Header Ads

WAKILI WA MAINJINIA WA KICHINA ATAKA WAKAISHI MELINI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilishindwa kutoa uamuzi wa kupatiwa dhamana au la kwa mainjia watano ambao hivi karibuni walikamatwa wakiwa katika meli ya Tawariq iliyokuwa ikifanya uvuvi haramu katika eneo la Bahari ya Hindi, baada ya kuzuka malumbano ya kisheria toka kwa mawakili wa pande mbili katika kesi hiyo.


Washtakiwa wanaokabiliwa na tuhuma hizo ni Cai Dong Li (44), Chen Rui Hai (34),Vu Dong Liu (39), Zhao Jong (23), Zhao Hoi Gong, wote ni raia wa China.

Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwaseba, ambaye juzi alisema angelitoa uamuzi wa kutoa dhamana wa mainjinia hao leo, baada kuhoji iwapo wana vibali vya kukaa nchini, jambo lililoibua malumbano toka pande mbili za kesi

Wakili wa utetezi, Kapteni Bendera, aliinuka na kudai kuwa hati za kusafiria za washtakiwa zimechukuliwa na Jeshi la Polisi.

“Sasa nikiwaruhusu wapate dhamana washtakiwa wataenda kuishi wapi?” alihoji Hakimu huyo.

Wakili bendera alieleza kuwa iwapo wateja wake watapewa dhamana watakwenda kuishi kwenye meli kwa sababu maisha yao yote waliishi humo na meli hiyo hivi sasa inashikiliwa na polisi hivyo hawawezi kutoroka.

Kwa upande wa mawakili wa serikali, Biswalo Mganga, yeye alidai kuwa, meli ni kielelezo katika kesi hiyo na wakati wowote upande wa mashtaka utaweza kuitembelea hivyo haiwezekani washtakiwa hao kuishi kwenye meli hiyo.

Baada ya mabishano, Mwaseba aliamuru Machi 27, ndiyo siku ya kutoa uamuzi wa maombi hayo na kuamuru kwamba upande wa mashtaka katika kesi hiyo ulete hati za kusafiria za washtakiwa hao mahakamani na washtakiwa hao kurudishwa rumande.

Juzi washtakiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo kwa mara ya kwanza, wakikabiliwa na shtaka moja la uvuvi wa haramu katika ardhi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya kuwasomea mashtaka hayo, wakili wa utetezi, Kapteni Bendera, aliomba mahakama ilegeze masharti ya dhamana, ili wateja wake waweze kudhaminiwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 25 ,2009

No comments:

Powered by Blogger.