Header Ads

ALIYEMPIGA MWINYI AIBUA MAPYA

*Asema ni mara ya tatu kufanya hivyo
*Apandishwa kizimbani, kukiri kosa
*Aliyemrushia viatu Bush afungwa miaka 3

Na Happiness Katabazi

KIJANA Ibrahimu Said Sultani ‘Ustaadhi’ (26) aliyempiga kofi Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, amemwomba radhi Mwinyi na Watanzania kwa ujumla na kuwataka wamsamehe kwa kosa alilolitenda.

Sultani, alitoa kauli hiyo jana mbele ya waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shitaka hilo ambalo alikiri.

“Namuomba Mzee Mwinyi, Watanzania, waislamu wenzangu na serikali inisamehe kwa kitendo nilichokifanya, kwani sikujua kama jambo hili litakuwa kubwa kiasi hiki.

‘Sikumuelewa vizuri Mwinyi kutokana na uelewa wangu mdogo ndiyo umesababisha nifanye kitendo kile. Bado ninahitaji kusoma. Nafundisha tuition na kipato ninachopata ni kidogo…naomba serikali na jamii inione mtu wa kawaida, licha ya tukio hili linaweza likasababisha nisipate nafasi ya ajira au shule serikalini.

“Hii ni mara yangi ya tatu kufanya matukio kama haya, licha ya tukio hili kuwa kubwa,” alisema Sultani, lakini kabla ya kujibu matukio mengine aliyafanyia wapi alichukuliwa na maofisa usalama na kupelekwa mahabusu ya mahakama hiyo.

Baada ya kupandishwa kizimbani, mbele ya Hakimu Mkazi, Neema Chusi, Wakili wa Serikali, Monica Mbogo akimsoma mashitaka alidai mshitakiwa huyo anakabiliwa na shitaka la shambulio la kudhuru mwili.

Alidai Machi 10 mwaka huu, katika ukumbi wa Dimond Jubilee, uliopo Upanga, Dar es Salaam, bila halali yoyote alimshambulia Mwinyi kwa kumpiga kofi katika shavu la kushoto.

Mshitakiwa huyo alikiri kosa na hakimu Chusi kuahirisha kesi kwa muda wa saa moja, ili wakili wa serikali apate muda wa kuandaa maelezo ya kosa hilo na kusomewa kabla ya kutolewa kwa hukumu.

Ilipofika saa 2:45 wakili mwingine wa serikali, Prospa Mwangamila aliingia mahakamani na kumuomba hakimu airishe kesi hiyo hadi leo kwa sababu wameshindwa kuandaa maelezo hayo kutokana na vifaa vya kuandaa maelezo hayo kupata hitilafu.

“Mheshimiwa hakimu tunaomba usomwaji wa maelezo ya kosa dhidi ya mshitakiwa leo (jana) uairishwe hadi kesho (leo), kwani vifaa vya kuchapia maelezo hayo vimekorofisha, hivyo licha ya mahakama hii kutupa saa moja kwenda kuandaa maelezo hayo tumeshindwa kuyaandaa,” alieleza Mwangamila.

Hakimu Chusi alikubali ombi hilo na kuairisha kesi hiyo hadi leo ambapo mshitakuwa huyo atasomewa maelezo na kupewa adhabu kwa mujibu wa kanuni ya adhabu.

Baada ya mshitakiwa kutolewa kizimbani, mama mzazi wa mshitakiwa huyo aliyejitambuliwa kwa jina la Mama Rehema, alikimbilia kwenye chumba kimoja cha mahakama ambacho mshitakiwa huyo na washtakiwa katika kesi nyingiine walikuwa wameifadhiwa na kuzungumza na mwanae.

Baadaye akizungumza na waandishi wa habari Mama huyo alisema mwanae amekuwa akitumia muda mwingi kusoma na kuongeza kuwa kitendo alichofanya mwanae ni kinyume na vitabu vya dini na sheria za nchi.

“Mwanangu hapati muda wa kupumzika amekuwa akijisomea na kufundisha watu kila mara na binafsi siungi mkono kitendo pia nawashukuru nanyi waaandishi wa habari kwa upendo wenu mmeweza kukusanyika hapa kumuona mwanangu..sote tumuombe Mungu” alisema Mama Rehema ambaye alikuwa ameongoza na ndugu na jamaa.

Jumanne wiki hii, Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Baraza la Maulidi wakati akihutubia ghafla alitokea mshitakiwa huyo na kumzaba kofi, hali iliyosababisha wanausalama kumkamata na kufikisha kituo cha Polisi.

Tangu kutokea kwa tukio hilo taasisi mbalimbali za kidini zimejitokeza kulaani kitendo hicho.

Wakati huohuo, Habari kutoka Baghdad, zinaeleza kuwa Mwandishi wa habari wa Iraq aliyemrushia viatu Rais wa zamani wa Marekani George W Bush, jana amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kumfedhehesha kiongozi wa kigeni.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya mwandishi huyo, Muntadhar al-Zeid (30) kudai kuwa hana hatia kwa kile alichokieleza kuwa kitendo hicho kilikuwa ni ujibuji wa kawaida (natural response).

Al Zeid alitoa jibu hilo baada ya Jaji aliyekuwa akitoa hukumu hiyo, Abdul-Amir al-Rubaie, kumuuliza kama alikuwa ana hatia ama la.

Hata hivyo, mwandishi huyo alipiga kelele wakati hukumu hiyo ikisomwa akisema ‘idumu Iraq’

Al-Zeidi ambaye ilibidi afungwe miaka 15 jela kwa kitendo cha kumrushia viatu vyake Bush wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki, lakini wanasheria wa upande wa utetezi walisema kuwa jaji aliyetoa hukumu hiyo ameonesha ubinadamu kwa sababu ya umri wa al-Zeidi pamoja na rekodi safi aliyonayo.

Hata hivyo, wanasheria hao wa upande wa utetezi walisema watakata rufaa kwa sababu wanaamini kitendo hicho kilikuwa ni upingaji wa kisiasa ambao ni wa halali na kwamba hakistahili kifungo.

“Hukumu hii sio mwisho,” alisema kaka wa al-Zeidi aliyejulikana kwa jina la Dargham huku akitokwa na machozi.

Baadhi ya ndugu wa mwandishi huyo walianguka na wengine kuzimia baada ya hukumu hiyo kutolewa na mahakama.

Habari zimeeleza ndugu wengine walitolewa kwa nguvu na maofisa wa usalama toka katika chumba cha mahakama baada ya kuanza kurusha maneno ya kashfa dhidi ya Bush.

Al-Zeid ambaye alikuwa amevailia suti ya rangi ya kahawia na viatu vya kahawia, alitembea kwa haraka hadi katika eneo ambalo wanawekwa watetezi na kusalimia jopo la majaji watatu huku akiinamisha kichwa chini kwa heshima.

Raia wengi wa Iraq wanamchukulia al-Zeidi kama shujaa kwa kuonesha hisia zake kwa Rais Bush ambao wanaamini ameiharibu nchi yao baada ya Marekani kuivamia kijeshi mwaka 2003.

Maelfu ya waamini wa dini ya kiislamu duniani waliandamana mitaani wakitaka mwandishi huyo wa habari aachiwe.

Mwandishi huyo alikuwa kizuizini nchini Iraq tangu alipotenda kitendo hicho Desemba 14 katika mkutnao wa waandishi wa habari ambako alimrushia viatu vyake Bush, ambaye hata hivyo alivikwepa haraka kwa kuinama na hivyo viatu hivyo kugonga ukuta.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi 13 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.