Header Ads

KESI YA LIYUMBA YAPANGIWA HAKIMU

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imempangia Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, kusikiliza kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Mradi wa BoT, Deogratius Kweka.

Hatua ya kupangiwa hakimu hiyo imekuja ikiwa wiki moja imepita, tangu hakimu Mkazi Hadija Msongo, aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, kuamua kujitoa kwa madai kuwa mwenendo wa kesi hiyo umekuwa ukilalamikiwa na waendesha mashitaka na mawikili kupitia vyombo vya habari

Wakili Kiongozi wa Serikali Stanslaus Boniface, aliyekuwa akisaidiana Prosper Mwangamila,Tabu Mzee toka Taasisi ya Kzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), alieleza kuwa, kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa hakimu.

Hakimu Lema kwa upande wake, alisema kesi hiyo itakuja tena Aprili 2 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa maombi ya kutaka Liyumba na mwenzake waachiliwe huru kwa madai kuwa uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kufungua kesi hiyo, una dosari za kisheria.

Ijumaa iliyopita, Hakimu Msongo, alitangaza uamuzi wa kujitoa kusikiliza kesi hiyo kwa kile alichokieleza kuwa baadhi ya wananchi na mawakili wa upande wa utetezi, wamekuwa wakilalamikia mwenendo wa kesi hiyo kupitia vyombo vya habari.

Februari 17 mwaka huu, hakimu Msongo alimwachia kwa dhamana iliyozua utata Liyumba.

Utata huo, ulitokana na kauli ya wakili wa serikali, Justas Mulokozi kuonyesha kushangazwa na uamuzi wa kumwachia mtuhumiwa huyo licha ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Moja ya masharti ambayo wakili huyo alidai hayakutimizwa na Liyumba ni kuwasilisha mahakamani hati zenye thamani ya sh bilioni 55, wadhamini wawili wa serikali wakiwa na barua kutoka kwa waajiri wao na kukabidhi hati za kusafiria mahakamani hapo.

Lakini siku hiyo Liyumba aliwasilisha hati yenye thamani ya sh milioni 882, hati ya kusafiria ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, huku wadhamini wawili wakiwa hawana barua zilizosainiwa na mwajiri wao kama masharti yalivyotolewa na mahakama.

Februali 24 mwaka huu, Liyumba alifika mahakamani hapo na hakimu Msongo alisema hati 10 za wadhamini zenye thamani ya sh bilioni 55, ndizo zilizotumika kujaribu kumdhamini mshitakiwa huyo mara ya kwanza, lakini zilikataliwa baada ya kubainika kuwa zilikuwa na kasoro za kisheria, huku nyingine zikidaiwa kuwa ni za kughushi.

Kutokana na kasoro hizo, hakimu Msongo aliagiza hati hizo zipelekwe Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na tayari Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba, aliliambia Tanzania Daima kuwa hati hizo uchunguzi wa hati hizo, umeanza.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Machi 21 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.