Header Ads

MTANGAZAJI MATATANI KWA DAWA ZA KULEVYA

Na Happiness Katabazi

MTANGAZAJI wa Redio Times FM, inayomilikiwa na Kampuni ya Bussiness Times Ltd, Hadija Shaibu, maarufu kwa jina la ‘Dida wa Mchops’ anashikiliwa na askari wa Kitengo cha Kuzuia
Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi baada ya kumshuku kuwa anasafirisha dawa za kulevya.

Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilizolifikia Tanzania Daima Jumatano, zilieleza kuwa Dida alianza kushikiliwa juzi baada ya askari wa kitengo hicho waliopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kumkamata wakati akijiandaa kupanda ndege kwenda China.

Habari zilieleza kuwa Dida alikuwa akijiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopian Air Line, lakini polisi walilazimika kumtia nguvuni baada ya kumpeleleza kwa muda mrefu na kuhisi kuwa huenda siku hiyo alikuwa amemeza dawa hizo ili azisafirishe nje ya nchi.

Zieleza zaidi kuwa baada ya Dida kukamatwa, alipelekwa kwenye choo maalumu kilichopo uwanjani hapo ambacho hutumiwa na askari wa kitengo hicho kuwahifadhi watuhumiwa wanaowakamata wakiwa wamemeza dawa za kulevya kwa muda ambapo endapo mtuhumiwa alikuwa amemeza dawa hizo atazitoa wakati akijisaidia.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa tangu alipoingizwa kwenye choo hicho juzi jioni hadi jana saa nne asubuhi, hakuweza kugundulika kuwa na dawa hizo tumboni ambapo alichukuliwa hadi makao Makuu ya Kitengo hicho, huko Barabara ya Kilwa kwa ajili ya kuhojiwa.

“Nakuhakikishia kuwa jana (juzi) tulimkamata Dida pale uwanja wa ndege, alikuwa akielekea China kwani tulikuwa tukimshuku kuwa amemeza dawa hizo lakini hadi hivi ninavyoongea na wewe yupo mikononi mwetu ila hatujamkuta na pipi hata mmoja.

“Tumemleta hapa ofisini kwetu Kilwa Road kwa ajili ya mahojiano zaidi na tayari mama yake ameishafika na tunaendelea kuchukua maelezo yake ila kwa sababu bado ni mchana ni mapema kukuhakikishia kuwa tutamalizana naye leo au la,” alisema mmoja wa maofisa wa kitengo hicho.

Taarifa nyingine zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa Dida alidhaminiwa jana majira ya saa kumi jioni.

Hata hivyo alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Godfrey Nzowa, ili aweze kuthibitisha taarifa hizo alishindwa kukubali au kukataa na badala yake akaishia kusema atafuatilia.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Machi 25,2009

No comments:

Powered by Blogger.