Header Ads

LIYUMBA BADO ASAKWA

*Yadaiwa amejificha Dar kukamilisha dhamana
*Wadhamini wake wafutiwa amri ya kukamatwa

Na Happiness Katabazi

VYOMBO vya ulinzi na usalama nchini bado vinaendelea kumsaka mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kusabisha hasara ya sh bilioni 221, inayomkabili Amatus Liyumba, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT).


Mbali na Liyumba, mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Meneja Mradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka, ambaye hadi sasa bado anasota rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Hatua hiyo ya vyombo vya ulinzi kuendelea kumsaka Liyumba, inatokana na juhudi za vyombo hivyo juzi na jana kushindwa kumkamata na kumfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Jumatano wiki hii ilitoa hati ya dharura ya kukamatwa kwa mshitakiwa huyo na wadhamini wake wawili.

Wakili wa serikali, Mwangamilia, aliyekuwa akisaidiana na Tabu Mzee kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), alidai mahakamani hapo jana kuwa bado hawajafanikiwa kumkamata Liyumba kama walivyoamriwa na mahakama hiyo.

Kwa upande wake, wakili wa mshitakiwa wa kwanza, Majura Magafu, aliyejiunga rasmi jana kumtetea mshitakiwa huyo akisaidiana na wakili Hudson Ndusyepo, aliiambia mahakama kuwa mteja wake hajafika mahakamani, lakini wadhamini wake - Otto Agatoni na Benjamin Ngulugunu - wamefika mahakamani hapo.

Akitoa uamuzi wake jana saa 8:52 alasiri, hakimu Hadija Msongo alisema ameshapokea jalada halisi la kesi hiyo kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, na kwamba amefuta hati ya kukamatwa kwa wadhamini hao isipokuwa hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa huyo bado inaendelea.

Msongo alisema kesi hiyo itatajwa Februari 24 kama ilivyopangwa awali na kwamba wadhamini hao wanatakiwa kufika siku hiyo.

Baada ya kutoa uamuzi huo, Magafu alisimama na kuanza kuulalamikia upande wa mashitaka kwamba umeanza kuinyanyasa familia ya Liyumba na kuiomba mahakama ikemee suala hilo.

Alikuwa anaomba gari la mdhamini wa mshitakiwa huyo lenye namba za usajili T329 AWY Toyota Chaser linaloshikiliwa, liachiliwe.

Hata hivyo, Msongo alimtaka Magafu aache kuwasilisha maombi yake kwani jana haikuwa tarehe ya kesi hiyo.

“Magafu, nimeshasema leo si tarehe ya kesi hii…kama una malalamiko yoyote yawasilishe siku ya tarehe ya kesi,” alisema Msongo na kuahirisha kesi hiyo.

Lakini habari Tanzania Daima iliyozipata jana kutoka vyanzo vya habari vya kuaminika, zinadai kuwa Liyumba hajatoroka, bali yupo nchini amejificha na anachokifanya ni kuhakikisha anakamilisha masharti ya dhamana ili Jumanne atakapofika mahakamani aweze kutimiza masharti hayo.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, taratibu zilizotumika kumpatia dhamana zitafutwa na atatakiwa aanze upya, hali itakayosababisha kurudishwa tena rumande.

Juzi uvumi ulizagaa Dar es Salaam kuwa Liyumba ametoroka. Kutokana na uvumi huo mahakama ilitoa hati ya kukamatwa kutokana na mazingira ya utata wa dhamana yake, kwani alidhaminiwa kwa hati ya mali ya sh milioni 882 badala ya mali zenye thamani ya sh bilioni 55.

Kabla ya kupewa dhamana, Liyumba alikwenda Mahakama Kuu kuomba alegezewe masharti ya dhamana hiyo iliyomtaka atimize masharti ya hati za mali au fedha taslimu sh bilioni 55, wadhamini wawili, kuwasilisha hati ya kusafiria, kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama na kila Ijumaa kuripoti katika Ofisi ya Takukuru.

Hata hivyo, Mahakama Kuu Ijumaa iliyopita, chini ya Jaji Projestus Lugazia, ilitupilia mbali ombi hilo, kwa madai kuwa haoni sababu za kutengua masharti ya dhamana ya Kisutu.

Baada ya maombi hayo kutupwa, Liyumba Jumatatu wiki hii aliwasilisha hati za dhamana zenye thamani ya sh bilioni 55, ambazo, hata hivyo, zilipangwa na mawakili wa serikali kwa madai kuwa zilikuwa na kasoro.

Liyumba na Kweka wanakabiliwa na matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuidhinisha ujenzi wa minara pacha ya BoT, maarufu kama ‘Twin Tower’ na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Februali 21 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.