Header Ads

TUWASHANGAE VIONGOZI WETU NA BAKORA MKONONI

Na Happiness Katabazi

GHAFLA, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza kuwaangukia wananchi. Ni jambo lililotarajiwa na wengi kutokea wakati kama huu tunapokaribia msimu wa kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Mwaka 2005, CCM ilinadi wagombea wake kwa kuwaahidi wananchi maisha bora kwa kila Mtanzania. Msemo huo ulichapishwa katika kila gazeti, ulitangazwa katika kila redio, kwenye maTV, fulana, kanga na vipeperushi mbalimbali.

Ukiacha thamani ya vipeperushi ambavyo haina shaka viligharimu mamilioni ya shilingi, viongozi wa chama hicho waliomba kura kwa kila mbinu ikiwamo ya kutoa takrima ambayo mwaka 2006 Mahakama Kuu iliitangaza kuwa ni rushwa.

Hakika msemo wa ari, kasi na nguvu mpya uliambatana na nguvu hiyo ya fedha ambazo leo tunaambiwa ni hizi za EPA na mikataba ya manunuzi ya umma na madini. Haina shaka kwamba wapiga kura wengi walidanganywa. Leo hakuna kiongozi wa kuchaguliwa wa awamu ya nne anayeweza kukwepa tuhuma kuwa alichaguliwa kwa kutumia mbinu hizi chafu.

Hakuna mwananchi aliyeyaona maisha bora miaka mitatu sasa baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, wala hakuna matumani kwamba maisha bora kwa kila Mtanzania yatapatikana katika kipindi cha miaka miwili iliyosalia.

Kwa mara ya kwanza katika histoaria ya nchi yetu, serikali iliyoingia madarakani kwa mbwembwe za kuchaguliwa ‘kwa kishindo’, viongozi wake kukumbwa na kashfa za wizi wa mali za umma, rushwa na ubadhilifu.

Kinachoonekana hapa ni kwamba serikali iliyoingia madarakani kwa rushwa haiwezi kujisafisha au kusafishika. Hii ni kwa sababu shetani anayejulikana kwa jina la rushwa aliyeweka maskani yake serikalini hawezi kuiachia pasipo serikali yenyewe kumfukuza yeye pamoja wafuasi wake kutoka serikalini.

Njia za kumfukuza shetani huyo ni pamoja na kuomba msaada wa wananchi kuikemea serikali kila pepo huyo mchafu anapoipanda kichwani kama walivyofanya katika ‘issue’ ya serikali kutaka kununua mitambo ya kuvua umeme ya kampuni ya Dowans.

Tunayoyaona sasa ya mawaziri, wabunge na madiwani kumiminika kwenye majimbo yao ya uchaguzi wakitumia nyenzo za kiserikali kupelekea misaada kwa wapigakura katika majimbo yao hayatuondoi katika hali tuliyonayo ya kuandamwa na rushwa rushwa.

Lugha za unyenyekevu kutoka kwa viongozi na kasi ya wabunge kuwatetea wananchi wao wanaodhulumiwa haki zao kupitia sera mbovu za serikali navyo havituondoi katika hali tuliyomo.

Ukitaka tushangae pamoja. Sikiliza kauli hii ya Rais Jakaya Kikwete ya kuwatetea wananchi wanaobomolewa makazi yao na kunyang’anywa ardhi zao ili kuwapisha wawekezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo bila malipo ya fidia. Rais anaibuka leo kuanza kuwatetea wapiga kura wake wakari tatizo hili analijua kabla hata hajaingia madarakani.

Anajua fika kuwa hiki ni kilio cha wananchi kila mahali nchini. Na kwa muda mrefu, serikali yetu imekuwa haijali maslahi ya wananchi wake bala ya wawekezaji na miradi yao.

Anajua kuwa umaskini wa raia unasababishwa na serikali yenyewe kwa kuwa kila mara kwa kuwalazimisha wananchi wake kuhama hama makazi yao pasipo kuwalipa fidia ya kutosha kwa ajili ya kujenga makazi mapya.

Lakini katika hali ya kushangaza, sasa wananchi wanatetewa na serikali hiyo hiyo iliyowasababishia matatizo hayo. Ili kuisadia kuondokana na shetani huyo wa kuwatesa, wananchi hawana budi kusimama kidete sasa na kushika bakora mkononi ambazo wasisite kuzitumia kuwacharaza wanaopita sasa kuwaomba kura wakati msimu wa kufanya hivyo haujafika.

Tukiwa na bakora zetu mikononi, tunapaswa kuwashangaa pia baadhi ya viongozi wanaotoka maeneo ya wafugaji walioanza kufukuta sasa kutetea haki za wafugaji, huku kukiwa na taarifa kuwa kauli zao zinatokana na baadhi yao kuwa wamiliki wa mamia ya mifugo inayoshughuliiwa sasa na serikali.

Tuwashangae kwa sababu licha ya kufahamu kuwa serikali ya CCM haina sera ya wafugaji bali ya mifugo, wao sasa wameanza kupiga kelele wa kuwatetea haki za wafugaji, hawa nao ni wasanii, ili kuwasaidia tunapaswa kucharaza bakora kama alivyofanya Albert Mnali.

Hawa ni lazima tuwacharaza kwa hasira kwa sababu wanatufanya kiini macho, ni wao waliohusika kulifanya taifa kuwa na sera ya mifugo pasipo kuwa na sera ya kuendeleza wafugaji.

Ni hawa waliosababisha kundi hili la jamii wa wafugaji kudharaulika kama ilivyo sasa, wanapojitokeza leo wakilia lia kuhusu hali za wafugaji, tujue kuwa wanalenga uchaguzi mkuu wa 2010.

