Header Ads

HAKIMU KESI YA LIYUMBA AJITOA

Na Happiness Katabazi

BAADA ya kelele nyingi kupigwa kuhusu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kupamtia dhamana yenye utata aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT), Amatus Liyumba, hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi amejitoa.

Hakimu Mkazi, Hadija Msongo ambaye ndiye alikuwa akisikiliza kesi hiyo, alitangaza uamuzi huo jana, wakati kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa kwa ombi la mawakili wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na wakili wa kujitegemea Profesa Gamaliel Mgongo Fimbo ya kutaka Liyumba na mwenzake waachiliwe huru kwa sababu uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa kuwashtakiwa una dosari za kisheria.

Hata hivyo, ombi hilo halikuweza kusikilizwa kutokana na hakimu huyo kutangangaza kujitoa kusikiliza kesi hiyo.

Hakimu Msongo alitoa uamuzi huo muda mfupi baada ya wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, Prospa Mwangamila na mawakili wa utetezi Profesa Fimbo, Hurbet Nyange, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu kujitambulisha kwake na kumweleza wapo tayari kwa ajili ya kesi hiyo kuendelea.

Baada ya mawakili hao kujitambulisha hakimu huyo alisema kutokana na mwenendo wa kesi hiyo kulalamimikiwa baada ya mshitakiwa Liyumba kupewa dhamana, anaona ni busara kujitoa kuendesha kesi hiyo.

“Kutokana na mwenendo wa kesi hii kulalamikiwa wazi wazi na Watanzania na waendesha mashtaka wa kesi hii kupitia vyombo vya habari na mbele ya jamii mahakma imeonekana imekosea.

“Na ili haki ionekane imetendeka, najitoa kwenye kesi hii na jalada la kesi nitampelekea kwa Hakimu Mfawidhi wa mahakama hii, ili aweze kumpangia hakimu mwingine,” alisema hakimu Msongo.

Baada ya kutoa uamuzi huo, Profesa Fimbo aliinuka kudai kuwa washtakiwa kwa kuwa wapo kizimbani aliomba kesi hiyo jana ile ile ipangiwe kwa hakimu mwingine, ili waweze kujua tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Hata hivyo, Msongo alisema kesi hiyo itatajwa Machi 20 mwaka huu, ambapo itakuwa imeshapangiwa hakimu mwingine wa kuiendesha kesi hiyo.

Februari 17 mwaka huu, Msongo alimwachia kwa dhamana iliyozua utata Liyumba na utata huo ulitokana na kauli ya wakili wa serikali Justas Mulokozi, kuonyesha kushangazwa na uamuzi wa kumwachia mtuhumiwa huyo licha ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Moja ya masharti ambayo wakili huyo alidai hayakutimizwa na Liyumba ni kuwasilisha mahakamani hati zenye thamani ya sh bilioni 55, wadhamini wawili wa serikali wakiwa na barua kutoka kwa waajiri wao na kukabidhi hati za kusafiria mahakamani hapo.

Lakini siku hiyo Liyumba aliwasilisha hati yenye thamani ya sh milioni 882, hati ya kusafiria ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, huku wadhamini wawili wakiwa hawana barua zilizosainiwa na mwajiri wao kama masharti yalivyotolewa na mahakama.

Februali 24 mwaka huu, Liyumba alifika mahakamani hapo na hakimu Msongo alisema hati 10 za wadhamini zenye thamani ya sh bilioni 55, ndizo zilizotumika kujaribu kumdhamini mshitakiwa huyo mara ya kwanza, lakini zilikataliwa baada ya kubainika kuwa zilikuwa na kasoro kubwa za kitaalam, huku nyingine zikidaiwa kuwa ni za kughushi.

Aidha alisema kutoka na hati hizo kuwa na kasoro hizo aliagiza zipelekwe Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na tayari Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(DCI) Robert Manumba aliliambia Tanzania Daima kuwa hati hizo ameishazipokea na tayari wameishaanza kuzifanyia uchunguzi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Machi 14 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.