Header Ads

ALIYEMPIGA MWINYI AFUNGWA MWAKA MMOJA

*Asema adhabu aliyopewa ni sahihi

Na Happiness Katabazi

KIJANA Ibrahimu Said Sultani ‘Ustaadhi’ (26), aliyempiga kofi Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Neema Chusi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, baada ya mshitakiwa huyo juzi kukiri kutenda kosa hilo.

Alipopewa nafasi ya kujitetea kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Sultani alisema kuwa, anaamini hukumu atakayopewa ni sahihi na itakuwa inatokana na mapenzi ya Mungu.

“Hakimu nashukuru kwa kunipa nafasi hii, mimi nakiri kwamba nimetenda kosa na ninaamini hukumu nitakayopewa na mahakama hii ni sahihii na itakuwa imetokana kwa mapenzi ya Mungu.

“Hata hivyo, naomba nipunguziwe adhabu, mimi ni kiumbe dhaifu wa Mwenyezi Mungu…kama adhabu hii nitapunguziwa Mungu ndiye atakuwa amepanga,” alieleza Sultani baada ya hakimu kumpa nafasi ya kujitetea kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo.

Awali, Sultani alianza kuomba dua kwa kutumia lugha ya Kiarabu, lakini Hakimu Chusi alimweleza kuwa haelewi na ndipo mshitakiwa huyo alipotaka atafutwe mkalimani.

Hata hivyo, hakimu alimweleza kuwa hawezi kufanya hivyo na kumtaka kusali kimyakimya.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Chusi alisema kwa kuwa mshitakiwa hajaisumbua mahakama kwa kuleta mashahidi na kwa kuzingatia kuwa ni kosa lake la kwanza, anamhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela.

“Kwa kuwa Sultani umekiri kosa mapema na kukiri kwako kumesaidia mahakama kutopata usumbufu wa kuletwa kwa mashahidi, na pia ni kosa lako la kwanza, nakuhukumu kwenda jela mwaka mmoja,” alisema Hakimu Chusi.

Mshitakiwa huyo alihukumiwa baada kukiri maelezo yote ya kosa aliyosomewa na Wakili wa Serikali, Monica Mbogo.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, mshitakiwa huyo alionekana ni mtu mwenye huzuni, huku mama yake akiangua kilio.

Juzi, mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza akikabiliwa na shitaka moja la shambulio la kudhuru mwili.

Ilidaiwa kuwa Machi 10, mwaka huu, katika ukumbi wa Dimond Jubilee alimpiga kibao shavu la kushoto Rais Mstaafu Mwinyi, ambaye siku hiyo alikuwa akihutubia kwenye Baraza la Maulid.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Machi 14 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.