Header Ads

MSHITAKIWA KESI YA ZOMBE AHAMISHIWA OCEAN ROAD

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA wa 11 katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, Rashid Lema amehamishiwa katika Taasisi ya Saratani, Ocean Road, jijini Dar es Salaam kwa matibabu, imefahamika.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka ndani ya Gereza la Keko na Ocean Road, vimeihakikishia Tanzania Daima kuwa Lema alifikishwa hospitalini hapo tangu juzi.
Vyanzo hivyo vilieleza kuwa Lema amelazimika kuhamishiwa katika hospitali hiyo baada ya kubainika kuwa ana kansa ya ngozi.

“Nakuhakikishia Lema amelazwa Ocean Road tangu juzi, kwa kweli hali yake inazidi kuwa mbaya kadiri siku zinavyozidi kwenda, cha msingi tuombe Mungu ampe nafuu,” kilieza chanzo hicho.

Aidha, vyanzo hivyo vilisema kuwa tayari serikali imeimalisha ulinzi kwa mgonjwa huyo tangu alipolazwa katika Hospitali ya Muhimbili na sasa Ocean Road.
Hata hivyo jitihada za gazeti hili za kumtafuta Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk. Twalib Ngoma, hazikuzaa matunda.

Hivi karibuni Lema alizidiwa gerezani na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke, lakini siku chache baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwa ajili ya matibabu zaidi ambako alilazwa kwa zaidi ya wiki tatu sasa.

Februari 19 mwaka huu, Jaji wa Mahakama ya Rufaa ambaye anasikiliza kesi inayomkabili mshitakiwa huyo na wenzake 12, alilazimika kuahirisha kusikiliza kesi hiyo baada ya mshitakiwa huyo kushindwa kufika mahakamani kutokana na afya yake kuwa mbaya.

Lema anaelezwa kuwa ndiye shahidi muhimu kwa sababu ndiye alibadilisha sura ya kesi hiyo, kwani baada ya kutoka mafichoni alikokuwa amejificha, alimweleza mlinzi wa amani aliyechukua maelezo yake kwamba mauaji ya watu hao, yalifanyika kwenye msitu wa Pande.

Mbali na Lema, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe, SP Christopher Bageni, SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Bakari na Festus Gwasabi.

Washitakiwa hao wanadaiwa Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, waliwaua, Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi 20 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.