Header Ads

JWTZ YAJA NA KAMANDI YA MAJESHI YA NCHI KAVU


*Sasa kuna muundo wa kamandi tatu za majeshi
*Rais Kikwete asema JWTZ inakwenda na wakati

Na Happiness Katabazi

“TUKIO hili la uzinduzi wa Kamandi ya Majeshi ya Nchi Kavu “Land Forces Command(LFC) ni tukio la kihistoria la maendeleo ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ).

“Leo ni siku muhimu kwani tunashuhudia mabadiliko ya muundo jeshi ambalo sasa litaundwa na Kamandi tatu yaani Jeshi Kamandi ya askari wa Majini, Anga na Nchi Kavu,”

Maneno hayo anayatamka Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, Rais Jakaya Kikwete wakati akizungumza na maafisa ,wapiganaji na wananchi wakati akizindua rasmi Kamandi ya Majeshi ya Nchi Kavu katika kambi
ya Nyerere ya JWTZ, Machi 4 mwaka huu.

Makao makuu ya kambi hiyo ipo eneo la Msangani, Kibaha Mkoani Pwani.


Kuzinduliwa kwa kamandi hii ya nchi kavu inayoongozwa na Kamanda, Meja Jenerali Wynejones Kisamba, kuna tufanya Watanzania tuwe na kila sababu ya kujivunia kwasababu sehemu kubwa ya jeshi letu ni la askari wa miguu( infantry)

Binafsi nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari wachache tulioudhuria uzinduzi wa Kamandi hiyo.

Safari yetu ya kwenda katika uzinduzi huo, ilianzia Idara ya Habari (MAELEZO) ambapo kulikuwa na waandishi watatu toka vyombo mbalimbali akiwemo mwandishi mmoja toka Jeshi la Polisi.

Tuliungana na waandishi wa JWTZ kuelekea Kibaha, tukiwa ndani ya basi la jeshi hilo tulipata fursa ya kubalidishana mawazo, kwa hakika tulifurahia safari ile na jinsi maongezi yalivyonoga tulishtukia tumechukua muda mfupi tumefika.

tulishamaliza rami ya barabara ya Morogoro na kukatisha kulia kuelekea eneo la Msangani Kibaha ambapo ndipo ilipo Kamandi hiyo.

Tukiwa njiani kuelekea kwenye eneo hilo , tuliwaona wanajeshi wakiwa wamesimama kandokando ya barabara ya hivyo vumbi pamoja na wananchi waliotumia njia hiyo kwenda uzinduzi.

Kwa kifupi ulinzi ulikuwa ni wa kutosha kwani licha ya sisi wanahabari kufika eneo lile, maofisa usalama waliokuwa nje ya geti katika eneo lile, walitushuhudia kwa macho tukishuka toka kwenye basi la JWTZ lakini walitupata ‘kashikashi’ za hapa na pale.

Lakini kwa mimi niliyezoea ubabaishaji wa baadhi ya wanajeshi wetu, halikunisumbua kwani nilitambua nipo pale kwaajili ya kutimiza wajibu wangu wa kulitumikia taifa kupitia kalamu yangu.

Rais Kikwete ambaye kabla kuingia kwenye ulingo wa siasa alikuwa mwanajeshi, siku hiyo muda wote alionekana kuwa ni mwenye furaha.

Akizungumza katika uzinduzi huo wa Kamandi ya Majeshi ya Nchi Kavu, rais Jakaya Kikwete anasema uzinduzi huo, umeleta tukio la kihistoria kwa maendeleo la JWTZ.

Anasema umeleta mabadiliko ya kiutawala na kudhibitisha kuwa jeshi hilo linakwenda na wakati.
“Kuundwa kwa Kamandi hii kuna kuleta ufanisi kwa Kamandi nyingine za Kamandi ya Maji na Anga.

“Naomba muendelee kuwa wabunifu ili muende na wakati...boresheni vifaa vyenu na mitaala ya mafunzo ya kijeshi kwani serikali inawaaidi kuwapa upendeleo pindi bajeti itakapo ruhusu,” anasema rais Kikwete ambaye muda wote alionekana kuwa na furaha.

Kikwete amewakumsha maofisa na wapiganaji wa jeshi hilo kwamba ili Jeshi liendelee kupiga hatua kimaendeleo ni lazima wadumishe umoja, mshikamano, ujasiri, nidhamu na weledi.

“Nitakuwa siwatendei haki kama sitatoa pongezi kwa JWTZ kwa kazi nzuri mnayofanya ya kulinda mikapa ya nchi yetu kwani leo hii amani tunayojivunia, kwa asilimia kubwa inatokana na ulinzi wenu imara katika mipaka yetu.

