Header Ads

JAJI RAMADHANI:UHURU WA MAHAKAMA UHESHIMIWE

Na Happiness Katabazi

“NAKUMBUKA Rais Jakaya Kikwete, mwaka jana ulituahidi kuiwezesha Mahakama. Lakini nakumbuka pia jeshini niliambiwa mjue kamanda wako. Nami nathubutu kusema kuwa ninamjua kamanda wangu, hana kauli mbili, alisemalo atalitenda tu ni suala la muda. Hivyo siombi kama mwaka jana kuwa utuwezeshe, bali naomba muda usiwe mrefu.”

Kauli hiyo nzito ilitolewa Ijumaa iliyopita na Jaji Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhani, katika viwanja vya Mahakama Kuu, Barabara ya Kivukoni Front, Dar es Salaam, ambako sherehe hizo ziliashiria mwanzo rasmi wa kazi za Mahakama kwa mwaka huu.

Baadhi ya watu waliohudhuria walijikuta wakivunjwa mbavu na kauli ya Jaji Mkuu, huku wengine wakisikika wakisema: “Leo mwanasiasa (Rais Kikwete) amepatikana kwa mwanasheria Ramadhani.”


Binafsi nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari za mahakamani tulioalikwa kuhudhuria sherehe hizo, hakuna ubishi kwamba sherehe za mwaka huu zilifana, ukilinganisha na za mwaka uliopita.


Moja ya mambo yaliyochagiza sherehe hizo ni matumizi ya lugha ya Kiswahili, ambayo ilitumika kwenye hotuba zote tatu zilizotolewa na Jaji Mkuu, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Dk. Fauz Twalib na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, iliyosomwa kwa niaba yake na naibu wake.


Matumizi ya lugha hiyo yalitoa nafasi kwa wananchi walioalikwa na waliokuwa wakipita njia kuelewa kile kilichokuwa kikizunguzwa, tofauti na sherehe zilizopita, ambapo ilitumika lugha ya Kiingereza, ambayo bado idadi kubwa ya Watanzania hawaielewi ipasavyo.


Siku ya Sheria huadhimishwa Februari 2, kila mwaka, lakini kwa mwaka huu imeadhimishwa Februari 6, ili kumpa nafasi Rais Jakaya Kikwete kuhudhuria kutokana na tarehe husika kuwa nje ya nchi kwa majukumu ya kikazi.


Hotuba ya Jaji Mkuu Ramadhani iliwagusa wengi kutokana na kuongea ukweli, kiasi cha kumfanya Rais Jakaya Kikwete kuamua kujibu baadhi ya mambo, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu maalumu uliowekwa na Mahakama wa kutomruhusu mgeni rasmi katika sherehe za kitaaluma kuhutubia.


Uamuzi huo wa Rais Kikwete ulipokewa kwa shangwe na umati wa wananchi uliofurika katika viwanja hivyo, ambao walibainisha kuwa uamuzi huo ni ishara kwamba ameguswa na hotuba ya Jaji Mkuu.


Jaji Mkuu anasema ibara ya 107A ya Katiba ya nchi inatamka wazi kuwa mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano ni mahakama na ibara ya 107B inasema mahakama zote zitakuwa huru katika utendaji wake na kuongeza kuwa ibara hiyo ndiyo chimbuko la uhuru wa Mahakama nchini.


Anasema mahakama inatakiwa iwe huru na mamlaka ya utendaji (executive). Uhuru huu wa mahakama kama papa baharini ndio unaovuma sana na pengine unakera pia.


Aliweka wazi kuwa ni vigumu kuelewa vipi rais amteue mtu kuwa jaji halafu asiweze kumdhibiti kama amdhibitivyo waziri, lakini Katiba imetamka hivyo.


Si hivyo tu, lakini ili kutenda haki kikamilifu, uhuru wa mahakama ni muhimu uwepo.
“Mahakama inapaswa iwe huru na umma au sehemu za umma, hitaji hilo nalo pia ni muhimu sana, wananchi wanaweza kuamini kuwa mshtakiwa ni mhalifu kumbe mahakama imemuona ana hatia.


Sasa mahakama isishinikizwe kumtia hatiani mtu ambaye hana hatia, uhuru ni muhimu sana katika nyakati kama hizi za tuhuma zilizokithiri za ufisadi, ambapo baadhi ya wananchi tayari wamekwisha kuwatia hatiani baadhi ya watuhumiwa hata kabla ya kufikishwa mahakamani,” alisema Jaji Ramadhani.


Anasema kuna uhuru wa kila jaji au hakimu binafsi, hupatikana kwa kumthibitishia uhakika wa ajira yake. Jaji au hakimu ambaye ana wasiwasi na ajira yake.


