Header Ads

WALIOSHTAKIWA KWA UVUVI HARAMU WAPATA MAWAKILI

Na Happiness Katabazi

MAWAKILI wawili raia wa Tanzania, wamejitosa kuwatetea raia 32 wa kigeni ambao hivi karibuni walikamatwa kwenye meli ya Tawariq 1 wakifanya uvuvi haramu katika Bahari ya Hindi.

Mawakili hao ni Elasimus Buberwa ambaye anamtetea mshitakiwa 7 na wa tisa wakati Elias Nawera anawateta washitakiwa 30 katika kesi hiyo ambayo ilifunguliwa Ijumaa iliyopita katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali Rose Chilongola ambaye alikuwa akiwasaidiana na Prospa Mwangamila mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi Addy Lyamuya waliambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo aujakamilika ila wanaiomba mahakama hiyo imruhusu mshitakiwa wa kwanza ambaye ni Naodha wa meli hiyo , Chin Tai Hsu(61),aruhusiwe kutoka gerezani kwa siku mbili ili aweze kwenye Kituo Polisi Kati kwaajili ya mahojiano.

Ombi hilo lilikubaliwa na Lyamuya na kuairisha kesi hiyo hadi Machi 27 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kuagiaza upande wa mashtaka uhakikishe tarehe hiyo wakalimani wote wanafika bila kukosa kwasababu jana alifika mkarimani mmoja toka ubalozi wa China.

Ijumaa iliyopita Wakili wa Serikali, Biswalo Mganga akisaidiana na Michael Lwena, Prospa Mwangamila aliwataja baadhi ya majina ya washtakiwa huku majina mengine yakitajwa na wakalimani kutoka Ubalozi wa China na Indonesia.

Mbali na Naodha wa meli washtakiwa wengine ni mabaharia, Jiojwen Chang (34), Jia Yin Zhao 26), Gexi Zhao (36), Zongmin Ma (36), Dong Liu (25), Yongiao Fang (22), Nguyen Tuan(23), Hsu Sheng Pao (55), Zhao Hanquing (39), Zho Hanging (39) ambaye wote ni wakala na raia wa China.

Wengine ni Tran Van Phuon (33), Pham Dinn Suong (31), Tran Van Thanh (23), Cao Vuong (27), Kristofer Padilla (29) raia wa Vietnam. Wengine ni Mohamed Kiki (61), Anul Mani (24) raia wa Taiwani.

Aidha, Wakili Mganga alisema washtakiwa wengine ni Jejen Priyana (22), Kuntoto Suratno (27), Tusi Ame (25), Ifan Herman Pandi (21), raia wa Indonesia, Silvano Garanes (32), Benjie Rosano (34), Ignacio Dacumos (31), Marlon Maronon (33), Jhoan Belano (34), Rolando Nacis (35) raia wa Philipins, Wakati Ali Ali Mkota (32), Juma Juma Kumu (40), Jackson Toya(39) raia wa Kenya.

Wakili Mganga alidai washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka mawili, shitaka la kwanza ni kuvua samaki bila leseni kinyume na sheria ya Uvuvi wa Samaki katika kina kirefu ya mwaka 2009.

Alidai Machi 8 mwaka huu, washtakiwa wote kwa pamoja, saa sita usiku katika ukanda wa bahari ya Hindi ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikamatwa wakiwa wakivua samaki bila leseni.Na washtakiwa wote walikana mashtaka na wapo rumande kwaajili ya wameshindwa kutimiza masharti dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 11 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.