Header Ads

WAKILI KORTINI KWA UTAPELI

Na Happiness Katabazi

WAKILI wa Kujitegemea, Ademba Gombal, wa Kampuni ya Uwakili ya Agumba ya jijini Dar es Salaam na mwenzake, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka ya kujipatia dola za Kimarekani 280,000 mali ya kampuni ya DI Abana Co.Ltd
Mbali na Gombal, mwingine ni mfanyabiashara Yusuph Nazir Khan, maarufu kwa jina la Manji Kharim Amir.


Mbele ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo, ilidaiwa na wakili wa serikali, Dereck Mukabatunzi, kuwa shtaka la kwanza ni kula njama na kutenda kosa.

Mukabatunzi alidai kuwa shtaka la pili ni kughushi katika muda usiofahamika jijini, waliwasilisha hati ya namba 186037/69 ya kitalu namba 104 iliyopo Mtaa wa Uganda, Oysterbay, jijini Dar es Salaam iliyoonyesha kutolewa Oktoba 19, mwaka 1995 kuonyesha kuwa ilikuwa ni halali na imetolewa na Wizara ya Ardhi, kitu ambacho si kweli.

Alidai shtaka la tatu linalomkabili mshtakiwa wa tatu, ni kuwasilisha hati isiyo halali ambayo inaonyesha Desemba 31 mwaka jana, katika Kampuni ya Uwakili ya Gombal iliyopo Mtaa wa Nkurum.

Alidai kuwa shtaka la nne ni kuwasilisha hati za uongo kwa mshtakiwa namba moja kwamba Desemba 31, mwaka jana, katika ofisi za wakili huyo, huku mtuhumiwa akijua kuwa si halali, aliwasilisha hati hiyo kwenye kampuni ya DI Abana Co Ltd kwa Stika.

Aidha alidai shitaka la tano ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kuwa tarehe hiyo washtakiwa walijipatia dola za Kimarekani 280,000 baada ya kumdanganya Stika, kwamba wamemuuzia eneo hilo ambalo limeonyeshwa kwenye hati huku wakijua wanafanya udanganyifu.

Washtakiwa wote walikana mashtaka na hakimu alisema ili mshtakiwa apate dhamana, alitakiwa awe na wadhamini wawili ambao watasaini dhamana ya dola milioni 10 na kila mshtakiwa alitakiwa kutoa fedha taslim au hati ya mali yenye thamani ya dola milioni 70.

Hata hivyo washtakiwa walishindwa kutimiza masharti na kurudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapokujatajwa tena.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 25,2009

No comments:

Powered by Blogger.