Anasema hivi sasa limezuka tishio dhidi ya uhuru wa mahakama kutoka mhimili wa nne wa dola (vyombo vya habari), alibainisha kuwa havitofautishi kati ya ukweli (facts) na maoni.


Baadhi ya vyombo huandika maoni kana kwamba ndiyo ukweli wenyewe, hali hiyo hupotosha wananchi na athari iletwayo haitibiki hata kwa shubiri.


Kwa mfano, mgomo wa walimu ulipigwa marufuku na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Uamuzi huo ulifikishwa Mahakama ya Rufaa ambayo iliona kuwa suala halikuwa limewasilishwa kihalali mbele ya Mahakama Kuu.


Hivyo shughuli yote mbele ya Mahakama Kuu ilifutwa.


Anasema magazeti mengi yaliandika vichwa vya habari kuwa Mahakama ya Rufaa imebariki mgomo, wakati mahakama hiyo haikuamua hivyo na alimuagiza Msajili wa Mahakama ya Rufaa kutoa maelezo sahihi kwenye vyombo vya habari.


Jaji Mkuu, ambaye ni brigedia jenerali mstaafu, anaeleza kuwa umejengeka mtazamo usio sahihi ambao unapotosha dhana halisi na sahihi ya uhuru wa mahakama.


Badala ya uhuru wa mahakama kueleweka kwa maana iliyokusudiwa, baadhi yao majaji, mahakimu na viongozi wengine wa serikali wametafsiri uhuru wa mahakama kuwa ni utengano wa watendaji wa mahakama na viongozi wa serikali.


Matatizo ya miundombinu ya mahakama hayajadiliwi na kusaidiwa kutatuliwa na kamati za ushauri za mikoa na wilaya katika maeneo yao kwa kinachodaiwa kuwa kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama.


Sababu hiyo inayafanya majengo ya mahakama za mwanzo mengi kuwa na hali mbaya na sehemu nyingine hakuna kabisa majengo, lakini shule, zahanati na hata vituo vya polisi hujengwa na kamati hizo au kutokana na uhamasishaji wa kamati hizo.


Uhuru wa mahakama hauna maana kuwa majaji na mahakimu wasichangamane na viongozi wengine au wananchi, na ni muhimu mahakama iwe na mahusiano mazuri na mihimili miwili mingine ya dola ili kuifanya kazi yake kuwa rahisi.


Akizungumzia uzingatiaji wa dhana ya mgawanyo wa madaraka katika utekelezaji wa shughuli za serikali nchini, alimpongeza Rais Kikwete kwamba katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, hajaingilia Mahakama kwa matendo na hata kwa kauli.Waliomtangulia waliwahi kuteleza na kuvunja mwiko huo.


Aidha, anasema mahakama imekuwa na matatizo na ngazi nyingine za serikali kwani baadhi ya hukumu za mahakama zimedharauliwa na kutotekelezwa na kutolea mfano katika kesi ya Devram P. Vallambhia V. Transport Equipment ambayo uamuzi ulitolewa muda mrefu lakini kwa miaka mingi utekelezwaji ukawa unazungushwa hadi mshinda tuzo, yaani aliyehukumiwa haki, akafariki dunia.


Anasema kwa bahati mbaya, Spika wa Bunge mara moja tu alighafirika na akatoa matamshi kuhusu sakata la mafuta ya petroli huko Morogoro, pale amri ya EWURA ya kuvifunga vituo kadhaa vya mafuta ilipositishwa kwa muda na Mahakama ya Hakimu Mkazi, na kusema kauli hiyo ingetolewa ndani na wala si nje ya Bunge, ingekuwa stahili yake.


Akitolea mfano wa kesi ya mfanyabiashara maarufu Tanzania, Reginald Mengi na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, Jaji Ramadhani alisema Bunge lilichukua kazi ya mahakama na kusikiliza tatizo kati ya wawili hao wakati mmoja hakuwa mbunge.


“Kwa upande mwingine, Bunge liliwahi kutaka liwe na madaraka ya kimahakama dhidi ya watu wanaozozana na waheshimiwa wabunge. Kwa bahati nzuri wazo hilo halikufanikiwa, lakini bado Bunge lilichukua kazi ya mahakama na kusikiliza tatizo hilo kati ya Malima na Mengi ambaye si mbunge, anasema Jaji Ramadhani.


Hata hivyo anasema kwa upande mwingine Bunge liliwahi kutaka liwe na madaraka ya kimahakama dhidi ya watu ambao wanazozana na wabunge lakini kwa bahati nzuri wazo hilo halikufanikiwa.


