Header Ads

FEDHA ZA EPA ZILIKUWA ZIKITUNZWA NBC-SHAHIDI

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa nane katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Meneja Uhusiano wa Benki Kimataifa katika Benki ya NBC, Lyson Mwakapenda (64) ameiambia mahakama kuwa malimbikizo ya fedha za EPA awali yalikuwa yakitunzwa kwenye benki hiyo.

Mwakapenda alieleza malimbikizo ya madeni ya EPA yalianza mwaka 1979 na ilipofika kwamba mwaka 1985 baada ya makubaliano katika ya NBC na BoT na serikali iliridhia madeni hayo yaamishiwe BoT.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili wa Serikali Vitalis Tomoni ambaye alikuwa akisaidiana na Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus na shahidi huyo;

Wakili: Unafanyakazi wapi?
Shahidi: NBC Makao Makuu.
Wakili: Kama nani pale?
Shahidi: Meneja Uhusiano wa Benki ya Kimataifa katika benki hiyo.
Wakili: Majukumu yako nini?
Shahidi: Kufanyakazi kwa kushirikiana na benki za nje ya nchi.
Wakili: EPA ni nini ?
Shahidi: Ni malimbikizo ya madeni ya wafanyabiashara wa nje ambao serikali yetu ilishindwa kuyalipa kwa wakati ule.
Wakili: NBC ilihusika vipi na malimbikizo hayo?
Shahidi: Wafanyabishara hao wa nje walikuwa na akaunti katika benki yetu na ndipo walikuwa wanatarajia malipo yao kupitia kwenye akaunti hizo.
Wakili: NBC ilikuwa inalipaje fedha hizi?
Shahidi: Kabla ya kuwalipa nilazima NBC ilikuwa inapata kibali cha kuwalipa toka BoT.
Wakili: Nini kilifanya msilipe fedha hizo za kigeni(EPA) kwa wakati?
Shahidi: Taifa lilikuwa lina uhaba wa fedha za kigeni za kuweza kulipa madeni hayo.
Wakili: Hao wafanyabiashara/waagizaji walikuwa wanaleta fedha za aina gani?
Shahidi: Fedha za Kitanzania.
Wakili: Kulikuwa na makundi gani ya waingizaji?
Shahid: Kundi la watubinafsi, makampuni ya serikali na umma.
Wakili: Hawa waagizaji walikuwa wa njia ngapi za kulipa fedha?
Shahid: Letter for Credit,Bill of Exchange , open account.
Wakili: Tuambie ni kipindi gani malimbikizo yalianza?
Shahidi: Mwaka 1979.
Wakili: Mliwekaje kumbukumbu za malimbizo hayo?
Shahidi: Kwenye rekodi ya vitabu vya benki.
Wakili: Je kulikuwa na rejista yoyote yoyote?
Shahidi: Kwenye matawi ya benki yetu rejista ilikuwepo.
Wakili: Zilikuwa zinaitwaje?
Shahidi: LC rejister, IFBC.
Wakili: Lini hizo kumbukumbu zilipelekwa BoT?
Shahidi: Mwaka 1985.
Wakili: Kwa sababu gani?
Sahidi: Baada ya makubaliano kati ya NBC na BoT ndiyo serikali ikalidhia kwamba malimbikizo hayo yamishiwe BoT. Na baada ya makubaliano hayo kila wiki NBC ilikuwa inakusanya fedha hizo na kupeleka Benki Kuu ambapo ndipo kwenye akaunti ya EPA.
Wakili: Utaratibu huo uliendelea hadi lini?
Shahidi: Septemba 1993.
Wakili: Nini kilisababisha kusimamishwa?
Shahidi: Ulitolewa waraka na BoT kwamba NBC isipeleke fedha BoT kwani fedha za kigeni wakati huo zilianza kupatikana kutokana na kuwepo kwa soko huria.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Farijara Hussein na Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda ambao wanadaiwa kuiibia BoT sh bilioni 1.8. Kesi imeahirishwa hadi Jumatatu ijayo itakapoendelea kusikilizwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Machi 21 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.