetea bado hawajazipata.

Kwa upande wake, wakili wa Mshitakiwa wa kwanza, Jerome Msemwa, alieleza kuunga mkono hoja zilizotolewa na mawakili wenzake kuwa shauri hilo liahirishwe.

Tanzania Daima ambalo lilifika mahakamani hapo saa 1:02 asubuhi, ilishuhudia umati mkubwa wa watu uliokuwa umekaa kwenye viwanja vya mahakama ukisubiri kusikiliza kesi hiyo.

“Tumefika hapa tangu saa 12 asubuhi tunasubiri mahakama ifunguliwe, ili tuwahi viti kumsikiliza Lema ambaye inadaiwa ndiye mshtakiwa aliyepania kutoa siri ya mauaji hayo,” alisema Jakson John ambaye ni mkazi wa Kimara.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Februari 3 mwaka huu ambapo mawakili wa utetezi waliwasilisha hoja za kwamba wateja wao hawana kesi ya kujibu na upande wa serikali kujibu hoja hizo.

Februali 9 mwaka huu, Jaji Massati alitoa uamuzi kuhusu hoja hizo na kuwaachiwa huru washtakiwa watatu ambao ni Noel Leonard, Koplo Moris Nyangerela na Koplo Felix Sandys Cedrick kwa maelezo kuwa ushahidi uliotolewa umeshindwa kuthibitisha kwamba wana kesi ya kujibu.

Mbali na Lema na Bakari, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe, SP Christopher Bageni, SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, na Festus Gwasabi, ambao wanadaiwa Januari 14 mwaka 2006, huko Mbezi Luisi Msitu Pande, waliwauwa Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge na Juma Ndugu ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 20 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.