Header Ads

DK.SALIM AWAFUNDA ASKARI WANAOENDA DARFUR

Na Happiness Katabazi, Bagamoyo

MSULUISHI wa mgogoro wa jimbo la Darfur nchini Sudan, Dk. Salim Ahmed Salim, amewataka maofisa na askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), wanaokwenda kulinda amani katika jimbo hilo, watimize majukumu yao bila ubaguzi.

Dk. Salim alisema hayo jana wakati akizungumza na wanajeshi 875 wanaokwenda Darfur, katika hafla ya kuwaaga iliyofanyika kwenye kambi ya Mafunzo ya Ulinzi wa Amani –Msata, wilayani Bagamayo.

“Wanajeshi mkiwa Darfur, nawaombeni sana mkafanikishe jukumu la ulinzi wa amani na kufikisha misaada ya kibadamu kwa wananchi walioathirika na vita, naamini mkizingatia haya ninayowaeleza pamoja na mafunzo mliyoyapata, mtafanikio,”.

“Darfur siyo sehemu zote zina machafuko, hivyo jukumu lenu si kwenda kupigana tu bali pia kulinda amani. Na ninataka mtambue kule mnakokwenda kuna magenge mbalimbali ya kiharifu, hivyo nasisitiza mzingatie mafunzo mliyoyapata,” alisema Dk. Salim.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kwamba haoni kutolewa kwa hati ya kukamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifaya The Hegue iliyopo Ufaransa kwa rais wa Sudan, Ally Bashir, kunaweza kuathiri kazi inayofanywa na vikosi vya walinzi wa amani, Dk Salim alisema, unaweza kuathiri kwa kiasi fulani ila hakutavuruga kazi ya walinzi wa amani.

Aidha akijibu swali kwanini Umoja wa Mataifa (UN), ulichelewa kupeleka walinzi wa amani katika jimbo hilo, Dk. Salim aliwataka wananchi watambue kuwa vita ya wenyewe kwa wenyewe historia inaonyesha huwa inadumu kwa muda mrefu lakini, alisema uchelewaji huo umetokana na uzembe wa jumuiya hiyo ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mnadhimi Mkuu wa Jeshi hilo, Luteni Jenerali, Abdurhman Shimbo alisema, wanajeshi wanaokwenda Darfur ni 875 kati yao wanawake 20 na 75 ni Waandisi wa Medani.

Shimbo alisema askari hao wakiwa Darfur, wataishi kwenye maeneo mawili ya Muhajaria na Khor Abeche.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 1 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.