Header Ads

MABAHARIA WA MELI YA UVUVI HARAMU WASOMEWA MASHTAKA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE raia 32 wa kigeni ambao wiki iliyopita walikamatwa kwenye meli ya Tawariq 1 wakifanya uvuvi haramu katika Bahari ya Hindi, jana walipandishiwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam na kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Wakili wa Serikali, Biswalo Mganga akisaidiana na Michael Lwena, Prospa Mwangamila na Wakili Kiongozi wa Serikali Stanslau Boniface, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Addy Lyamuya aliwataja baadhi ya majina ya washtakiwa huku majina mwengine yakatajwa na wakalimani kutoka Ubalozi wa China na Indonesia.

Washtakiwa hao ni Naodha wa Meli hiyo, Chin Tai Hsu(61), wengine ni mabaharia, Jiojwen Chang (34), Jia Yin Zhao 26), Gexi Zhao (36), Zongmin Ma (36), Dong Liu (25), Yongiao Fang (22), Nguyen Tuan(23), Hsu Sheng Pao (55), Zhao Hanquing (39), Zho Hanging (39) ambaye wote ni wakala na raia wa China.

Wengine ni Tran Van Phuon (33), Pham Dinn Suong (31), Tran Van Thanh (23), Cao Vuong (27), Kristofer Padilla (29) raia wa Vietnam. Wengine ni Mohamed Kiki (61), Anul Mani (24) raia wa Taiwani.

Aidha, Wakili Mganga alisema washtakiwa wengine ni Jejen Priyana (22), Kuntoto Suratno (27), Tusi Ame (25), Ifan Herman Pandi (21), raia wa Indonesia, Silvano Garanes (32), Benjie Rosano (34), Ignacio Dacumos (31), Marlon Maronon (33), Jhoan Belano (34), Rolando Nacis (35) raia wa Philipins, Wakati Ali Ali Mkota (32), Juma Juma Kumu (40), Jackson Toya(39) raia wa Kenya.

Wakili Mganga alidai washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka mawili, shitaka la kwanza ni kuvua samaki bila leseni kinyume na sheria ya Uvuvi wa Samaki katika kina kirefu ya mwaka 2009.

Alidai Machi 8 mwaka huu, washtakiwa wote kwa pamoja, saa sita usiku katika ukanda wa bahari ya Hindi ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikamatwa wakiwa wakivua samaki bila leseni.

Mganga ambaye wakati akisoma shitaka alilazimika kuwapatia hati ya mashtaka wakalimani, ili waweze kuwasomea washtakiwa kwa lugha za nchi zao, alidai kuwa shitaka la pili ni kuvua samaki katika kina kirefu kinyume na sheria hiyo ya uvuvi.

Hata hivyo, washtakiwa hao ambao walikuwa awali wote walikana kutojua kiingereza miongoni mwao baada ya kuulizwa kama ni kweli au si kweli kwamba walitenda kosa hilo, walikana mashtaka yote.

Baada ya kukana mashtaka Wakili Kiongozi, Boniface alisema upande wa serikali hauna pingamizi la dhamana na aliomba mahakama iwapatie kibali cha washtakiwa wote leo wapelekwe kituo cha polisi Kati, ili wakahojiwe zaidi na Jeshi la Polisi na kuomba wafikishwe kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni.

Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Lyamuya ambaye alisema endapo washitakiwa hao wana wadhamini wawili kila mmoja wajitokeze, ili wadhaminiwe sharti ambalo lilishindwa kutimza na washtakiwa hao na kusababisha kwenda rumande. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 17 mwaka huu, itakapotajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Machi 14 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.