SERIKALI INAFANYA USANII
(Mtazamo)
Kura za mauaji ya albino ni usanii mtupu
Na Happiness Katabazi
NINAPENDA kuishauri serikali iache kuwadanganya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwa kura za maoni. Nataka itamke wazi kuwa hili limewezekana kutokana na tabia ya Watanzania kuwa na mazoea ya kushabikia hoja zinazotolewa na viongozi wetu hata kama hoja hizo ni mufilisi.
Tabia hiyo inafanana na mfano huu. Kuna Wazee wa Baraza la Mfalme wa nchi moja ambalo walijua kwamba mfalme wao anapenda sana sifa.
Kwa hiyo, kila mara wazee hao walipomwona mfalme wao amefanya jambo walimsifu sana hata kama jambo lenyewe ni la kipuuzi; halina manufaa kwa taifa.
Basi siku moja mfalme alitaka avae nguo nzuri ya kupendeza kuliko binadamu yoyote. Akatokea msanii mmoja, fundi cherehani, akaja mbele ya mfalme huyo akasingizia kwamba amebeba nguo aliyomshonea mfalme.
Mfalme akahoji: ‘‘Hiyo nguo mbona siioni?’’ Fundi cherehani akamjibu: “Nguo hiyo haionekani hadi nikuvishe mimi na nikishakuvisha kila mtu atakusifu jinsi utakavyopendeza.”
Basi wakaingia faragha. Fundi cherehani akamvisha ile nguo na kisha mfalme akajitokeza hadharani akiwa uchi wa mnyama.
Ndipo mfalme akawauliza Wazee wa Baraza: “Mnaonaje nguo yangu hii mpya niliyovaa?’’ Basi wazee wale wakasema leo ama kwa hakika mfalme umependeza na hujawahi kupendeza kama leo.
Lakini akapita mtoto mdogo akamwona mfalme akiwa katika hali ile na kuhoji: ‘‘Mbona leo mfalme yupo uchi?’’ Ndipo baraza zima la mfalme lilipotambua ukweli kwamba hakika mfalme alikuwa uchi.
Je, yahitaji ajitokeze mtoto mmoja kumwambia Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa wazo la kura za maoni si ufumbuzi wa tatizo la mauaji ya albino na halina tija yoyote kwa taifa?
Kwa hakika wazo hili halina mantiki yoyote na pilikapilika hizi za kura za maoni hazitufikishi mahala popote.
Ila zinatudhihirishia kwamba Serikali ya Awamu ya Nne imeshindwa kulipatia tatizo hili ufumbuzi wa kudumu.
Tukubali kwamba Tanzania haina sheria ya uchawi. Sheria tuliyorithi kutoka kwa wakoloni inapinga kuwapo kwa uchawi, ila inakubali mtu kukamatwa akiwa na zana zinazosadikiwa kuwa ni za kufanyia uchawi.
Huo ni upungufu mkubwa katika sheria za nchi, kwa sababu uchawi upo na watu wenye imani za kishirikina wameamua kushiriki kikamilifu kwenye vitendo vya kichawi kila kukicha.
Katika medani ya siasa, idadi kubwa ya wanasiasa hapa nchini wanashiriki kwenda kwa waganga wa kienyeji kuchanjwa chale kupiga ramli, kufanya mazindiko, kung’arishwa nyota, kupewa mvuto wa kupendwa na watu na vikorombwezo vya kila namna.
Je, hawa wanasiasa wa aina hii wakiombwa na waganga wao wapeleke viungo vya albino watavipata wapi?
Katika sekta ya michezo, hususani mpira wa miguu, ni utamaduni wa kawaida timu husika kuamini mambo ya kishirikina kama sehemu ya mbinu ya kupata ushindi.
Hapo zamani ilikuwa kila timu ina mganga wake na aliitwa ‘fundi’, ambaye huweza kutoa matokeo hata kabla ya mchezo ukiwa bado haujachezwa.
Kwenye sekta ya ajira, wapo watu ambao ajira zao zimeegemea sana tunguli. Pia kupanda kwao vyeo kunategemea tunguli.
