Header Ads

MAINJINIA UVUVI HARAMU WABURUZWA KORTINI

Na Happiness Katabazi

MAINJINIA watano ambao hivi karibuni walikamatwa kwenye meli ya Tawariq 1 wakifanya uvuvi haramu katika Bahari ya Hindi nao jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, na kusomewa shitaka lao.


Wakili wa Serikali, Biswalo Mganga, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Cai Dong Li (44), Chen Rui Hai (34),Vu Dong Liu (39), Zhao Jong (23), Zhao Hoi Gong, wote ni raia wa China, ambao ni mainjinia wa meli hiyo.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwaseba, Wakili huyo wa Serikali alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na shitaka moja la uvuvi haramu katika ardhi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya kuwasomea mashitaka hayo, Wakili wa utetezi, Kapteni Bendera, aliomba mahakama ilegeze masharti ya dhamana, ili wateja wake waweze kudhaminiwa.

Hata hivyo, Wakili Mganga, alieleza kuwa upande wa mashitaka hauna pingamizi, ila unashangazwa na ombi la wakili huyo kwa sababu ni lazima wakili huyo atoe uthibitisho kwamba washitakiwa hao wakidhamiwa hawatatoroka, kwa kuwa washitakiwa wote ni wageni.

Hakimu Mwaseba alisema uamuzi wa kupata dhamana au kutopatiwa dhamana kwa washitakiwa hao atauotoa leo na kuamuru washitakiwa wote waende rumande.

Mapema mwezi huu washitakiwa 32 ambao nao walikuwa kwenye meli hiyo walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shitaka la kuvua samaki bila leseni. Walikana mashitaka na kupelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo kila mshitakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 24 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.