Header Ads

JK AWAONGEZEA WANAJESHI UMRI WA KUSTAAFU

Na Happiness Katabazi, Kibaha

AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, Rais Jakaya Kikwete, ameongeza umri wa kustaafu kwa wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).


Rais Kikwete alisema hayo jana alipozungumza na maofisa, wapiganaji na wananchi wakati akizindua Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu (Land Force Command (LFC) ya (JWTZ) yenye makao makuu yake eneo la Msangani, Kibaha mkoani Pwani, kupandisha bendera mpya ya kamandi hiyo, kupanda miti na kukagua gwaride.

Rais Kikwete alisema uamuzi huo utaanza kutekelezwa Julai mosi mwaka huu na utahusisha wanajeshi wa vyeo vyote.

Alisema kwa sasa mwanajeshi wa cheo cha juu kama Meja Jenerali anastaafu akiwa na umri wa miaka 57 na kufafanua uamuzi huo ukianza kutekelezwa mwanajeshi mwenye cheo hicho atastaafu akiwa na umri wa miaka 60.

Alisema amefikia uamuzi wa kuongeza umri wa kustaafu kwa wanajeshi baada ya kubaini kuwa kuna wanajeshi wenye sifa na taaluma ambao kutokana vyeo vyao na taratibu za kijeshi wamekuwa wakistaafu huku jeshi likiwa linahitaji mchango wao.

“Ndani ya jeshi letu kuna wanajeshi wenye taaluma mahususi na muhimu katika jeshi letu na kutokana na utaratibu wa kustaafu ambao uliwekwa ndani ya JWTZ, wanajeshi hao wamekuwa wakistaafu wakiwa na umri mdogo, na kwa sababu hiyo…leo (jana) natangaza rasmi kwamba nimeongeza umri wa kustaafu kwa wanajeshi wa vyeo vyote na agizo hili litaanza kutekelezwa Julai mosi mwaka huu,” alisema Rais Kikwete.

Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa kamandi hiyo inayoongozwa na Meja Jenerali Wynejones Kisamba, alisema uzinduzi huo ni tukio la kihistoria kwa maendeleo la JWTZ, kwani yameleta mabadiliko ya kiutawala na kuthibitisha kuwa jeshi hilo linakwenda na wakati.

‘Kuundwa kwa LFC, kutaleta ufanisi kwa kamandi nyingine za Maji na Anga. Naomba muendelee kuwa wabunifu, ili mwende na wakati. Vifaa vyenu mboreshe, mitaala ya mafunzo ya kijeshi mboreshe na serikali inawaaidi kuwapa upendeleo pindi bajeti itakaporuhusu,” alisema.

Hata hivyo, aliwakumbusha maofisa na wapiganaji wa jeshi hilo kwamba ili jeshi liendelee kupiga hatua kimaendeleo, ni lazima wadumishe umoja, mshikamano, ujasiri, nidhamu na weledi.

“Nitakuwa siwatendei haki kama sitatoa pongezi kwa JWTZ kwa kazi nzuri mnayofanya ya kulinda mipaka ya nchi yetu, kwani leo hii amani tunayojivunia, kwa asilimia kubwa inatokana na ulinzi wenu imara katika mipaka yetu.

“Jeshi letu ni imara, kwani limeshiriki operesheni nyingi duniani na limefundisha wapiganaji wengi hadi sasa (jana), ninavyozungumza nanyi tumepokea maombi ya kutaka tupeleke askari wetu nchini Chad kwa ajili ya kwenda kukomesha machafuko,” alisema Rais Kikwete.

Kwa upande wake, Mkuu wa jeshi hilo, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema uzinduzi huo ni hatua moja mbele ya jeshi hilo kutimiza malengo yake na kabla ya kuundwa kwa kamandi hiyo, makao makuu ya jeshi ndiyo yalikuwa na jukumu la kusimamia kikosi hicho cha askari wa miguu.

Jenerali Mwamunyange alisema kuanzishwa kwa kamandi hiyo, kumepunguza mzigo kwa makao makuu ya jeshi hilo, kwani sasa yatabaki na jukumu la kusimamia sera na masilahi ya wanajeshi nchi nzima.

‘Uzinduzi wa kamandi hii umedhihirisha kwamba JWTZ lipo tayari kwenda na wakati, kwani limedhihisha kuwa tayari litaendelea kujiimarisha kiutendaji, kivita na utawala na kwamba uzinduzi huo utaliwezesha JWTZ kuwa na kamandi tatu,” alisema.

Alisema tukio hilo ni la kihistoria ndani ya jeshi na taifa kwa ujumla, kwani jeshi hilo lilikuwa na kamandi mbili ambazo ni Kamandi ya Ulinzi wa Anga (AFC) na Kamandi ya Wanamaji (Navy).

Alisema Kamandi hiyo ya Nchi Kavu itakuwa ikiziongoza Brigedi tano, ambazo ni Brigedi ya Faru-Tabora, Chui iliyopo Dar es Salaam, Nyuki-Zanzibar, Mbuni-Arusha na Tembo-Arusha, na kuongeza kuwa itakuwa ikiongoza vikosi vyote vya mizinga na vifaru, vikosi vya waandisi wa medani, vyuo na shule zinazotoa mafunzo ya kijeshi.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alisema muundo huo mpya utaliwezesha JWTZ kutekeleza majukumu yake ya ulinzi wa nchi, watu na mali zao kwa ufanisi mkubwa zaidi, kwani kila kamandi itakuwa na majukumu yake.

Mamia ya watu wakiwemo makamanda wastaafu, wakuu wa majeshi, wanadhimu wastaafu, familia za wanajeshi na wananchi wa maeneo mbalimbali walihudhuria uzinduzi huo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 5 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.