Na ukisoma kwenye matangazo magazetini, kwenye mabango mitaani, ukitazama televisheni, hata ukisikiliza redio, waganga wa jadi wanajisifu kwa uwezo mkubwa walionao wa kuweza kuyafanyia kazi maisha ya wanadamu wenzao, achilia mbali suala la mahusiano.
Ukweli ni kwamba suala la imani ya kishirikina limetamalaki. Waganga wanasema wanaweza kukupatia dawa kama ukitaka kumvutia mwanamme akupende na akupe mshahara wake wote, atelekeze familia yake na akufuate wewe. Sisi wenyeji wa Mkoa wa Kagera tunaita dawa hizo ‘shuntama’.
Hata kuvipa nguvu viungo vya kufanyia tendo la ndoa na kuvinenepesha au kuvirefusha, waganga maarufu kwa jina la ‘sangoma’ wanasema hayo yote wanayaweza pia.
Kwa ufupi, utamaduni wetu kuhusu suala la uchawi linatusuta. Na kwamba bahati mbaya sheria zetu hazitambui uchawi upo, jambo linalozifanya kura za maoni zilizozinduliwa wiki iliyopita na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kutokuwa na mguu wa kisheria wa kusimamia.
Hapa kilichobaki ni kufurahisha roho zetu kwa ‘kuwalamba visogo’ ndugu zetu albino ili waamini tatizo lao lipo mbioni kutatuliwa. Pia tupo nao pamoja.
Kama kura za maoni zina lengo la kutoa dodoso kwa makachero wa polisi ili wawachunguze hao waliopigiwa kura nyingi, je, huo si wajibu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Jeshi la Polisi?
Lini Idara hiyo ya Upelelezi inayoongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, ilikiri haina dodoso za kutosha au uwezo wa kuzipata, hivyo kwamba tuisaidie kwa kupiga kura za maoni?
Aidha, tujiulize huyu aliyepiga marufuku waganga wa kienyeji wakati akijua hawa ndio wenye dodoso zote, hakuwa mshiriki mkuu wa kuficha ukweli wa wauaji wa albino?
Kwa nini makachero wetu hawakutumia mtandao wa waganga wa jadi kupata dodoso za washiriki wa wauaji wa albino badala yake serikali ikawapiga marufuku waganga ili ukweli huo ufichike?
Mimi nadhani suala la mauaji ya albino linahitaji kwanza mabadiliko ya sheria kabla ya kukurupuka na kura za maoni. Lakini serikali imejichanganya zaidi kueleza kuwa kura hizo watapigiwa pia wauaji wa vikongwe na wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Kwa kufanya hivyo, serikali imetengeneza mkorogo wa maziwa na rangi nyeupe. Japo kuwa vyote ni vyeupe na vinafanana, lakini rangi inatumika kung’arisha, na maziwa ni kwa ajili ya matumizi ya wanyama na binadamu.
Pia hofu yangu iko palepale, hasa baada ya serikali kupewa majina ya wauza dawa za kulevya, lakini badala ya kuwashughulikia, ikawapa muda wabadili mwenendo wao kwa kuiacha biashara hiyo.
Kwa kufanya hivyo, si rais aliwapatia likizo wafanyabiashara hao? Iweje leo zihitajike kura za maoni kuwatambua watu hawa?
Mauaji ya vikongwe maeneo ya Kanda ya Ziwa, yamekuwepo tangu miaka ya 1970, lakini tangu yaibuke haijatungwa sheria wala hapakufanyika elimu ya uraia kupambana na mila za watu kuhusu wazee wanaodaiwa kuwa na nguvu za kichawi ndani ya jamii. Na kama ipo, haikutiliwa maanani.
Leo hii miaka 20, bado ni wazi serikali imeshindwa kulitafutia ufumbuzi suala hilo. Kwa hiyo, tunaiomba iache usanii wa kutudanganya kwamba inafanya jambo wakati haifanyi lolote katika matatizo hayo.
Hizo fedha za walipa kodi wanazotumia kwa ajili ya kuendesha kura za maoni, zitumike kuleta maendeleo kama kujenga shule, zahanati na swala hilo la albino lifanyiwe kazi upya ili taifa lijipange upya kupambana nalo.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 11 mwaka 2009

No comments:
Post a Comment