Header Ads

MAGUFULI:MELI ILIYOKAMATWA INA TANI ZAIDI YA 200

*Wahusika wafikishwa kortini, washindwa kusomewa mashitaka

Happiness Katabazi

WAZIRI wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, John Magufuli, amesema meli ya Tawariq 1 iliyokamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita ikifanya uvuvi haramu katika Bahari ya Hindi, inakadiriwa kuwa na tani 200 za samaki.

Magufuli, alieleza hayo jana alipofanya ziara ya kuangalia kazi ya upakuaji wa samaki katika meli hiyo, bandarini Dar es Salaam.

Alisema wahusika walipokamatwa walieleza kuwa ni tani 70, lakini kutokana na upakuaji unavyoendelea, wamebaini kuwa samaki waliopo ni wengi na kwamba mpaka sasa waliopakuliwa ni wachache ukilinganisha na waliobaki.

“Mpaka jana usiku (juzi) zilikuwa zimepakuliwa tani 96, na hizo zilizopakuliwa ni ndogo kuliko zilizoko ndani. Tumekuta mayai na matezi ya papa, samaki aliyepigwa marufuku kuvuliwa, ambapo kilo moja ya papa ni zaidi ya dola 20.

“Hii ni meli moja tu, inaweza kuwa na tani zaidi ya 200 na katika bahari yetu, zinaonekana zaidi ya meli 200 zikivua samaki, hivyo kwa miaka 50 iliyopita, tungekuwa matajiri wakubwa, ambao tungeweza kuwa wafadhili kwa nchi nyingine,” alisema Magufuli.

Aliwataka wanasheria kukaa chini na kuhakikisha kesi dhidi ya meli hiyo inakwenda mahakamani na wanashinda kwa kuwa adhabu yake ni faini ya sh bilioni 20, kutaifishwa au vyote viwili.

Alisema kazi ya upakuaji itaendelea hadi hapo samaki hao watakapokwisha, na kwamba samaki hao wanaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu, hata kama kesi hiyo ikichukua hata miaka mitano.

Wakati huohuo, Waziri Magufuli alisema juzi meli nyingine iliponea chupuchupu kukamatwa baada ya kukimbilia ukanda wa Kenya ilipoona ndege ikifanya doria katika eneo hilo.
“Juzi, kidogo tukamate meli nyingine, tulituma ndege ndipo ikakimbia ikatoka nje ya eneo letu. Wameshabonyezana,” alisema Magufuli.

Katika hatua nyingine, watu 32 waliokamatakwa kweye meli hiyo, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, lakini walishindwa kusomewa mashitaka kutokana na kukosekana kwa wakalimani.

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana saa sita mchana, huku wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi waliokuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Mkumbo.

Baada ya kufikishwa mahakamani, walikalishwa kwenye mahakama ya wazi hadi saa sita alasiri bila kupandishwa kizimbani. Baadaye Wakili wa Serikali, Prospa Mwangamila aliwaeleza waandishi wa habari kwamba wameshindwa kuwapandisha kizimbani kwa sababu baadhi ya wakalimani wameshindwa kufika mahakamani.

“Hatuwezi kuwapandisha kizimbani hadi kesho (leo) kwa sababu hadi sasa wamekuja wakalimani toka ubalozi wa China na Indonesia, wakalimani toka ubalozi wa Philipines, Vietnam na Taiwan bado hawajafika, hivyo tunaahirisha hadi kesho,” alisema Mwangamila nje ya mahakama.

Baada ya muda, makachero wa polisi ambao walikuwa wametanda katika mahakama hiyo, waliwapandisha watuhumiwa hao katika basi la polisi na kurejeshwa rumande.

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Ijumaa, Machi 13 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.