Header Ads

MILIONEA BALHABOU KIZIMBANI KWA WIZI

*Adaiwa kuiba mabilioni kwa njia ya mtandao
*Aunganishwa na wafanyakazi saba wa Barclays
*Golikipa wa zamani ya Yanga amwekea dhamana

Na Happiness Katabazi

MKURUGENZI Mtendaji wa Dar es Salaam Cement Muslim na mfanyabiashara maarufu wa mafuta nchini, Merey Ally Saleh (41) maarufu kwa jina la Merey Balhabou, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na kesi ya wizi wa dola za Kimarekani milioni 1.8, sawa na sh bilioni 1.4 kwa njia ya mtandao wa kompyuta, mali ya Benki ya Barclays.


Mbali na Merey ambaye ni mdogo wa Balozi wa Comoro nchini, mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Meneja Mwendeshaji wa Kigamboni Oil Co. Ltd, Abdallah Said Abdallah (48).Washtakiwa wote wanatetewa na mawakili wa kujitegemea; Martin Matunda na Walter Chipeta.

Mkuu wa waendesha mashitaka ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Charles Kenyela, akisaidiana na Mwanasheria wa Serikali, Monica Mbogo, mbele ya Hakimu Mkazi, Waliawande Lema, alidai kuwa wamebadilisha hati ya mashitaka iliyokuwa ikiwakabili washitakiwa saba ambao ni wafanyakazi wa Barclays na kwamba wanawasilisha hati mpya itakayowaunganisha washitakiwa hao wawili na kufanya idadi yao kufikia tisa.

Kenyela alidai washitakiwa hao wawili wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama kwa nia ya kudanganya kwamba Oktoba 29, mwaka jana, katika eneo lisilofahamika jijini Dar es Salaam, kwa kutumia ujanja, wote kwa pamoja walifanya udanganyifu na kuibia benki hiyo dola za Kimarekani milioni 1.08.

Alidai kuwa, kati ya Oktoba 29 hadi 30 mwaka jana, katika Benki ya Barclays, tawi la Slipway, jijini Dar es Salaam, waliiba dola za Kimarekani 80,500 mali ya benki hiyo.
Hata hivyo, hakuwasomea shitaka la pili hadi saba kwa kuwa yanawahusu wafanyakazi wa benki hiyo ambao wameunganishwa katika kesi hiyo.

Katika shitaka la nane, Kenyela alidai kuwa Oktoba 27 mwaka jana, washitakiwa kwa pamoja, kwa nia ya kudanganya, walighushi ujumbe wa kasi, wenye namba SEQ 00305, kuonyesha kwamba ujumbe huo unakwenda Kigamboni Oil Co. Ltd, kwenye akaunti namba 00181993 kwa ajili ya kuhamisha dola za Kimarekani 299,974, mali ya benki hiyo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Aidha, aliendelea kudai kuwa katika shitaka la 10 linalohusu wizi, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Oktoba 30 mwaka jana, kwa nyakati tofauti, katika Benki ya Barclays, tawi la Ohio, bila uhalali wowote, waliiba dola za Marekani 700,769.00.

Katika shitaka la 12, washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 30 mwaka jana, katika benki hiyo, tawi la Ohio, waliiba dola za Kimarekani 299,974.00.

Washtakiwa wote walikana mashitaka hayo na hakimu Lema alisema dhamana ipo wazi.
Alitaja masharti ya dhamana hayo kuwa ni wawe na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini bondi ya sh milioni 40, kila mshitakiwa kutoa fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh milioni 78, kusalimisha hati za kusafiria na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.

Alisema masharti hayo ya dhamana ni sawa na yaliyotolewa kwa washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wapo nje kwa dhamana.

Baada ya kutaja masharti hayo, wakili Matunda aliinuka na kuiambia mahakama kuwa, wateja wake wapo tayari kutimiza masharti hayo ambapo Saleh Ally Awadhi alitoa hati ya mali yenye thamani ya sh milioni 900, iliyotumika kuwadhamini washitakiwa wote wawili.

Ipyana ambaye ni dereva wa Ubalozi wa Comoro nchini na Said Awadhi ambaye naye ni mfanyakazi wa ubalozi huo, walimdhamini mshitakiwa wa pili Abdallah wakati golikipa wa zamani wa timu ya soka ya Yanga ambaye kwa sasa ni mshauri wa balozi wa Comoro nchini, Sahau Kambi na Paul Fernandez ambaye pia ni dereva wa ubalozi, walimdhamini mshitakiwa wa kwanza, Merey.

“Kwa sababu washitakiwa mmetimiza masharti ya dhamana, nawaachia kwa dhamana na mnatakiwa mfike mahakamani hapa Aprili 29, mwaka huu ambapo kesi hii itakuja kwa ajili ya kutajwa, na mtaunganishwa rasmi na washitakiwa wenzenu saba ambao wao walifikishwa mahakamani hapa Novemba 13, mwaka jana,” alisema Hakimu Lema.

Washtakiwa hao ambao ni wafanyakazi wa benki hiyo waliofikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka yao ni Winford Mwang’onda, Shubira Mutungi, Naima Saria, Upendo Mushi, Magreth Longway, Emmanuel Mukoni na Ramadhani Khamis.

Wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alitahadharisha mabenki kuwapo kwa mbinu mpya ya wizi unaotumia teknolojia ya kisasa ya kompyuta ambapo benki za CRDB na Barclyas zilishakumbwa na wizi huo.

Alisema aina hiyo ya wizi ni ngeni nchini na wahusika wanaweza kuchota fedha nyingi kuliko wizi uliozoeleka wa kughushi hundi, saini au ule unaofanywa kwa kuvamia na kupora kwa nguvu kutumia silaha za moto.

Alisema wizi huo umeanza kujitokeza zaidi kuanzia mwaka jana ambapo wezi hao wa mtandao wa kompyuta walifanikiwa kuwashawishi baadhi ya wafanyakazi wa benki na watu wa kupitisha fedha hizo kwenye akaunti zao.

Wiki chache zilizopita, iliripotiwa kuwa kikundi cha watu wachache walichukua sh bilioni 5, mali ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), kwa njia hiyo mpya ya wizi, zilizokuwa ni malipo ya kawaida kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kwa mujibu wa taarifa hizo, fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti mbalimbali ikiwamo akaunti ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ambapo ziliingizwa zaidi ya sh milioni 671 kwenye akaunti yao iliyopo katika Benki ya CRDB, tawi la Lumumba bila wahusika kujua.

Ilielezwa kuwa fedha hizo hazikuwa za TUCTA wala chama chochote chenye uhusiano nayo, na hawajawahi kufanya biashara yoyote na TTCL kuweza kulipwa kiasi hicho cha fedha.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi 6 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.