Hawa wanaowalilia wafugaji leo walikuwapo wakati serikali ikiwanyang’anya wafugaji ardhi yao huko Hanang na kuanzisha mashamba makubwa ya kilimo cha ngano pasipo kuwalipa fidia wala ardhi mbadala kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao. Ni hao ambao hivi sasa wamesambaa kila mahali huko Mvomero, Ihefu na kwingineko.

Kama kushangaa, kwa wafugaji tutashangaa hadi kesho, kwa sababu tukimaliza ya huko Mvomero, tushangae ya kule Mkomazi ambako wafugaji wa eneo hilo chini ya kiongozi wao, Lakei Faru Parutu, walifukuzwa ndani ya hifadhi bila kulipwa fidia wala ardhi mbadala. Leo wanatangatanga bila kujua wapi watalisha mifugo yao.

Hawa nao tumemsikia Mbunge wao, Anna Kilango, akiwatetea na kutaka watafutiwe maeneo mbadala ya kulisha mifugo yao na wejengewe huduma za kijamii ili jamii yao iweze kujisikia kama nyingine zinavyojisikia.

Kundi jingine la jamii yetu linalopaswa kuanza kujipanga sasa na bakora zao mikononi ni la wakulima. Hili ni kundi la Watanzania wengi lakini lililosahaulika likiwa limeachwa likiishi katika lindi la umaskini wa kutupa.

Watanzania wa kundi hili kwa miaka makumi manne wamekuwa wakiahidiwa kupelekewa zana za kisasa za kilimo na katika siku za usoni, tumewasikia watawala wetu wakihubiri kuwapelekea miradi ya umwagiliaji ili waweze kuboresha kilimo chao, jambo ambalo kama limetekelezwa, sijui kama inafika asilimia 20.

Sote ni mashihidi wa jinsi hali zilivyo katika maeneo ya vijijini, hawa wanaochangia kwa kiasi kikubwa kuwaweka watawala madarakani, bado wanasota na kilimo cha jembe la mkono.

Wanavuja jasho kila uchao kwa kilimo hicho cha jembe la mkono pasipo kusaidiwa hata pembejeo za uhakika, walichabakiza ni kutegemea kudra za mwenyezi mungu ili mazao yao yaweze kustawi.

Kama wafugaji, hawa nao natamani kusikia kuwa wako tayari na bakora zao mikononi wakiwasubiri hao wanaokwenda kuwaomba kura sasa, bila kujali staili wanayoitumia kuwaendea, kama ni ya kuinama au kupiga magoti kama ishara ya kuwasihi wadodoshe chini bakora zao.

Kwa upande wa wafanyakazi, sina wasiwasi kwa sababu ninaamini wapo ambao wamekwishaanza kuwacharaza bakora wanasiasa wa aina hii, kisa ni hasira walizo nazo za kukamilika kwa mzunguko wa gurudumu la utandawazi, kwa maana ya kukamilika kwa zoezi la kurahisisha uporaji wa rasilimali zetu, viwanda na migodi na kuzimilikisha kwa wageni.

Wafanyakazi wanajitahidi hata kuicharaza bakora serikali, kwa kudai mafao zaidi kuliko kidunchu wanayolipwa kama masurufu wakati wa kustaafu.

Ninafurahi kwa sababu ninatambua wanasiasa ambao wameanza zoezi la kuwahadaa wapiga kura sasa kwa visingizo mbalimbali vikiwamo vya kuwatetea na kuwapekelea vijizawadi, huko kwa wafanyakazi hawatathubutu hata kunusa kwa vile hawa tayari wanazo bakora mikononi mwao.

Watu wa hatari ambao jamii haina budi kuwaangalia kwa macho mawili ni waandishi wa habari ambao katika uchaguzi mkuu uliopita, baadhi yao waliwalazimisha Watanzania kuamini kuwa Rais Kikwete ndiye aliyechaguliwa na Mungu kuwa rais wa Tanzania.

Walifanya hivyo baada ya kulidaka tamko la viongozi wa dini kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu, wakatumia kalamu na ndimi zao kulihuburi hilo kwa Watanzania wote, wakafanikiwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kumpeleka Ikulu.

Lakini ni waandishi hawa hawa ambao hivi sasa wameanza kumgeuka Rais Kikwete kwa kumkosoa karibu kwa kila hatua anayoichukua katika kutekeleza majukumu yake kama kiongozi mkuu wa nchi. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa baadhi ya vyombo vya habari na waandishi wa habari wameshawekwa sawa kuanza kampeni za kuirejesha serikali ya awamu ya nne madarakani.

Hawa tunapaswa kujiuliza, wanalifanya hilo kwa maslahi ya nani? Kwa nini wasijielekeza katika kazi ya kuelimisha umma zaidi na kusuburi muda wa kumpigia kampeni utakapowadia ndipo waanze kazi hiyo?

Hawa nao hawana budi kushikiwa bakora kwa sababu mapito yao katika taaluma hii si sahihi. Kinachoonekana kwao ni kuichafua taaluma hii na kuifanya w atu wanaoweza kununuliwa kwa kibaba cha unga na kumpigia chapua mwanasiasa yoyote hata asiye faa kushika madaraka makubwa ya nchi yetu.

Hawa tunapaswa kuwaambia mapema kuwa kitakachowanusuru na bakora za umma ni kujiheshimu na kulinda maadili ya taaluma ya uandishi wa habari hata ikibidi kufa njaa.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 18 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.