Header Ads

KWANINI DOWANS?

Na Happiness Katabazi

WATANZANIA si majuha au mazezeta. Watanzania ni watu wenye utashi uliotimia na uwezo mkubwa wa kufikiri.


Ukifungua mtandao wa ‘Google’, ukauliza ni kampuni gani bora ya kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura, utaleta kampuni bora zaidi ya 50; utapata anwani, bei na kila kitu cha kitaalamu unachokitaka kuhusu mitambo hiyo.

Pili, Tanesco, ambalo ni Shirika la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiamua kupeleka yenyewe oda ya kutaka mitambo hiyo kwa makampuni hayo yanayotengeneza na kuuza mitambo, italetewa bei na kupewa garantii ya mitambo hiyo.

Hatuhitaji kampuni ya tatu ya kupewa tenda kununua jenereta, labda kama sisi Watanzania tumeleweshwa unyang’au! Kwani ni lazima mtu apewe ‘ten percent’ ndiyo tupate jenereta?

Huu ndio uzezeta na ufisadi uliopindukia ambao serikali yetu imefikishwa. Leo Tanesco inalilia mitambo ya Dowans. Je, Dowans ni mama yao?

Kwani Dowans ndiyo inayotengeneza hizo jenereta za umeme? Kama tunataka jenereta kwa nini tusinunue moja kwa moja kiwandani?

Huu ni mwaka wa tatu sasa tangu Rais Kikwete aingie madarakani; kama kweli tulikuwa tunaitaka hiyo mitambo tungekuwa tumeishaiagiza kutoka kiwandani siku nyingi na ingekuwa imeshakuja na kufungwa sehemu husika.

Leo mvua haijanyesha ndipo watu wanashikwa na kiwewe na kukimbilia viberiti vya Dowans!
Sasa imefika mahala tumruhusu Rais Jakaya Kikwete, avae u-DC wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Vijijini, Kagera, Albert Mnali, awachukue wanaoshupalia Dowans awapeleke Uwanja wa Taifa awacharaze bakora; wala hatutamlaumu sana, kwa sababu huu ni mwaka wa tatu tunajadili tatizo la umeme.

Mara tulimsikia Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, akisema tatizo la umeme lisingekuwepo kwa sababu angelileta mganga wa mvua, sasa yuko wapi mganga huyo?

Lakini Tanzania si nchi pekee Afrika isiyo na mvua; hizo nchi nyingine mvua zinapata wapi?
Tanzania tupo jirani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; nchi hiyo ina umeme unaotosha matumizi ya Afrika chini ya Jangwa la Sahara! Je, kwa miaka mitatu sasa tumeshindwa kupata umeme kutoka Bwawa la Inga, ambalo lipo Kongo?

Kama ni uzembe au uzezeta au uhujumu, basi serikali ya Kikwete imetia fora! Hayo ndiyo maisha bora kwa kila Mtanzania?

Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uongozi wake alikuwa anajenga vinu ambavyo viliwezesha kujenga gridi ya taifa; lakini cha kushangaza serikali zote zilizofuata baada yake zimebobea

katika kukodisha, hivi hazina aibu? Serikali hizi zimefikia mahali zinakodi hata kwa watu binafsi!
Serikali ya Awamu ya Pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, ilileta IPTL; Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa ilileta Net Group Solution; na Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Kikwete imeleta Richmond!

Na sasa pasipo haya imedhamiria kuleta Dowans! Kweli kwa kasi hiyo ya ‘ulaji’ tutafika? Kama huko si kula kwa mikono miwili bila kunawa ni nini?

Sisi tunachotaka: hatutaki kusikia kuhusu Dowans, kwa sababu Dowans ni mtoto wa kampuni ya kihuni ya Richmond. Mtoto wa shetani ni shetani tu; nani aliwaambia kwamba shetani anatakasika?

Kama Richmond ilikuwa ni batili, Dowans ni batili kadhalika. Kwa hiyo mkataba wa kuuza tenda ya kuleta jenereta za umeme katika Richmond na Dowans ni batili; au kununua mitambo ya Dowans, kama ndiyo nia ya Tanesco, ni kichekesho na ni batili vilevile!

Serikali inapaswa kuwaonea huruma wananchi kutokana na mateso yanayotokana na ufisadi na si kuendelea kuwatwisha mzigo wa maisha!

Tunachotaka twende tukanunue mitambo yetu kwenye viwanda vinavyotengeneza hizo jenereta sisi wenyewe.

Hatutaki mchuuzi au dalali yeyote katikati! Inaonekana kwamba tunaonekana Watanzania wote hatuna akili! Kwani ni Dowans pekee wanaopajua mitambo hiyo inapotengenezwa na kupatikana?

Hivi hakuna Mtanzania mwingine anayeweza kufika kwenye hivyo viwanda? Hawa wataalamu wa Tanesco ndio waliotuingiza kwenye matatizo ya Aggreco, IPTL na Richmond; hivi leo ndiyo wameibuka kusema tutakuwa hatuna mvua na mitambo ya Dowans ni mizuri sana!

Kibaya zaidi, miongoni mwa watu wanaotushawishi kununua mitambo ya Dowans ni Dk. Idris Rashid, ambaye ni mmoja wa watu wanaotuhumiwa kuhusika katika kashfa ya rada.

Hatuna imani naye hata kama bado hajahukumiwa na mahakama. Kwa nini tushauriwe na watu wanaotuhumiwa na ufisadi kuinunua Dowans? Hii inaingia akilini kweli?

Haya ni matokeo ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kulala usingizi wa pono kwa kushindwa kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Dk. Harrison Mwakyembe, kwa sababu hakuna mtendaji wa serikali aliyehusika kwenye kashfa ya Richmond kapelekwa mahakamani au kufukuzwa kazi.

Tunajua kuna kulindana serikalini na sasa ‘manyang’au’ walewale wamejipanga upya wanatuambia Dowans ni malaika mzuri. Sawa, wajinga ndio waliwao!

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 4 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.