“Jeshi letu ni imara kwani linameshiriki operesheni nyingi duniani na limefundisha wapiganaji wengi hadi leo ninavyozungumza nanyi tumepokea maombi ya kututaka tupeleke askari wetu nchini Chadi kwaajili ya kwenda kukomesha machafuko,” anasema Kikwete huku hotuba yake ikiwa inakatishwa na makofi na wanajeshi hao.

Aidha Kikwete anasema ameamua kuongeza umri wa kustaafu kwa wanajeshi hao na uamuzi huo utaanza kutekelezwa rasmi Julai mosi mwaka huu na utausisha wanajeshi wa vyeo vyote.

Kikwete anasema kwa sasa mwanajeshi wa cheo cha juu kama Meja Jenerali anastaafu jeshi akiwa na umri wa miaka 57 na kufafanua uamuzi huo ukianza kutekelezwa mwanajeshi mwenye cheo hicho atastaafu jeshi akiwa na umri wa miaka 60.

Anasema amefikia uamuzi huo wa kuongeza umri wa kustaafu kwa wanajeshi baada ya kubaini kuwa kuna wanajeshi wenye sifa na taaluma mahususi ambao kutokana vyeo vyao na taratibu za kijeshi wamekuwa wakistaafu huku Jeshi likiwa linahitaji mchango wao.

“Ndani ya Jeshi letu kuna wanajeshi wenye taaluma mahususi na muhimu katika jeshi letu.

“Kutokana na utaratibu wa kustaafu uliowekwa ndani ya JWTZ, wanajeshi wamekuwa wakistaafu wakiwa na umri mdogo na kwasababu hiyo…leo natangaza rasmi kwamba nimeongeza umri wa kustaafu kwa wanajeshi wa vyeo vyote na agizo hili litaanza kutekeleza Julai Mosi mwaka huu,” anasema.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi hilo (CDF), Jenerali Davis Mwamunyange anasema uzinduzi huo ni hatua moja mbele ya jeshi hilo kutimiza malengo yake.

Mwamunyange anasema kabla ya kuundwa kwa Kamandi hiyo, Makao Makuu ya Jeshi ndiyo ilikuwa na jukumu la kusimamia kikosi hicho cha Askari wa Miguu.

Jenerali Mwamunyange anasema kuanzishwa kwa Kamandi hiyo, kumepunguza mzigo wa kwa Makao Makuu ya Jeshi hilo kwani hivi sasa itabaki na jukumu la kusimamia sera na maslahi ya wanajeshi nchi nzima.

Mwamunyange amekumbusha kuwa tangu miaka 1980 Jeshi hilo lilikuwa na Kamandi mbili za anga na maji nakuongeza kuwa askari wa miguu waliongozwa na Divisheni iliyokuwa chini ya Makao Makuu ya Jeshi.

Anasema uzinduzi wa Kamandi hiyo ya nchi kavu umeiwezesha Makao Makuu ya Jeshi kubaki na majukumu ya kisera za jeshi hilo kwa nchi nzima na kusimamia maslahi ya wanajeshi wa jeshi hilo .

“Uzinduzi wa Kamandi hii umedhiirisha kwamba JWTZ lipo tayari kwenda na wakati, litaendelea kujiimarisha kiutendaji kivita na utawala na kwamba uzinduzi huo utaiwezesha JWTZ kuwa na Kamandi tatu.

Tukio hili ni la kihistoria ndani ya Jeshi na taifa kwa ujumla kwani Jeshi hilo lilikuwa na Kamandi mbili, Kamandi ya Ulinzi wa Anga(AFC) na Kamandi ya Wanamaji(Navy).

“Kwa niaba ya JWTZ na Watanzania kwamba jeshi hili litaendelea kujiimarisha zaidi na kwenda na wakati kwa maslahi ya taifa letu,” anasema Jenerali Mwamunyange.

Anasema Kamandi hiyo ya nchi kavu itakuwa ikiongoza Brigedi tano; Brigedi ya Faru-Tabora, Chui iliyopo Dar es Salaam, Nyuki-Zanzibar, Mbuni-Arusha na Tembo-Arusha.

Anaongeza kuwa itakuwa ikiongoza vikosi vyote vya mizinga na vifaru,vikosi vya waandisi wa medani pamoja na vyuo na shule zinazotoa mafunzo ya Kijeshi.

Aidha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa , Dk. Hussein Mwinyi anasema muundo huo mpya utaliwezesha JWTZ kutekeleza majukumu yake ya ulinzi wa nchi, watu na mali zao kwa ufanisi mkubwa kwani kila Kamandi itakuwa na majukumu yake.

Mamia ya watu wakiwemo wakuu wa majeshi, wanadhimu wastaafu, familia za wanajeshi na wananchi wa maeneo mbalimbali waliudhuria uzinduzi huo ambao umeweka historia kwa JWTZ.
(Pichani juu kulia ni Mkuu wa Kambi hiyo Meja Jenerali, Kisamba)
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 12 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.