Anasema mahakama nchini zinahitaji kubadilika ili kutafuta njia za kuleta mkabala murua na mihimili miwili mingine ya dola kwa lengo la kupanua wigo wa demokrasia pamoja na haki za kila mtu.


Hata hivyo alitoa rai kwa Rais Kikwete kuwa huenda ikafaa kama viongozi wa hiyo miwili mitatu watakuwa na utaratibu wa kukutana pamoja faragha ili kuzungumzia mambo wanayokinzana na huenda ikasaidia kuzuia mitafaruku.


Ziara za Tume ya Utumishi ya Mahakama mikoani, anasema kuanzia mwaka jana tume hiyo imefanya ziara mikoani na kutembelea mikoa ya Iringa, Dodoma na Morogoro,
Kilimanjaro, Arusha, na walieleza maana sahihi ya uhuru wa mahakama na kuna mafanikio makubwa yamepatikana na wataendelea kuzuru mikoa mingine.


Kuhusu hali ya mahakama tangu mwaka jana, anasema mbali na shughuli za kawaida kusikiliza kesi na rufaa, mahakama kwa kipindi cha mwaka mmoja imepiga hatua za kuridhisha, imeingia maelewano na Investment Climate Facility for Africa (ICF) ambao wamewapa dola milioni mbili kwa ajili ya kuendeleza teknolojia ya kisasa.


Anasema tayari majaji wote wa Rufaa na wa Mahakama Kuu wa Dar es Salaam wapatao 31 wamepata mafunzo ya kompyuta kwa majuma mawili huko ESAMI, Arusha na watapatiwa kompyuta ndogo (Laptops) chini ya msaada huo huo.


“Tumekarabati mahakama za mwanzo nne kwa msaada wa Programu ya Kuboresha Sekta ya Sheria (LSRP).


Serikali imekamilisha ujenzi wa mahakama za mwanzo sita na kukarabati mbili.
Wananchi wamechangia nguvu zao na serikali imekamilisha nguvu hizo katika Mahakam za Mwanzo tisa. Haya ni maendeleo,” anasema Jaji Ramadhani.


Anasema hayo ni baadhi ya mafanikio lakini bado mahakama inakabiliwa na matatizo mengi mno, baadhi yao ni ufinyu wa bajeti, mwaka wa fedha wa 2007/8 walipewa sh bilioni 25.06, mwaka 2008/9 walipewa sh bilioni 21.08 na kwa mwaka 2009/10 wamepewa kiwango cha juu cha sh bilioni 20.03 ambacho alisema kiasi wanachopewa kinazidi kupungua wakati gharama zinapanda.


Aliongeza kuwa kiwango hicho cha mwaka 2009/10 Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu zitaweza kila moja kuwa na vikao vinane tu vya kusikiliza mashauri kwa mwaka huo wa fedha na kuongeza kuwa endapo kiwango hicho hakitaongezwa, juhudi zote wanazofanya za kuharakisha usikilizaji wa kesi zitavia.


Aidha, anasema tatizo jingine ni uhaba wa mahakama za mwanzo, jumla ya mahakimu 1,102 wanahitajika katika mahakama za mwanzo nchi nzima, lakini hivi sasa wapo 602 tu na hivyo kuna upungufu wa mahakimu 500.
Anasema wamepata kibali mwaka huu waajiri mahakimu 100 na wapo katika mchakato wa kuwapata.
Baada ya kusema matatizo hayo matatu alisema: “Rais wewe ndiye tegemeo letu mahakamani. Spika Samuel Sitta naye anayo matatizo yake, lakini hali yake si mbaya kama yetu. Mawaziri wote ni wabunge. Hivyo masilahi ya wabunge yakiwa bora, basi na masilahi ya mawaziri yanakuwa bora pia.
“Lakini mahakamani tupo kama watoto yatima, hatuna ubia na masilahi na mhimili wowote,” alisema kwa masikitiko.
Rais Kikwete alikiri kuwa hotuba ya Jaji Ramadhani imemgusa na kuahidi kuongeza bajeti ya Mahakama katika mwaka ujao wa fedha ili kuiwezesha sekta ya sheria angalau kufanya kazi kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Rais Kikwete ambaye kwa mujibu wa taratibu hakupaswa kuzungumza katika sherehe hizo, alilazimka kuomba azungumzie baadhi ya mambo ambayo yalisemwa na Jaji Mkuu.
Rais Kikwete alikiri hadharani kwamba hotuba ya Jaji Ramadhani imemgusa na kuahidi kuongeza bajeti ya Mahakama katika mwaka ujao wa fedha.

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Jumatano,Februali 11 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.