Header Ads

CHENGE KIZIMBANI

*Asomewa mashitaka ya kusababisha vifo
*Yuko nje kwa dhamana ya milioni moja
*Ndugu zake wawakejeli wanahabari Dar

Na Happiness Katabazi

MBUNGE wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, akiwakabiliwa na mashitaka matatu yakiwemo ya kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha vifo vya wanawake
wawili.

Chenge (61), alifikishwa mahakamani hapo jana, chini ya ulinzi mkali wa wanausalama na kupelekwa moja kwa moja katika chumba cha mahakama ambako alisomewa mashitaka hayo.

Chenge aliingia mahakamani hapo majira ya saa 5:57 asubuhi kwa msafara wa magari mawili, akiwa ameketi kiti cha nyuma kwenye gari PT0217 aina ya Yundai, mali ya Jeshi la Polisi.

Nyuma lilifuatiwa na gari lingine, lenye namba za usajili, T 200ACC, aina ya Toyota Land Cruser ambapo ndani alikuwa amepanda mke wake Chenge na ndugu zake ambao walifika mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo iliyoshuhudiwa pia na umati wa watu ulifurika kushuhudia Waziri huyo wa zamani, akipandishwa kizimbani.

Gari hizo ziliingia mahakamani hapo kwa mwendo kasi na mtuhumiwa aliposhuka, alizongwa na wananchi lakini makachero walijitahidi kudhibiti hali hiyo na kumuongoza hadi kwenye chumba cha kimoja mahakamani hapo na kusomewa mashitaka.

Akimsomea mashitaka hayo, Mwendesha Mashtaka Mkuu, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), David Mafwimbo, alidai mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi, Emiliusi Mchaulo, kuwa katika shitaka la kwanza, Chenge anadaiwa kusababisha kifo cha Victoria George kwa uendeshaji wa gari kizembe.

Alidai kuwa Machi 27 mwaka huu, saa 10:30 alfajiri katika barabara ya Haile Selaissie, Wilaya ya Kinondoni, akiwa anaendesha gari namba T13 ACE, Toyota Hilux Double Cabin, kwa uzembe na kushindwa kuchukua tahadhari kama inavyotakiwa kwa watumiaji wa barabara, aligonga Bajaji T739 AXC na kusababisha kifo cha Victoria ambaye alikuwa abiria katika bajaj hiyo.

ASP Mafwimbo alidai katika shitaka la pili, Chenge anadaiwa siku na muda huo huo, alisababisha kifo cha Beatrice Constantine kwa kuendesha gari kizembe.

Aidha, alidai shitaka la tatu ni kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha uharibifu wa bajaji ambayo ilikuwa imebeba marehemu hao.

Mshitakiwa huyo alikana mashtaka yote na ASP Mafwimbo aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Mchaulo, alisema ili mshitakiwa adhaminiwe, lazima awe na mdhamini mmoja ambaye atasaini bondi ya sh milioni moja.

Chenge, alidhaminiwa na Mkurugenzi wa Fedha toka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHCR), Ezekiel Masanja na kesi hiyo kuahirishwa hadi Aprili 30, itakapotajwa.

Kutokana na uamuzi wa mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo katika chemba ndogo, kulisababisha waandishi wa habari wengi kushindwa kuingia kuisikiliza, huku waandishi wa habari wawili ndio waliofanikiwa kuingia katika chumba hicho.

Wakati hali hiyo ikijitokeza, baadhi ya ndugu za Chenge walikuwa wakitoa kauli za kuwakejeli wanahabari waliokuwapo mahamani hapo kwamba kamwe kesi hiyo haitawaondoa kwenye umaskini.

“Mnajifanya mnaandika na kupiga picha sasa kwa taarifa yenu andikeni weee… lakini kamwe mkijua kesi hii haitawaondoa kwenye umaskini unaowakabili,” alisema mwanamke mmoja ambaye anasadikiwa kuwa ni ndugu wa mshitakiwa.


Hata hivyo, wakati wapiga picha wakizingira gari lililomleta Chenge mahakamani hapo, ili waweze kumpiga picha wakati akitoka mahakamani, katika hali isiyotarajiwa ndugu na jamaa wa mshitakiwa huyo waliwapiga chenga ya mwili na kumpitishia mlango wa nyuma na kisha kupanda gari ambalo liliondolewa kwa mwendo wa kasi.

Chenge ambaye amepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika serikali ya awamu ya tatu na Waziri wa Miundombinu katika serikali ya awamu ya nne, wakati ajali hiyo ikitokea alikuwa akiendesha gari lake binafsi.

Tangu kutokea kwa ajali hiyo, dereva wa bajaj alitoroka na hadi sasa hajulikani alipo.

Kwa Chenge, tukio hilo ni mkasa wa tano mkubwa tangu ilipoanza kumwandama ambapo alishinikizwa ajiuzulu Uwaziri katika Wizara ya Miundombinu mwaka jana kutokana na kashfa ya kuhifadhi zaidi ya bilioni moja katika akaunti aliyokuwa akiimiliki katika visiwa vya New Jersey

Kujizulu kwake kulitokana na kauli yake aliyoitoa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam kwamba fedha zilizokutwa kwenye akaunti hiyo ni Vijisenti tu, akiwa na maana kuwa ni fedha chache kwa mtu wa hadhi yake kuzimiliki.

Kauli hiyo iliamsha hasira kwa wananchi waliokuwa wakimwandamana kupitia vyombo vya habari na hatimaye kuliomba radhi taifa kwa kauli hiyo na baadaye kutangaza kujizulu Uwaziri.

Kabla ya kugundulika kuhifadhi fedha hizo, Chenge alikuwa akikabiliwa na kashfa ya ununuzi wa rada ya serikali inayodaiwa kununuliwa kwa bei kubwa zaidi (sh bilioni 40) na serikali ya awamu ya tatu.

Tukio jingine lilomkumba mbunge huyo ni kuzushiwa kifo ambapo baadhi ya watu walidai amekunywa sumu, ili kukwepa uchunguzi unaofanywa na taasisi ya kuchunguza makubwa ya jina ya Uingereza (SFO)

Baada ya Chenge kujiuzulu, siku chache baadaye alikwenda Bungeni ambako alipatwa na mkasa mwingine pale alipodaiwa kukutwa akitangatanga ndani ya ukumbi wa Bunge, akiambatana na Ofisa mmoja wa Bunge na kudaiwa kuwa alikuwa akimwaga kitu kilichosadikiwa kuwa ni sumu ya kisasa kwenye viti vya baadhi ya wabunge.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 31,2009

No comments:

Powered by Blogger.