Header Ads

MRAMBA AZUIWA KUSAFIRI,MGONJA ARUHUSIWA

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake wawili ambao wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7, wamewasilisha maombi ya ruhusa ya kutoka nje ya Dar es Salaam na kurejeshewa hati zao na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Mbali na Mramba, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.

Maombi hayo ambayo yamewasilishwa na mawakili wao mbele ya Hakimu Mkazi, Henzron Mwankenja kwa tarehe tofauti, Mramba anaomba aruhusiwe kwenda jimboni kwake Rombo kuanzia Machi 4 mwaka huu na atarejea siku ya karibu na kesi.

Pia aliiomba mahakama imrudishie hati ya kitalu 446 Kawe, iliyondikwa jina la Basil Mramba na hati ya kitalu 294 iliyoandikishwa kwa jina la H.K. Senkoro ambazo zilitumika kumdhamini.

Kwa upande wa Yona ambaye maombi yake yaliwasilishwa na wakili wake, Joseph Thadayo, Februari 10 mwaka huu, anadai kutokana na amri iliyotolewa Februari mosi mahakamani hapo kwamba kiwango cha dhamana kimepunguzwa hivyo anaomba mteja wake aruhusiwe kupewa hati yake yenye namba CT57467 ya kitalu 745 na CT 57230 ya kitalu namba 745, zote zimeandikishwa kwa jina la Daniel Yona, ambazo zote zipo Block A, Makongo Juu.

“Na kwa kuzingatia masharti ya sasa ya dhamana mahakama hivi sasa inashikilia hati yenye namba CT 59935 kwa ajili ya kitalu 744 iliyopo Makongo Juu yenye thamani ya sh bilioni 2.2, ambayo inakidhi masharti ya dhamana iliyowekwa na mahakama.

Kwa upande wa Mgonja, wakili wake kutoka kampuni ya uwakili ya Kisarika, Malimu Mlola, aliwasilisha ombi la ruhusa Machi 12 mwaka huu, akiomba mteja wake aruhusiwe kwenda Kilimanjaro na Arusha kwa ajili ya kuwatembelea wazazi wake na atarejea jijini Aprili 15.

Hakimu Mwankenja alisema amekubaliana na maombi ya kurejeshewa hati Yona na Mramba, ila amelikataa ombi la Mramba la kutaka aruhusiwe kwenda jimboni kwake kwa sababu katika ombi hilo mshitakiwa huyo hajaonyesha tarehe ya kurejea.

Hata hivyo alisema licha ya kukubali ombi la Yona na Mramba kurejeshewa hati, alisema hati hizo zitarejeshwa mikononi mwao Aprili 17 mwaka huu, wakati kesi yao itakapotajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Machi 19 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.